Utaratibu mpya wa kutoa viza za Tanzania walalamikiwa

TANZANIA VIZA Haki miliki ya picha Getty Images

Tanzania imeingia lawamani kwa hatua yake ya kubadili utaratibu wa utoaji wa viza kwa baadhi ya nchi ikiwemo Nigeria.

Hivi karibuni, serikali ya Tanzania kupitia idara yake ya Uhamiaji ilitoa muongozo wa kubadili kutolewa kwa vibali vya kuingia nchini humo yaani viza.

Baadhi ya raia wa nchi ambazo awali walikuwa wanakata vibali hivyo wakiingia Tanzania, sasa wanatakiwa kuomba vibali hivyo kabla ya kusafiri, tena maombi yao yanaweza kuchukua mpaka miezi mitatu.

Baadhi ya nchi zilizoathirika na utaratibu huo ni Nigeria, Somalia, Pakistan, Yemen na Iran.

Tayari taharuki na usumbufu umewakuta baadhi ya wasafiri kutoka nchi hizo tangu utaratibu huo mpya uanze kutumika mwisho wa mwezi Septemba. Baadhi ya wasafiri raia wa Nigeria wameeleza masikitiko yao mitandaoni baada ya kuzuiwa kuingia Tanzania kwa kutoomba kibali kabla ya kuingia.

Mwandishi wa blogu ya masuala ya kusafiri kutoka Nigeria aliandika katika ukurasa wake wa twitter wiki iliyopita kuwa amezungumza na afisa mmoja wa idara ya Uhamiaji Tanzania na kumwambia kuwa raia wa Nigeri, Mali, Niger na Somalia hawana tena uwezo wa kupata kibali cha kuingia Tanzania pindi wanapofika katika mpaka wa nchi hiyo ama kutua uwanja wa ndege.

Madaktari wawili raia wa Nigeria wanaoishi Uingereza pia wamezuiliwa kuingia Tanzania hivi karibuni na kurudishwa kwenye ndege saa chache baada ya kuingia kutokana na kutoomba viza kabla.

Madaktari hao wameelezea mkasa wao kupitia chaneli yao ya mtandao wa video wa Youtube iitwayo AdannaDavid wamesema hawakuwa na taarifa ya mabadiliko ya utolewaji wa visa ya Tanzania na hata shirika la ndege waliotumia kusafiria kutoka Uingereza kwenda Tanzania hawakuwa na taarifa hiyo.

Jarida la mtandaoni la Quartz Africa kuwa mkutano wa wavumbuzi wa masuala ya mtandao wa bara la Afrika uliondaliwa na taasisi ya AfriLabs wiki iliyopita ulikumbana na kadhia ya baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kuzuiliwa kuingia Tanzania kutokana na mabadiliko hayo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Pasi ya Umoja wa Afrika ilizinduliwa Julai 2016 na inatazamiwa kurahisisha usafiri wa wakazi wa Afrika nadani na nje ya bara lao.

BBC imezungumza na msemaji wa idara ya Uhamiaji Tanzania Ally Mtanda ambaye amethibitisha kuwepo kwa mabadiliko hayo.

"Huu ni utaratibu wa kawaida tu wa utendaji wetu wa kaziā€¦sio nchi hizo tu, zipo nyengine 30 ambazo zinahitaji viza rejea. Niseme tu kuwa hawajazuiliwa kuingia Tanzania bali wanahitajika kufanya maombi ya awali...idara ya uhamiaji tunatekeleza yale ambayo serikali imeyaamua kupitia wizara ya mambo ya nje."

Alipoulizwa iwapo tishio la ugaidi ndilo lilopelekea hatua hiyo hususan kwa nchi za kiafrika kama Somalia na Nigeria ambapo kuna vikundi vya kigaidi , Mtanda alikiri hali ya usalama ni moja ya vigezo vinavyoangaliwa na kusema kuna vigezo vingine ambavyo havikuvitaja.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii na wachambuzi wa sera za uhamiaji na umajumui wa Afrika wanapinga vikali hatua hiyo ya Tanzania kuzilenga nchi nyengine za Afrika wakisema inazorotesha hatua za utengamano wa bara la Afrika.

Mataifa ya Kiafrika yalitakiwa kufutilia mbali masharti ya viza kwa wananchi wote wa Afrika kufikia mwaka 2018.

Hii ilikuwa sehemu muhimu ya makubaliano na ushirikiano wa mataifa ya Umoja wa Afrika (AU) iliyopitishwa na wanachama wote mwaka 2013.

Hadi wa leo Ushelisheli ndilo taifa la pekee barani Afrika ambalo limeweka huru masharti ya usafiri kwa Waafrika wote na raia wa mataifa hayo

Ripoti ya hivi karibuni ya AU imebaini kuwa waafrika wanaweza kutembelea 22% ya mataifa mengine ya Afrika bila viza.

Kitu pekee kinachoziunganisha nchi hizo ambazo zimeathirika na maamuzi ya Tanzania ni uwepo wa makundi ya kigaidi. Nigeria na Niger zinasumbuliwa na kikundi cha Boko Haram. Somalia kuna kikundi cha Alshabab.

Mali wanasumbuliwa na kundi la Al Qaeda tawi la jangwa la sahara na Afrika Kaskazini. Al Qaeda pia imekita mizizi katika eneo la kaskazini mwa Pakistan kwenye mpaka wake na Afghanistan. Kundi hilo liloasisiwa na Osama Bin Laden pia lipo Yemen na Syria , nchi ambazo zipo ndani ya vita vya wenyewekwa wenyewe kwa miaka kadhaa sasa.

Ingawa kuna utulivu Iran, nchi hiyo inashutumiwa kudhamini makundi ya kigaidi nchini Lebanon, Yemen na Syria.

Mada zinazohusiana