Mwanafunzi ashtakiwa baada ya kumtishia mwalimu silaha bandia

Waziri wa elimu wa Ufaransa Jean-Michel Blanquer Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri wa elimu wa Ufaransa Jean-Michel Blanquer akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la mwanafunzi kumtisha mwalimu

Mwanafunzi mmoja ameshtakiwa kwa kosa la kusababisha mtafaruku baada ya picha ya video ikimuonyesha akimtisha mwalimu wake silaha bandia, mjini Paris, waendesha mashtaka wameeleza.

Tukio hilo lilirekodiwa na kuwekwa mitandaoni na mmoja wa wanafunzi wenzake

Mvulana huyo mwenye miaka 15 alisema kuwa alifanya ''mzaha'' na kuongeza kuwa hakujua kama alikuwa akirekodiwa,vyombo vya habari nchini ufaransa vimeripoti.

Mwalimu huyo alipeleka malalamiko yake polisi siku ya Ijumaa.

Mwanafunzi huyo alikwenda polisi siku hiyohiyo akiwa kaongozana na baba yake.

Katika video, alionekana akimnyooshea silaha bandia mwalimu wake, aliyekuwa amekaa kwenye dawati.Alimpigia kelele akimtaka amuorodheshe kuwa alikuwa darasani.

Mwalimu aliendelea kufanya kazi kwenye Kompyuta yake huku akizungumza na wanafunzi.

Gazeti moja jijini Paris limeripoti kuwa mwanafunzi huyo alipandwa na ghadhabu kwa kuwa aliandikwa kwenye orodha kwamba hakuwa darasani baada ya kufika darasani katika shule ya Edouard-Branly akiwa amechelewa.

Tukio hilo limekemewa vikali na waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa,Christophe Castaner.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron amesema tukio hilo ''halikubaliki''.

Mkutano wa kujadili namna ya kukomesha vitendo vya ghasia shuleni utafanyika viungani mwa jiji la Paris.

Didier Sablic,amekuwa mwalimu wa shule hiyo kwa miaka 25, ameliambia gazeti la Le Monde kuwa ''hajazoea matukio ya namna hii'' , alisema wanafunzi shuleni hapo hufundishwa ''namna ya kuwasiliana na nidhamu''.

Mada zinazohusiana