Mogambi: Sababu ya vuta nikuvute kuhusu mageuzi ya katiba Kenya

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Mjadala kuhusiana na iwapo mabadiliko ya katiba yanafaa nchini Kenya ama la umeanza kuchacha na kushika.

Katika mjadala mkali unaoendelea, viongozi mbali mbali wanaonekana kubadilisha misimamo yao ya awali kuhusiana na mabadiliko ya kikatiba na kuzua maswali mengi.

Kwa muda sasa, viongozi mbali mbali nchini Kenya wamekuwa wakitoa maoni yao baada ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kutangaza kwamba mageuzi ya Katiba ya Kenya iliyoanza kutumika mwaka wa 2010, umefika.

Msingi wa msukumo anaoutoa Bw Raila Odinga ni kuwa marekebisho haya yatatoa nafasi mwafaka kwa Wakenya kushughulikia swala la utata unaokumba chaguzi za Kenya na hali inayoghubika taifa la Kenya kila baada ya uchaguzi mkuu.

Baadhi wanahoji kuwa kuna haja ya kushughulikia mfumo wa serikali ambao utahakikisha kuwa baada ya uchaguzi jamii zote nchini Kenya zitajisikia kuwa kushirikishwa katika serikali badala ya kujihisi kuwa wametengwa.

Image caption Kenya ilipata katiba mpya mwaka 2010

Aidha, kuna haja ya kupiga msasa na kuamua iwapo mfumo wa ugatuzi ambao Kenya ilichagua, na nafasi zilizopo, na jinsi pesa zinavyotumika katika ngazi ya kitaifa na kwenye kaunti unawatumikia Wakenya walio wengi ama viongozi wachache na nyadhifa nyingine nyingi zinazofaa kupigwa msasa na kufaa kwao.

Ingawa kwa muda viongozi wengi wakiongozwa na Naibu Rais wa Kenya William Ruto waliokuwa wakionekana kupinga marekebisho ya katiba, swala hili limekuwa telezi sana kiasi kwamba Bw. Ruto amekuwa akionyesha kulegeza msimamo wake siku za hivi karibuni.

Kuna wale wanaopinga kuongezwa kwa vyeo serikalini wakidai kuwa hali hii haitawanufaisha Wakenya bali viongozi wachache.

Hata hivyo, kuna upande mwingine unaodai kuwa suala la gharama si tatizo iwapo suala la ufisadi uliojaa serikalini litashughulikiwa.

Kabla ya kutangaza kwamba anaunga mkono mabadiliko ya katiba, Naibu Rais wa Kenya alikuwa akionekana kuwa aliyekuwa akiongoza upande mmoja wa wanasiasa nchini Kenya waliokuwa wakipinga marekebisho ya katiba.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bunge la Kenya

Hata hivyo, anaonekana kulegeza msimamo huo lakini kumrushia maneno kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akisema: "sisi hatuna tatizo lolote na kura ya maoni kuhusiana na marekebisho ya katiba lakini tuna tatizo na wale wanaowadanganya Wakenya kuwa walikubaliana kuhusiana na swala hili wakati wa makubaliano na Rais Kenyatta mnamo Machi 9," alieleza Naibu Rais akilegeza msimamo wake kuhusiana na kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba.

Wanasiasa kujipata njia panda

Hata hivyo, Bw Ruto alieleza kuwa ingawa sasa akiunga mkono marakebisho ya katiba, hangependa kuhusishwa katika majibizano kuhusiana na swala hili kwa kuwa alikuwa na kazi ya kufanya ya kuhakikisha kuwa ajenda kuu nne za Rais Kenyatta zinafikiwa.

Kilicho bayana ni kuwa wanasiasa wengi nchini Kenya wamejikuta katika hali ngumu ya kuamua ni upande upi wa ama kuunga au kupinga marekebisho ya kikatiba.

Suala linalotatiza hali yenyewe ni kuwa kulingana na historia ya siasa za Kenya, suala la marekebisho ya kikatiba hulandana na uchaguzi mkuu unaofuata.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Makamu wa Rais William Ruto (mwenye kofia)

Pia, siasa za marekebisho ya kikatiba mara nyingi hufungamana na uundaji wa mirengo ya kisiasa na vyama vipya.

Hivi ndivyo hali ilivyokuwa wakati wa kampeni za marekebisho ya kikatiba mwaka wa 2005 ambapo chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kiliundwa.

Aidha, wanasiasa wengi wanahofu kuwa kujitokeza waziwazi wakati huu ambapo masuala yatakayoshughulikiwa katika marekebisho ya katiba bado hayajaafikiwa kunaweza kutatiza nafasi yao katika siku za baadaye, kisiasa.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta amekuwa akiwaonya viongozi wote nchini Kenya dhidi ya kampeini za mapema za mwaka wa 2022 na badala yake kuwashauri kuzingatia utekelezaji wa ajenda zake kuu nne za maendeleo.

Ingawa mwanzoni Rais Kenyatta alikuwa ameonyesha kutopendezwa na siasa za marekebisho ya kikatiba, katika siku za hivi karibuni amekimya kabisa kuhusiana na swala hili.

