Kangi Lugola: Waziri wa ndani Tanzania asema Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu visa vya utekaji

Lugola amewahakikishia Watanzania kwamba Jeshi la polisi nchini linaendelea kufanya kazi Haki miliki ya picha KAJUNASON
Image caption Lugola amewahakikishia Watanzania kwamba Jeshi la polisi nchini linaendelea kufanya kazi

Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amewahakikishia Watanzania kwamba Jeshi la polisi nchini linaendelea kufanya kazi katika kuchunguza visa vya utekaji nyara.

Lugola amezungumza kwa mara ya kwanza tangu kutekwa kwa mfanyabiashara tajiri nchini Tanzania Mohammed Dewji siku ya Alhamisi ambaye mpaka sasa hajapatikana.

Kufikia sasa waziri Lugola ameeleza kwamba watu 20 wamekamatwa, katika uchunguzi huo kuhusu kutekwa kwa Mo Dewji.

Kuna maswali kadhaa ambayo yamekuwa yakijitokeza toka iliporipotiwa kutokea kwa tukio hilo Alhamisi alfajiri na kupatikana kwa majibu yake kunaweza kukatoa mwangaza wa kulielewa tukio lenyewe na pengine kupelekea kupatikana kwa tajiri huyo.

Baadhi ya maswala hayo ni, Kwanini ametekwa? Nani amemteka? na Kwanini hakuwa na mlinzi?

Akihotubia vyombo vya habari mchana huu mjini Dar Es Salaam, waziri Lugola amesema uchunguzi wa jeshi la polisi umebaini sababu za kuwepo kwa matukio ya uhalifu ni pamoja na shughuli za siasa, wivu wa mapenzi pamoja na visasi.

Aidha ameeleza kwamba kwa mwaka 2018 watu 21 walitekwa na kufikia sasa 17 wamepatikana wakiwa hai huku polisi ikiwa bado inaendelea kuwatafuta wengine waliosalia.

Amewahakikishia Watanzania kwamba jeshi la polisi linaendelea kufanya kazi likishirikana na vyombo vingine vya usalama nchini kutekeleza wajibu wake licha ya 'udhaifu wa hapa na pale'.

Lugola amesema swala la hofu linastahili kuondolewa miongoni mwa Wananchi Tanzania.

Kuhusu matukio ya utekaji, Waziri amesema kwamba pamoja na kujitokeza kwa matukio haya, jeshi linaendelea kuyashughulikia na kuwa wanakusanya taarifa mbali mbali za kiintelijensia zinazohusiana na matukio ya utekaji watu.

Kangi Lugola: Waziri 'mwiba' Tanzania

Huwezi kusikiliza tena
Kangi Lugola: Mbona imechukua muda kuwabaini wasiojulikana Tanzania?

Ameendelea kutaja ufanisi wa jeshi la taifa akitaja mfano wa mwaka 2016 ambapo kulikuwa na matukio ya watu 9 kutekwa kati yao amesema watu 5 walipatakina kwa ushirikiano wa taarifa kutoka kwa wananchi.

Mo Dewji ni nani?

Mohammed Dewji, maarufu kama Mo Dewji, ni mmoja wa wafanyabiashara wanaofahamika sana kutoka nchini Tanzania.

Ni bilionea ambaye ametambuliwa kuwa miongoni mwa mabilionea wa umri mdogo zaidi Afrika.

Ni mfanyabiashara na mwanasiasa ambaye pia amewekeza katika kandanda na pia katika shughuli za hisani.

Anafahamika kwa unyenyekevu na huwa mara nyingi haandamani na walinzi kama ilivyo kwa wau mashuhuri.

Mo alizaliwa tarehe 8 Mei mwaka 1975, ikiwa na maana kwamba kwa sasa ana miaka 43.

Alizaliwa eneo la Ipembe, Singida maeneo ya katikati mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Haki miliki ya picha MO DEWJI

Ni wa pili miongoni mwa watoto sita wa Gulamabbas Dewji na Zubeda Dewji.

Alisomea elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Arusha na baadaye akasomea elimu ya sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam.

Alihamishiwa Marekani kwa masomo zaidi ya sekondari katika jimbo la Florida mwaka 1992.

Alisomea chuo kikuu cha Gerogetown jijini Washington DC na kuhitimu mwaka 1998 akiwa na shahada ya kwanza katika biashara ya kimataifa na fedha, na masuala pia ya dini. Miongoni mwa watu mashuhuri waliosomea chuo kikuu hicho ni rais Bill Clinton, rais wa zamani wa Ufilipino Gloria Arroyo, Mfalme wa Jordan Abdullah na wachezaji wa NBA kama vile Allen Iverson na Patrick Ewing.

Baada ya kufuzu, alirejea Tanzania na kuanza kushiriki katika usimamizi wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) iliyoanzishwa na babake miaka ya 1970.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii