Jamal Khashoggi: Saudi Arabia sasa yasema aliuawa katika operesheni isiyo rasmi

Jamal Khashoggi Haki miliki ya picha AFP/Getty

Saudi Arabia imelaumu kuwa mwandishi habari Jamal Khashoggi aliuawa katika 'operesheni isiyo rasmi', ikitoa mtazamo mwingine wa hatua iliyochangia shutuma kubwa duniani.

Waziri wa mambo ya nje Adel al-Jubeir amekiambia kituo cha televisheni cha Fox News kwamba "mauaji hayo" yalikuwa 'makosa makubwa' na amekana kwamba Mwanamfalme wa Saudia aliagiza mauji hayo.

Khashoggi alionekana mara ya mwisho akiingia katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul.

Saudia ikiwa chini ya shinikizo kubwa kueleza aliko Khashoggi, imetoa kauli za kutofuatiana.

Kauli ya Saudia ilivyobadilika

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kumekuwa na maandamano sehemu mbalimbali kudai ukweji juu ya kilichompata mwandishi Jamal Khashoggi.

Awali Saudia ilisema mwandishi huyo alitoka katika ubalozi huo akiwa mzima mnamo Okotoba 2 lakini siku ya Ijumaa ilikiri kwa mara ya kwanza kwamba amekufa, ikieleza kwamba aliuawa katika mapigano, kauli iliyokabiliwa na shaka kubwa.

Maafisa wa UTuruki wanaamini Khashoggi, mkosoaji maarufu wa serikali ya Saudia, aliuawa na kundi la maajenti wa Saudia ndani ya jengo hil na wanasema wana ushahidi kulithibitisha hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al-Jubeir amesema uchunguzi wa kina unaendelea na watatoa vielelezo vyote vinavyohitajika kwa uwazi, "ukweli ni kwamba waliofanya ukatili huu walichupa mipaka ya kazi zao. Ni Dhahiri makosa yamefanyika na makossa makubwa Zaidi ni kujaribu kuuficha ukweli."

Mamlaka za Saudia zinasema awali walitangaza kuwa Khashoggi alitoka nje ya jengo lao kwa sababu taarifa waliyopata kutoka kwa wawakilishi wao ilisema hivyo, na waliibadili mara tu walipotambua kuwa haikuwa ya kweli.

Mgahawa ambapo wateja hulipa kwa njia ya Bitcoin Kenya

Hatahivyo, Yeni Safak, kituo cha habri kilicho na ukaribu na serikali ya Uturuki, kinasema kina taarifa zinazoonyesha kuwa ofisi ya mwanamfalme ilipokea simu nne kutoka ubalozi huo baada ya mauaji.

Gazeti hilo ambalo limewahi kufichua taarifa kuhusu uchunguzi wa Uturuki kufikia sasa, limeashiria afisa wa ubalozi Maher Mutreb ametumia simu yake ya mkononi kupiga simu katika ofisi hiyo, pamoja na nambari ya Marekani inayoaminika kuwa ya kakake mdogo mwanamfalme, Khaled, aliyekuwa balozi wa Saudia kwa Marekani.

Mwanamfalme Khaled bin Salman aliondoka Marekani punde baada ya kutoweka kwa Khashoggi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mamlaka za Saudia zimekanusha Mwanamfalme Mohammed Bin Salman kuhusika katika mauaji ya Khashoggi.

Wadadisi na wakosoaji wa dola hiyo wanasema Saudia inabadili maelezo yake kutokana na shutuma zinazolekezwa kwao kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vinanukuu vyanzo kutoka ndani ya serikali ya Saudia vikisema mwanamfalme Bin Salman ameshtushwa na ukubwa wa shutuma zinaolekezwa kwa nchi yake na hakutegemea suala hilo lingelikuwa kubwa kama ilivyo kwa sasa.

Shirika la habari la Reuters limeripoti jana kuwa kiongozi mmoja wa Saudia amewaambia kuwa Khashoggi aliuawa mara baada ya kukataa kurudishwa Saudia.

Baada ya kuuawa, shirika hilo linaripoti kuwa, mwili wake uliviringishwa kwenye zulia na kupewa mshiriki mmoja wa tukio hilo ambaye ni raia wa Uturuki ili akauteketeze.

Mmoja wa washiriki wa tukio hilo ambaye ni raia wa Saudia inadaiwa alivaa nguo za Khashoggi na kutoka nje ya ofisi hizo za ubalozi ili kupoteza ushahidi.

Saudia yabanwa mbavu na mataifa yenye nguvu

Nchi tatu zenye ushawishi mkubwa barani Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimelaani vikali mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi na kuitaka Saudi Arabia kutoa ufafanuzi wa kina haraka iwezekanavyo.

Taarifa ya pamoja ya mataifa hayo yanaitaka Saudia kutoa vielelezo vya kina juu ya madai kuwa Khashoggi aliuawa wakati akijaribu kupigana ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudia jijini Istanbul, Uturuki.

Rais wa Marekani Donald Trump pia amebainisha kuwa "hakuridhishwa" na maelezo hayo ya Saudia.

Rais wa Uturuki Racep Tayyip Erdogan jana Jumapili ameahidi kudhihirisha ukweli wote juu ya tukio hilo.

Erdogan amesema atatoa maelezo juu ya sakata hilo kesho Jumanne atakapolihutubia bunge la nchi hiyo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachunguzi wanasaka msitu wa Belgrad kutafuta mwili

"Tunataka haki itendeke hapa, na juu ya jambo hili tutadhihirisha ukweli wote," Erdogan aliuambia mkutano wa hadhara jijini Istanbul.

Khashoggi aliingia katika jingo la ubalozi mdogo mnamo tarehe 2 Oktoba kwa minajili ya kushughulikia karatasi zake muhimu kuhusiana masuala ya ndoa.

Awali mamlaka za Saudia zilidai kuwa alitoka, lakini mamlaka za Uturuki zilikanusha vikali na kusema kuwa wanaushahidi kuwa mwanahabari huyo alizuiliwa na baadae kuuawa na kisha mwili wake kukatwa vipande vipande.

Uturuki: Mwandishi 'aliuawa' ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia

Khashoggi alikuwa mkosoaji kinara wa sera za Mwanamfalme Mohammed Bin Salman na alihamia Marekani mwaka 2017 akihofia usalama wake.

Katika taarifa yao ya pamoja, nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesema kuwa zimeshtushwa na mkasa huo wakiamini hakuna sababu yeyote ile ya kutetea mauaji.

"Maelezo Zaidi na yenye ushahidi usiokuwa na chembe ya shaka yanahitajika… Hivyo basi, tunataka uchunguzi wa kina ufanyike na wahusika wote watambulike na hatua za kisheria zinastohili zichukuliwe kwa waliotenda unyama huu."