Celestine Egbunuche: Mfungwa mkongwe zaidi Nigeria aomba kusamehewa hukumu ya kifo

Paul and Celestine Egbunuche Haki miliki ya picha Global Society For Anti-Corruption
Image caption Paul na Celestine Egbunuche wamekua jela kwa miaka 18

Mfungwa anayekabiliwa na hukumu ya kunyongwa Celestine Egbunuche ametajwa kuwa "mfungwa mkongwe" zaidi wa Nigeria licha ya shinikizo za kutaka aachiliwe huru.

Ana miaka 100 na ameishi jela miaka 18 baada ya kupatikana na hatia ya kupanga mauaji.

Anaonekana akipepesa macho huku akiangalia juu kwa mawazo japo ameketi kwenye ubao ndani ya chumba cha wageni wa jela.

Akiwa amevalia fulana nyeupa na suruali fupi, anainua kichwa chake taratibu kama ishara ya kuitikia uwepo wetu.

Hata hivyo amekuwa kimya wakati wa ziara yetu ukimlinganisha na wafungwa wengine katika chumba hicho cha wageni katika gereza kuu la Enugu lililopo kusini mashariki mwa Nigeria.

Mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 41, aliyekaa karibu na yeye ndiye anayezungumza kwa niaba yake.

Yeye pia amekuwa gerezani kwa mashtaka ya mauaji.

Wote wawili wanatuhumiwa kwa kuwakodisha watu kumteka nyara na kumuua mtu mmoja kwa madai ya mzozo wa ardhi katika jimbo la Imo.

Paul anashikilia kuwa hawana hatia.

Wamezuiliwa tangu mwezi Juni mwaka 2000 na hatimae kuhumiwa kifo mwaka 2014.

Haijakua rahisi kuwasiliana na familia ya mtu aliyeuawa - hata wahudumu wa magereza nchini Nigeria hawajafanikiwa kuwapata.

'Kuchanganyikiwa na kukaa kama mtoto'

Huku maafisa wa gereza wakifuatilia mazungumzo yake, ananiambia kwamba baba yake hawezi kujieleza kwa sababa hata hana uwezo wa kufahamu mazingira yake.

"Ukimuuliza kitu hiki, anakujibu kitu kingine. Daktari wameniambia hali hiyo imetokana na umri wake, amekuwa kama mtoto mdogo.

Image caption Wananchi wengi wa Nigeria wanazuiliwa jela kwa miaka mingi wakisubiri kufunguliwa mashtaka

Paul anasema kuwa hapendi kukaa mbali na baba yake; amekuwa akimtunza tangu afya yake alipoanza kuzorota akiwa jela.

Matatizo ya kiafya yanayo mkabili ni pamoja na kisukari na kupoteza uwezo wa kuona vizuri - na Paul anasema kuwa anafanya kila analoweza kumsaidia.

"Kile ninachofanya kumsaidia ni kuhakikisha anapata chakula kizuri, na wao [maafisa wa gereza] wanampatia dawa."

Picha ya siku ya kuzaliwa

Baba na mwana wanaishi katika seli moja na wafungwa wengine walio hukumiwa kunyongwa, ambao wametenganishwa na wafungwa wengine.

"Nikiamka asubuhi, napasha maji moto na kumuogesha,,"

Paul pia, anasema kuwa anambadilisha nguo na kisha kumuandalia chakula.

Wakifungua seli yetu namtoa nje kuota jua.

"Kila wakati nakuwa karibu kusema nae na kucheza nae."

Paul anaongeza kuwa wafungwa wengi wanataka babake aachiliwe huru.

Mzee Egbunuche alipofikisha umri wa miaka 100 Agosti 4 ndio kampeini ya kushinikiza kuachiliwa kwake zimeshika kasi.

Picha ya Paul na mzee Egbunuche anayomuonyesha akiwa mnyonge ilisambaa mitandaoni mwezi Agosti baada ya gazeti moja kuchapisha taarifa kwamba amefikisha miaka 100 akiwa jela.

Picha hiyo ilizua mjadala mkali kuhusu muda mrefu wanaokaa jela wanaigeria waliyohukumiwa kunyongwa na nafasi ya hukumu hiyo kwa jumla.

Takwimu za mamlaka ya magereza nchini Nigeria zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 2,000 wanakabiliwa na hukumu ya kifo na wengi wao wameishi jela kwa miaka mingi wakisubiri kunyongwa.

Si sana hukumu ya kifo kutekelezwa nchini Nigeria.

Kati ya mwaka 2007 na 2017 ni watu saba tu waliyo nyongwa - Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International hukumu ya mwisho ya kifo ilitekelezwa mwaka 2016.

Umasikini naadhabu

Hata hivyo hukumu ya kifo bado hutolewa na majaji kwa makosa kama vile uhaini, utekaji nyara na wizi wa mabavu.

Wakili Pamela Okoroigwe anasema " Visa vya watu ambao wameishi jela miaka 30 wakisubiri kunyongwa ni vya kawaida,"

"Magavana hawataki kutia saini [waranti ya kifo] na hawako tayari kutoa msamaha- hii ndio sababu kuna idadi kubwa ya wafungwa walio hukumiwa kunyongwa."

Bi Okoroigwe anasema hukumu ya kifo ni "adhabu kwa watu masikini" na idadi kubwa ya wananchi wa Nigeria wanataka ifutiliwe mbali.

Anauliza ..."Ushawahi kumuona mtu tajiri akikabiliwa na hukumu ya kifo?"

"Ni watu wangapi wanaweza kumudu gharama ya kumchukua wakili atakaye wawakilisha mahakamani? Bila shaka mtu mwenye pesa ana uwezo wakujinasua katika mtego wa mauti na hatimae kuwa huru."

Hoja hii inaungwa mkono na Franklin Ezeona, rais wa shirikisho la kimataifa linalopinga ufisadi ambayo imewasilisha kesi ya mzee Egbunuche mahakamani, ikitaka asamehewe makosa na kuachiliwa huru kwa maslahi ya umma.

Bwana Ezeona anasema "Iwapo mzee huyu angelikua mzazi wa mtu mashuhuri, sidhani angelikua bado yuko jela,".

"Umasikini katika mataifa mengi ya Afrika huwanyima watu haki."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hatima ya Celestine Egbunuche sasa iko mikononi mwa Gavana Rochas Okorocha

'Kila mmoja anastahili kupewa nafasi ya pili maishani'

Franklin Ezeona anasema kuwa ana matumaini kesi ya Egbunuche itaifanya serikali kuangalia upya kesi zingine na kutafakari upya mfumo mzima wa sheria nchini.

" Naamini kila mmoja anastahili kupewa nafasi ya pili."

Mzee Egbunuche huenda akasamehewa na kupewa nafasi ya pili maishani baada ya mkuu wa sheria wa jimbo la Imo Miletus Nlemedim kupendekeza aachiliwe huru.

Pendekezo hilo linasubuiri kuidhinishwa na Gavana Rochas Okorocha.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii