Mazombi wa Mars: Mambo 11 ya kushangaza kuhusu kutafuta viumbe anga za juu

A bigfin reef squid (Sepioteuthis lessoniana) staring at the camera Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Muonekano wa viumbe kama hao utakuwaje?

Yupo mtu huko? Na kiumbe je?

Hili ni swali ambalo binadamu wamekuwa wakijiuliza kwa miaka mingi, kama wapo viumbe walio hai anga za juu.

Wanasayansi wamekuwa wakitafuta majibu mazuri ... au majibu tu.

Ni katika harakati hizi za kutafuta ukweli, ambapo kumekuwa na mafanikio makubwa, nadharia za ajabu na mambo mengi ya kushangaza.

Lakini jambo moja lnafahamika, kwamba iwapo wapo viumbe walio hai anga za juu, basi wanapatikana eneo lifahamikalo kama 'The Goldilocks Zone'.

1. Viumbe wa Mwezini

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Darubini ya Galileo ilibadilisha kabisa mtazamo kuhusu anga za juu na mfumo wa jua

Watu walipata hamu ya kutafuta viumbe anga za juu zaidi baada ya darubini mpya ya Galileo kuwawezesha wataalamu kutazama kwa undani yaliyokuwemo anga za juu mapema mwanzoni mwa karne ya 17.

Maeneo ya rangi nyeusi yaliyoonekana kwenye Mwezi kwa kutumia darubini yaliaminika kuwa mabahari makubwa yaliyojaa maji.

Yaliitwa "maria" ambalo maana yake ni "bahari" kwa Kilatino.

Kuna uwezekano mabahari hayo yamejaa viumbe kama mabahari ya humu duniani?

Baadaye ilibainika kwamba maeneo hayo yalikuwa mabonde yaliyojaa mawe meusi ya volkano aina ya basalt, yaliyotokana na milipuko ya volkano miaka mingi iliyopita.

2. Viumbe kutoka Mars

Kukawa na viumbe wa kutoka Mars muonekano wao utakuwaje?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mars wakati wa mpambazuko

Viumbe wakawepo Mars watakuwa warefu, kwa wastani, kuliko binadamu wa kawaida. Hii ni kwa mujibu wa mtaalamu wa anga za juu William Herschel aliyesema hivyo miaka ya 1870.

Kwa kutumia darubini yenye nguvu sana, alipima ukubwa wa Mars, pamoja na urefu wa misimu na siku zake.

Sayari hiyo ni ndogo kidogo kuliko Dunia, kwa hivyo nguvu mvuto zake ni za chini kidogo, alisema Herschel. Hii ina maana kwamba kukawa na viumbe kama binadamu huko watakuwa wa kimo kirefu, kwani hawavutwi sana na nguvu mvuto za sayari.

3. Viumbe wa Saturn

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mfumo wa jua, kuanzia kwa jua hadi kwa sayari ya Neptune

Mwanafalsafa Immanuel Kant alidai kwamba werevu wa viumbe wa anga za juu ungekuwa unawiana na urefu wa sayari yenyewe kutoka kwenye jua. Hivyo, viumbe wa Mercury au Zebaki wangekuwa wapumbavu, nao wale wa Saturn wawe werevu ajabu.

4. Unaweza kuwahesabu viumbe wote?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Karakana ya darubini: Galileo akionyesha jinsi ya kutumia darubini yake kwa baadhi ya wataalamu karne ya 17

Mwaka 1848, kasisi wa kanisa la Kiskotchi ambaye pia alikuwa mwalimu wa sayansi, Thomas Dick, alijaribu kufanya hesabu ya idadi ya viumbe wa anga za juu wanaoishi kwenye Mfumo wa Jua.

Alibashiri kwamba iwapo idadi ya viumbe anga za juu inatoshana na idadi ya watu England, kwamba kuna watu 280 kwa kila eneo la ukubwa wa maili moja mraba, basi Mfumo wa Jua una viumbe 22 trilioni..

5. Maisha kwenye Miezi

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mabahari ya Europa yana viumbe?

