Mo Dewji: Tajiri mkubwa Afrika Mashariki atekwa Dar es Salaam

Mo Dewji Haki miliki ya picha Mo Dewji
Image caption Mfanyabiashara tajiri Tanzania,Mo Dewji

Mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji ,ametekwa leo alfajiri wakati alipokuwa akielekea mazoezini, vyombo vya usalama nchini Tanzania vimethibitisha.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mo alifika katika hoteli moja ya kifahari katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam kama ilivyo ada yake kila siku alfajiri kwaajili ya kufanya mazoezi ya viungo.

Hatahivyo, punde aliposhuka tu kwenye gari yake, watu wasiofahamika walijitokeza na kufyatua risasi hewani kisha kumnyakua mfanyabiashara huyo na kutokomea nae kwenye gari lao.

BBC imefanya mazungumzo na Kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam kwa njia ya simu, Lazaro Mambosasa ambaye amesema wamepata taarifa hiyo na wanaifuatilia.

"Tumepata taarifa juu ya tukio hilo na polisi wanalifuatiria kwa karibu"Mambosasa aeleza.

Waziri wa Muugano na Mazingira Tanzania Januari Makamba ambaye ni rafiki wa karibu wa Mo Dewji ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa amezungumza na baba mzazi wa Mo ambaye amethibitisha kuwa mfanyabiashara huyo ametekwa.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda amesema vyombo vyote vya usalama viko kazini na watu takribani watatu wamekamatwa ila kwa muonekano wa haraka ni kwamba wazungu wawili ndio waliomteka Mo Dewji hivyo sio raia wa Tanzania ,hivyo kama sio raia msako utapita kote ijulikane walipita wapi na wanakaa wapi.

Mo Dewji mbali na biashara pia ni mwanasiasa na amekuwa mbunge wa Singida Mjini kwa miaka 10 mpaka alipoacha mwaka 2015.

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba ya Tanzania.

Kwamujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha na utajiri, Mo mwenye umri wa miaka 43 ndiyo tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia tajiri mdogo zaidi Afrika.

Kwa mujibu wa jarida hilo, Mo anautjiri wa dola bilioni 1.5.

Mada zinazohusiana