Wanasiasa wengi nao wameonekana kupanga mikakati ya kuhakikisha kuwa wako kufua mbele kuhusiana na siasa za 2022.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ingawa mwanzoni Rais Kenyatta alikuwa ameonyesha kutopendezwa na siasa za marekebisho ya kikatiba, katika siku za hivi karibuni amekimya kabisa kuhusiana na swala hili.

Hali hii inayomkumba Rais Kenyatta inaweza kuwa inatokana na ukweli kwamba Rais hangependa kujiingiza katika joto la kisiasa linaloendelea kupanda kila kukicha nchini Kenya.

Hilo linaweza kumfanya kutoangazia kuhakikisha zile ajenda kuu zake nne ambazo angependa kukumbukwa kwazo zinatimizwa.

Pia, Rais Kenyatta kwa sasa yuko afisini kwa kipndi chake cha mwisho na hivyo analenga kuhakikisha kuwa anatekeleza malengo yake uongozini huku muda ukiyoyoma.

Kulingana na katiba ya Kenya, ili kufanikiwa, ili kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba, itawahitaji wale wanaopendekeza kupata uungwaji mkono wa wapiga kura asilimia 20 katika kaunti angalau 24 kati ya kaunti 47 nchini Kenya.

Katika kura ya aina hii ya mabadiliko ya katiba, ushindi wa kura moja wa upande wowote ndio utakaoamua.

Muda na gharama

Pia, lazima ikumbukwe kuwa mchakato wa kubadilisha katiba utachukua muda mrefu, gharama kubwa, wenye siasa nyingi na pamoja na kwamba unahusisha hatua nyingi pamoja na bunge la kitaifa ambapo sheria ya bunge lazima iwasilishwa katika bunge la kitaifa ama lile la seneti.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY
Image caption Upigaji kura Kenya

Ni sharti thuluthi mbili ya wabunge katika hafla kama hiyo kuunga mkono mswada kama huo pamoja na kwamba mjadala wa umma ni lazima.

Itakumbukwa kuwa katiba ya Kenya ya kwanza iliwahi kubadilishwa mara 23; ile ya Marekani imebadilishwa mara 27 na ile ya nchi ya India ikabadilishwa mara 98.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amekuwa katika mstari wa mbele katika kuitisha kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba akionyesha kuwa hili lilikuwa suala muhimu katika majadiliano na makubaliano waliyoafikiana na Rais Uhuru Kenyatta yaliyofanyika mwezi wa Machi mwaka huu ambayo hata Naibu Rais wa Kenya hakuhusishwa.

Kubadilisha huku kwa msimamo kwa Naibu Rais kunaonekana kuchanganya hali ya kisiasa nchini Kenya huku wengi wakihoji kuwa kutulia kwa hali kutasaidia mwananchi wa kawaida kuweza kuelewa mjadala wa mabadiliko ya katiba na kuweza kuchangia vilivyo kuliko ilivyokuwa hapo awali. .

Viongozi wa Kikatoliki nchini Kenya wakiongozwa na Kadinali John Njue wameunga mkono na kupendekeza marekebisho ya kikatiba ili kuisaidia nchi ya Kenya kuwa na umoja na kuponya vidonda vya awali.

Haki miliki ya picha Musalia Mudavadi
Image caption Musalia Mudavadi

Kiongozi wa Amani Naional Congress (ANC) Musalia Mudavadi ameunga mkono mfumo wa serikali wenye misingi ya bunge ili kuhakikisha usawa na ujumuishaji wa Wakenya wote kwenye serikali.

Kiongozi wa chama cha Kanu, Gideon Moi anaunga mkono mabadiliko ya katiba pamoja na mwenzake wa Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka. Wanasema kuwa huu ndio wakati wa Wakenya kuhakikisha kuwa yale yote yaliyokuwa yanawasumbua Wakenya kwa miaka ya baada ya kuwa na katiba mwaka wa 2010, yatashughulikiwa sasa.

Viongozi hawa wawili walieleza kuwa matatizo na changamoto zinazokumba Kenya zinaweza kupatiwa ufumbuzi kutokana na nafasi hii ya sasa ya kuwa na marekebisho ya katiba.

Wanasiasa kucheza karata

Wananchi wengi nchini Kenya wanaeleza matatizo ya Kenya kuwa, pamoja na gharama ya maisha kupanda kupita kiasi kwa Wakenya wa kawaida, matumizi ya juu katika viwango vya serikali za kaunti na serikali kuu,

Image caption Mkutano bustani ya Uhuru Nairobi

Ingawa msukumo wa kuibadilisha katiba ya Kenya unaonekana kuanzishswa na matamshi ya Raila Odinga, katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na mjadala miongoni mwa Wakenya kuhusiana na iwapo wakati umefika wa kufanyia katiba ya Kenya mabadiliko.

Tayari, wabunge watano wametuma maoni yao kwa bunge la kitaifa kuhusiana na mabadiliko ya kikatiba.

Mapendekezo ya kubadilisha katiba pia yametolewa na makundi ya kidini na makundi ya raia.

Kilicho bayana katika siasa za marekebisho ya kikatiba nchini Kenya ni kuwa wanasiasa wanacheza karata zao kuhakikisha kuwa maslahi yao yanalindwa huku mwananchi wa kawaida akitaka pia kuhakikisha kuwa katiba itakayokuwepo inamlinda dhidi ya viongozi wasiofaa wanaomtwika mzigo mzito.

Prof Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi@yahoo.co.uk