MV Nyerere mwezi mmoja baadaye: Je kuna mabadiliko na mafunzo yoyote?

Kivuko cha MV Nyerere baada ya kunyanyuliwa majini kufuatia ajali iliosababisha vifo vya zaidi ya watu 200

Ni mwezi mmoja sasa tangu kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere, huko ziwa Victoria, kaskazini magharibi mwa Tanzania , ajali ambayo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 200.

Lakini hali ya usafiri na usalama wa majini imebadilika kwa namna yoyote tangu kutokea kwa ajali hii?

MV Saba Saba ni moja ya kivuko kinachofanya shughuli yake kutoka Ukerewe hadi katika kisiwa cha Ukara, kama ilivyokua kwa MV Nyerere iliyozama mwezi mmoja tuu uliopita.

Tofauti ya sasa na mwezi uliopita ni matumizi ya maboya ya kuogelea kwa wasafiri wa kivuko hiki.

Asilimia 90 ya abiria humu wamevaa maboya ya kujiokoa kama kitatokea chochote, lakini naambiwa kuwa kabla ya ajali utaratibu huu haukuwepo kabisa, unaweza kupanda katika kivuko na hata abiria mmoja asivae boya la kujiokelea.

Huwezi kusikiliza tena
MV Nyerere: Hali ilivyo mwezi mmoja baadaye

Kuingia tu katika kivuko kama sehemu ya kujilinda kama abiria wengine, nilibeba boya langu na kulivaa kisha kuwauliza kama wao huwa wanavaa kila siku

''Hapana mimi nimeanza kuvaa baada ya ajali kutokea, kabla ya hapo sijawahi kabisa kuvaa wala kuliulizia lakini baada ya MV Kuzama hata nisipoona lazima niulize na nivae, nimejifunza sana ajali iliotekea imemgusa kila mtu sio lazima kushurutishwa sasa'' alisema Veronica mmoja wa abiria.

Baadhi ya abiria kama Yohana Mafulu wanadai kuwa maboya yalikua yanafungiwa na hawayaoni ndio maana walikua hawayavai

'' Zamani nilikua sivai kwasababu yalikua yanafungiwa sasa leo nimevaa kwasababu kutokana na hii ajali nimeamua kuomba na wameyaachia ndo mana nimevaa'' anasema Yohana.

Utaratibu ukoje wa kupata maboya katika kivuko?

Ukiingia katika kivuko kuna pande mbili ambazo zimewekwa maboya , na kila abiria hutakiwa kuchukua kisha kuvaa kabla safari haijaanza.

Lakini kuwepo kwa utaratibu huu haimanishi kila mtu anaufata, baadhi ya watu wachache ambao hawakuvaa maboya wanasema kuwa hawajaelekeza namna gani wanatakiwa wavae, jambo ambao ni kweli hakuna mafunzo ya aina yoyote yanayotelewa katika kivuko hiki cha MV saba saba.

''Sijavaa kwasababu najua mungu atanisaidia nitafika salama, lakini mimi sijawahi kufundishwa jinsi ya kuvaa, sasa nitavaa vipi , mi naona tu watu wanakuja wanachukua mimi sijui nianzie wapi'' alisema mzee Mwailo Sokolo.

Hali ikoje kisiwa cha Ukara?

Baada ya kumaliza safari hii ya masaa mawili kutoka Ukerewe hadi kufika katika kisiwa cha ukara, hali inaonekana kuwa shwari na shughuli zikiendelea kama kawaida, lakini simanzi bado haijaisha kwa baadhi ya familia zilizopoteza wapendwa wao.

Timu ya maafisa ustawi wa jamii kutoka mkoa wa Mwanza wamepiga kambi takribani mwezi mmoja sasa tangu kutokea kwa Ajali hii ya MV Nyerere , wamekua wakifanya tafiti mbalimbali na kutoa msaada ikiwemo ushauri wa kisaikolojia kwa wahanga wa ajali hii pamoja na familia zilipoteza ndugu na jamaa.

Wambura Kizito ni mmoja wa maafisa ambaye anasema kuwa hali imebadilika kidogo.

''Hapo nyuma kidogo hali ilikua mbaya, watu walipoteza matumaini kutokana kuwa wengi waliokufa katika ajali hii ni nguvu kazi ya vijana, lakini kutokana na ushauri tunaowapa kwa ngazi ya mtu binafsi na familia, wameanza kubadilika taratibu na tunaona kuwa wanarejea katika shughuli zao za kila siku'' anasema Kizito.

Ajali za majini hutokea kwa kiasi gani Tanzania

Ajali ya Mv Nyerere mwezi uliopota si kisa pekee cha ajali za majini chini Tanzania, ajali kubwa na zinazokumbukwa kuacha simanzi kwa baadhi ya familia hadi sasa, ni ikiwemo za habari ya hindi Mv Skagit na Mv Spice Islander pamoja na MV Bukoba ziwa victoria iliyosababisha vifo zaidi ya mia nane, Huku ikitajwa kuwa ajali mbaya zaidi ya karne.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii