Jamal Khashoggi: Saudia inasema mwandishi huyo aliuawa alipojaribu kupigana

Jamal Khashoggi Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Hii ni mara ya kwanza kwa Saudia kukiri kuuawa kwa Jamal Khashoggi

Mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliuawa katika vita katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, runinga ya taifa hilo imesema ikinukuu uchunguzi wa awali.

Naibu afisa mkuu wa idara ya Ujasusi Ahmad al-Assiri na mshauri mkuu wa Mwanamfalme Mohammed Bin Salma Saud al-Qahtani walifutwa kazi kufuatia kisa hicho.

Wakati huohuo huo Uturuki imeapa kufichua maelezo yote kuhusu mauaji ya mwandishi huyo , baada ya Saudia kukiri kwa mara ya kwanza kwamba aliuawa katika ubalozi wake mdogo mjini Istanbul.

'Uturuki haitaruhusu mauaji yake kufichwa', alisema msemaji wa chama tawala cha taifa hilo.

Saudia ilisema siku ya Ijumaa kwamba Bwana Khashoggi , ambaye ni mkosoaji maarufu wa Saudia alifariki alipokuwa 'akipigana ngumi'.

Maafisa wa Uturuki awali walikuwa wamesema kuwa aliuawa kwa makusudi ndani ya ubalozi huo na mwili wake kukatwa katwa.

Mapema wiki hii maafisa wa Uturuki ambao hawakutaka kutajwa waliambia vyombo vya habari kwamba walikuwa na ushahidi wa sauti na kanda za video kuthibitisha hilo.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa kile kilichotokea hakitakubalika lakini akaongezea kuwa Saudia ni mwandani wake mkuu.

Hii ni mara ya kwanza kwa ufalme huo kukiri kwamba Khashoggi amefariki. Saudia imesema kuwa haikushiriki katika kutoweka kwa mkosoaji wake mkubwa wakati alipoingia katika ubalozi mdogo mjini Istanbull tarehe 2 Oktoba ili kutafuta vyeti vya harusi yake.

Ufalme wa Saudia ulikuwa umeshinikizwa kuzungumza kuhusu kutoweka kwa bwana Khashoggi baada ya maafisa wa Uturuki kusema kuwa aliuawa kwa makusudi ndani ya ubalozi huo na mwili wake kukatwakatwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachunguzi wa Uturuki tayari wamechunguza ubalozi wa Saudia nchini humo

Siku ya Ijumaa maafisa wa polisi wa Uturuki waliendeleza upekuzi wao hadi katika msitu mmoja jirani ambapo maafisa wasiotaka kujulikana wanaamini mwili wake ulikuwa umetupwa.

Wachunguzi wanahoji iwapo washirika wa Saudia kutoka mataifa ya magharibi wataamini madai hayo ya Saudia na iwapo itawashawishi kutochukua hatua zozote kali dhidi ya taifa hilo.

Wizara ya maswala ya kigeni nchini Uingereza imesema kuwa inafikiria kuchukua hatua baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo.

Uongozi wa Saudia sasa utatumai kwamba kukiri kwake kwa kuchelewa kwamba Khashoggi alifariki ndani ya ubalozi huo na kuchukua hatua za kuwafuta kazi na maafisa wake na kuwakamata wengine kutatosha kufinika yaliotokea.

Hi ni hatua mojawapo ya kuchapisha ukweli wa kile kilichotokea.

Kutokana na hatua ya uongozi wa Saudia kukataa kukiri kufariki kwa Khashoggi haijulikani iwapo viongozi wake wangekiri bila shinikizo ya kimataifa.

Je saudia inasema nini?

Taarifa kutoka kwa mwendesha mashtaka wa Saudia inasema kuwa vita vilizuka kati ya bwana Khashoggi , ambaye alikuwa amekosana na serikali ya Saudia na watu aliokutana nao katika ubalozi huo na kuuawa.

Uchunguzi bado unaendelea ,unasema na raia 18 wa Saudia wamekamatwa. Mamlaka ya Saudia bado haijatoa ushahidi wowote ili kuunga mkono hoja yake.

Maafisa ambao hawakutaka kutajwa waliozungumza na chombo cha reuters na New York Times anasema kuwa raia wa Saudia hawakujua kule mwili huo ulikopelekwa baada ya kupatiwa washirika wake ili kuukata kata.

Nani aliyefutwa kazi?

Saud al-Qahtani ni mtu maarufu wa ufalme wa Saudia na mshauri wa mwanamfalme Mohammed bin Salman.

Haki miliki ya picha Twiiter/@suadq1978
Image caption Saud al-Qahtani ana zaidi ya wafuasi milioni moja katika Twitter

Meja jenerali Ahmed al-Assiri ndiye msemaji mkuu wa ufalme wa Saudia kuhusu vita vya Yemen. Alizungumza na BBC mwaka 2017 kuhusu mzozo huo akitetea vitendo vya Saudia.

Mfalme Salman pia amedaiwa kuamrisha kuundwa kwa kamati inayoongozwa na mwanamfalme Mohammed, kubadilisha idara ya ujasusi.

Saudia inasema ilitumia habari zilizotolewa na mamlaka ya Uturuki ikiwa mojawapo ya uchunguzi wake kuwahoji baadhi ya washukiwa.

Je washirika wa Saudia wamechukua hatua gani?

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa kukamatwa kwa baadhi ya washukiwa ni hatua ya kwanza na kuusifu ufalme huo kwa kuchukua hatua za haraka.

Amesema kuwa maelezo yaliotolewa ni ya kweli , licha ya wabunge wengi nchini Marekani kutoamini maelezo hayo

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii