Eric Njoka: Mimi ni mwandishi lakini nahifadhi maiti Kenya, na naipenda kazi yangu

Bw Njoka ni mtangazaji wa habari

Watu hufanya kazi nyingi za pembeni na kwa sababu nyingi, baadhi kujiongezea pato na wengine kutokana na kuipenda kazi fulani au kutaka kutoa mchango wa jamii.

Lakini tafakari hili, kwenye runinga kila siku unamtazama mtangazaji wako umpendaye akiwa amevalia nadhifu, suti na tai na sauti ya kumtoa nyoka pangoni.

Anakupasha kuhusu yanayojiri ulimwenguni, lakini wakati hayuko kazini anahusika katika kuwaandaa maiti kwa safari ya mwisho duniani.

Ni mfanyakazi katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Haya ndiyo maisha ya Eric Njoka, mmoja wa watangazaji mashuhuri katika kituo cha televisheni cha K24, moja ya vituo vikuu nchini Kenya.

Kama mwanahabari, yeye ni mpevu, mbunifu na mwenye pia kupewa sura na sauti yenye kwenda sambamba na mahitaji ya kuwa kwenye runinga.

Licha ya hayo bwana huyu ana upande mwingine wa maisha ambao umewashangaza wengi, na kuwafanya baadhi kumuangalia na jicho la pembeni .

Hii ni kutokana na kuwa katika siku za hivi karibuni alivunja kimya chake na kutangazia ulimwengu kuwa yeye ana uzoefu mkubwa wa kuhudumia maiti .

Ameeleza BBC kwamba kwa muda mrefu hakutaka watu wajue kuwa yeye ana tajriba ya kazi hiyo.

Bw Njoka alihisi watu watamuogopa na pia kumuangalia kwa njia isiyo ya kawaida.

Kwa miaka zaidi ya mitano Eric Njoka amekuwa anatenga wakati wake hususan wakati anapokuwa hayuko kazini, kama mtangazaji na kuvalia sare nyeupe mfano wa aproni kama mhudumu wa maiti.

Aliingiaje katika kazi hii?

Mwanahabari huyu anasema kuwa babake marehemu aliwahimiza wanawe wote wawe na taaluma zaidi ya moja katika maisha yao.

Kwa hivyo alipojenga hospitali pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya, babake Njoka aliwalazimisha wanawe kuhudumu pale na kuwapa mafunzo mwenyewe. Babake mwanzoni hakutana ajihusishe na kazi ya uanahabari. Alitarajia kwamba angemrithi katika kazi hiyo ya chumba cha kuhifadhia maiti.

Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Bw Njoka akiwa kazini kwenye ufuo

"Lilikuwa wazo la baba yangu kuwa nisaidie katika kazi ya kuhudumia maiti, pindi nilipomaliza shule ya upili ilinibidi niungane na babangu marehemu ili anifundishe jinsi ya kuandaa na kuhifadhi maiti kabla ya mazishi," anasema.

Aidha Njoka anasema kuwa mwanzo mwanzo wa kufanya kazi ile, alikuwa na wasiwasi na hofu kuhusu jinsi ya kuosha mwili wa marehemu japo anasema kuwa kwa sasa hana wasiwasi wala hofu yoyote.

Anasema kuwa kinachompa hofu huwa wakati anapotakiwa kuhudumia maishi ya watoto wadogo, kutokana na kutekwa na hisia na huruma.

"Mimi ninawapenda watoto sana, kwa hivyo ninapohudumia watoto katika mochari mimi huwa na huzuni kuliko kawaida," anasema.

Vile vile hofu nyengine huwa wakati anapohudumia maiti ambazo zimechomeka, au waliouawa kwa njia isiyo ya kawaida.

Je, picha za maiti huwa hazimujii kwenye akili yake anaposoma habari au kutekeleza shughuli zake nyingine?

Njoka anasema: "Nimejifundisha kuangazia jambo mmoja ninalolifanya wakati huo, kwenye akili yangu sipendi kushikilia mambo mengi kwa wakati mmoja kwani yanaathiri utendakazi wangu. Huwa sitatiziki."

Japo Njoka anasisitiza kuwa moja ya mambo yanayomchochea yeye kutenda kazi ile pia ni ile hali ya kutoa motisha kwa vijana , anasema kuwa katika karne hii tunayoishi vijana wengi wanapoteza muda wao mwingi katika mitandao ya kijamii na kujisahau.

Ndiposa anatoa nasaha kwa kila kijana kufanya kazi yoyote ile, 'bora muda wako usipotee bure'.

Haki miliki ya picha HISANI

Pia Njoka anapingai dhana ya kuwa wenye kuhudumu kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti huwa ni walevi wa kupindukia na wavutaji bangi ili kujibana kwenye mawazo ya kuwa kazi yao ni yenye kuogofya.

Mwanahabari huyu anasema kuwa kazi ya kuhudumia maiti sio mbaya kwani huwa ni safari ya mwisho ya binadamu, kila mmoja ataipitia.

Anaogopa kifo?

"Naam Ndio mimi naogopa kifo kama binadamu yeyote yule. Sijui nitakapokufa lakini sipendi kufikiria sana kuhusu hayo, ninaishi maisha yangu kila siku kwa nyengine."

Mmojawapo ya kumbukumbu nzito katika kazi ya kuhudumia maiti iliyomgusa zaidi ilikuwa hali ya yeye na ndugu yake kuhudumia mwili wa baba yao marehemu.

Anasema kuwa ilikuwa wakati mgumu sana kwake, kukosa kuamini kuwa mzazi wake hayuko tena duniani.

Na wakati mamake alipoaga, yeye pamoja na nduguze walishindwa kuhudumia mwili wake na walimpeleka sehemu nyingine kwa kukosa nguvu za kutosha kuhimili kifo chake.

Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Bw Njoka akiwa kazini

Njoka amesema kuwa ataendelea kufanya kazi ya uanahabari kwa kuwa ni kazi aipendayo pamoja na kuwa ana kipaji cha utangazaji.

Kadhalika, ataendelea kuwa muhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti kama njia ya kuendeleza biashara aliyoianzisha babake marehemu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii