Lulu Jemimah: Apata nusu ya ada Oxford baada ya kujioa Uganda

Bibi harusi aliyejioa Uganda, Lulu Jemimah. Haki miliki ya picha Lulu Jemimah

Lengo la Lulu Jemimah, 32, ni kuionesha jamii yake kuwa inawezekana kufikia malengo kimaisha bila ya msaada wa mume.

Hata baada ya kujioa mwezi Agosti mwaka huu jijini Kampala Uganda, Bi Jemimah alikuwa anachangamoto moja ya kutafuta ada ya kumalizia masomo ya uzamili.

Mwanamke huyo anasoma chuo maarufu cha Oxford, kilichopo Uingereza. Kumalizia mwaka wa pili wa masomo yake, anahitaji pauni 10,194.

Alitumia ndoa yake hiyo, ambayo baadhi ya watu, wanaiona kama kituko kufanya kampeni mtandaoni ili kupata usaidizi wa kulipa ada hiyo.

Kampeni yake ambayo ina wiki ya pili sasa katika mtandao wa Go Fund Me imeweza kufanikisha nusu ya malengo, ameshakusanya pauni 5,122 kutoka kwa watu 96 kutoka sehemu tofauti duniani.

Maisha magumu Oxford

Katika mwaka wake wa mwanzo wa masomo Bi Jemimah anasema alikumbana na changamoto nyingi za kifedha zilizomfanya aishi katika mazingira magumu.

Licha ya kuchangiwa na watu kadhaa, alishawahi kulala maktaba kutokana na kukosa pesa ya kodi ya chumba.

Haki miliki ya picha Lulu Jemimah

Anasema haikuwa dhamira yake kuomba msaada lakini hofu ya kufutwa chuo kutokana na kukosa fedha imemlazimu afanye hivyo.

"Nimepata bahati ya kuwa katika chuo bora chenye wanafunzi makini na walimu wenye weledi mkubwa...Nimefikia hapa kutokana na msaada wa marafiki na watu nisiowafahamu. Kwa mara nyingine tena naomba msaada wenu. "

Kwa nini alijioa?

Licha ya mafanikio ya kielemu kwa kujiunga na chuo maarufu duniani, anasema watu waliendelea kumuuliza swali moja ambalo kwa miaka kadhaa hakuwa analifurahia.

Swali lenyewe ni anapanga kuolewa lini, ili aanzishe familia na kupata watoto.

"Hawaamini kuwa kinachonifanya kuwa macho usiku sio hofu ya uwezekano wa kutopata bahati ya kutembea altarini kwenda kufunga ndoa."

Haki miliki ya picha Lulu Jemimah

"Nikiwa na miaka 16 baba yangu aliandika hotuba yake kwa ajili ya kuisoma siku ya harusi yangu. Kila nilipokuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa mama yangu alikuwa akiniombea, na kwa miaka ya karibuni maombi yake yalikuwa pamoja na kupata mume bora, ambaye atanifaa," amesema Bi Jemimah.

Kutokana na hali hiyo, Jemimah anasema aliamua kuchukua uamuzi wa kuwatuliza; "Nilipotimiza miaka 32 nikaamua kujioa. Naamini mimi nitajitunza na kujipa amani."

Harusi yake ilimgharimu kiasi cha dola 2 tu ambazo ni gharama yake ya usafiri. Aliazimisha gauni la harusi kwa rafiki, vito kutoka kwa dada yake na keki ya harusi iliokwa na kaka yake.

Waalikwa walitakiwa kujinunulia chakula na vinywaji kwa pesa zao wenyewe.

Mada zinazohusiana