Mwanasiasa wa upinzani nchini Burundi alaumiwa kupanga njama ya kumuua Rais Pierre Nkurunziza

Pierre-Celestin Ndikumana anasema madai hayo ni njia mbaya ya kutaka kumdhulumu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pierre-Celestin Ndikumana anasema madai hayo ni njia mbaya ya kutaka kumdhulumu

Serikali ya Burundi imemlaumu mwanasiasa maarufu wa upinzani kwa kupanga njama ya kumuua Rais.

Kwenye tangazo la televisheni, wizara ya ulinzi ilisema kuwa Pierre-Celestin Ndikumana, wa muungano mkuu wa upinzani alikuwa amepanga njama na watu wengine watatu, kumuua Rais Pierre Nkurunziza, maafisa wengine wa vyeo vya juu na wabunge wawili.

Kuna hatua za kumvua kinga yake ili apate kufunguliwa mashtaka.

Bw Ndikumana anasema madai hayo ni njia mbaya ya kutaka kumdhulumu wakati serikali inaukandamiza upinzani na kuzua hali ya hofu nchini Burundi.

Ni miaka mitatu tangu Rais Nkurunziza atangaze kuwa angewani Urais muhula wa tatu, tangazo lililosababisha vurugu na kuchangia vifo vya zaidi ya watu 1,000 na wengine 500,000 kuhama makwao.

Mada zinazohusiana