Uchunguzi wa BBC: Gari alilotekewa Mo Dewji limesajiliwa Msumbiji

Gari alilotekewa Mo Dewji

Uchunguzi uliofanywa na BBC umebaini kuwa gari linalosadikiwa kutumika katika tukio la kumteka bilionea Mohammed Dewji nchini Tanzania lina namba za usajili wa nchi ya Msumbiji.

Mkuu wa Polisi nchini Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP) Sirro mapema leo, aliwaambia waandishi kuwa gari hilo aina ya Toyota Surf liliingia nchini Tanzania kutoka nchi jirani ambayo hakuitaja jina mnamo Septemba mosi 2018, likiendeshwa na Obasanjo Zacharius Junior.

Namba za usajili wa gari hiyo ni AGX 404 MC. Uchunguzi uliofanywa na BBC kwa kulinganisha namba za usajili wa magari wa nchi nane zinazopakana na Tanzania unaonesha kuwa namba hizo ni za Jiji la Maputo (Maputo City-MC).

Tanzania inapakana na Msumbiji kwa upande wa kusini. Nchi hiyo toka mwaka 2011 inatumia mfumo wa usajili wa namba za magari kwa alama za majina ya majimbo matano. Jimbo la Nampula alama yao ni NP, Sofala SF, Niassa NS. Maputo imegawanywa mara mbili, Jiji, Maputo City (MC) na mkoa wa Maputo (MP).

Huwezi kusikiliza tena
Gari lililotumika kumteka Mo Dewji lilikuwa na nambari za usajili za Msumbiji

Hivyo, gari ambayo polisi wanaamini lilitumika kumteka bilionea Mo Dewji katika hoteli ya Colosseum Alhamisi, Oktoba 11 linatokea nchini Msumbiji, Maputo City.

Sirro amesema kwa kutumia kanda za kamera za CCTV wamebaini kwamba gari hilo aina ya Surf baada ya kutoka hoteli ya Colosseum, lilipita barabara za Haile Sellasie, Ally Hassan Mwinyi, Maandazi, Mwai Kibaki na kisha likapotelea kwenye eneo la Mlalakuwa karibu na mzunguko wa Kawe.

"Bado watu wetu wanafuata kuona kama walielekea maeneo ya SilverSand au Kawe. Hapo tunaamini gari hilo lilipotelea, tunakwenda jumba kwa jumba kutafuta," amesema.

Katika hatua nyengine, kamanda Sirro amebainisha kuwa kati ya watu nane ambao inaendelea kuwashikilia ikuchunguza tukio hlo ni Kapteni wa boti. Lakini hakusema ni wa boti gani, na inayofanya safari zake maeneo gani, japo awali polisi walisema wameimarisha ulinzi mpaka katika bahari ya hindi kuzuia Mo kutoroshwa nchini.

Mpaka sasa bado haijajulikana sababu za Mo kutekwa na nani hasa ambao wamemteka. Awali ilidaiwa kuwa Mo ametekwa na Wazungu wawili jambo ambalo IGP Sirro alikataa kukubali ama kukanusha akisema hilo ni suala la kiupelelezi zaidi.

Familia ya bilionea huyo imetangaza zawadi nono ya shilingi bilioni 1 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Mada zinazohusiana