Pahala pazuri zaidi kuwatafuta viumbe anga za juu katika Mfumo wa Jua huenda isiwe katika sayari zilizo karibu na Dunia kama vile Mars, lakini katika miezi ya sayari za mbali, mfano Europa (mwezi unaozunguka Jupiter) na Enceladus (sayari ya Saturn).

Miezi yote ina mabahari yenye maji yanayotiririka chini ya mawe ya barafu.

Inaaminika kwamba huenda kukawa na chanzo cha joto ndani ambacho huzuia maji yote ya mabahari hayo kuganda.

Joto hilo huenda likawa linatoka kwenye kitovu cha kila mwezi, na kupitia mifereji ya chini kwa chini hadi kwenye sakafu ya mabahari hayo.

Duniani, mifereji kama hiyo huanzisha shughuli za kemikali ambazo huzalisha vyakula vinavyoliwa na viumbe wengi wa baharini.

6. Ngisi wa anga za juu

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Muonekano wa viumbe kama hao utakuwaje?

Iwapo kuna viumbe walio hai katika miezi hiyo, basi fizikia inaweza kueleza muonekano wao.

Iwapo kuna viumbe wakubwa wa baharini anga za juu, watahitajika basi kwenda kwa kasi ili kunasa windo na kuwakwepa wengine wanaotaka kuwawinda. Kwa hivyo, muonekano wao unaweka kuwa kama wa ngisi, pomboo au papa.

7. Dunia za mbali

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kunaweza basi kuwa na sayari kama dunia iliyo ya miezi na inayozunguka jua kama letu?

Wataalamu wa anga za juu wanakadiria kwamba huenda kukawa na sayari 40 bilioni zinazofanana na Dunia katika Kilimia au Milky Way ambao huwa ni mkusanyiko wa nyota ndogo nyingi sana pamoja (kama wingu jeupe) mbinguni usiku.

Walifikia idadi hiyo baada ya kupata sayari takriban 3,800 zinazokaribiana sana na Dunia katika nyota zilizo karibu.

Ukakadiria kamba hilo limeendelea katika utando wote wa anga za juu, basi zinafikia mabilioni.

8. Dalili za uhai

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maputo ya hewa yaliyokwama chini ya ziwa la barafu. Yakapatikana katika sayari za mbali, itakuwa dalili ya uhai?

Utatafutaje uhai anga za juu? Wanapochunguza sayari mbalimbali, wataalamu hutafuta gesi ambazo huwa wanaziita biosignatures, au kwa kifupi dalili za uhai.

Methane hutolewa na viumbe Duniani, mchwa hadi ng'ombe, lakini pia hutolewa na volkano.

Lengo huwa ni kutambua iwapo kutapatikana gesi ya methane, pamoja na gesi nyingine kama vile oksijeni na ozoni, ambazo huzalishwa Duniani kutokana na miali ya jua.

9. Eneo la Goldilocks Zone

Goldilocks, mpo?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Goldilocks, mpo?

Tutatafuta viumbe wapi? Wanasayansi hufikiria pahali bora zaidi ni kuangazia sayari zilizo katika eneo ambalo huitwa The Goldilocks Zone au kwa kifupi tu eneo ambalo viumbe wanaweza kuishi.

Hili ni eneo ambalo haliko karibu sana na jua au nyota, kwa hivyo halina joto sana, na pia si mbali sana, maana kwamba si baridi sana.

Sayari ya karibu zaidi kama hiyo ni Proxima Centauri b - ambayo hupatikana katika eneo linaloweza kuishi viumbe katika nyota inayokaribia Jua zaidi.

10. Kusafiri kwa jua

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mwanakosmolojia Stephen Hawking alikuwa mmoja wa wanasayansi waliounga mkono wazo la kuwa na chombo cha kusafiri anga za juu kutafuta viumbe walio hai, kwa kusafiri kwa kazi ya asilimia 20 ya kasi ya mwanga wa jua

Mpango wenye ndoto kubwa wa kufikia mfumo huo wa nyota, uliofahamika kama Breakthrough Starshot, ulizinduliwa 2016.

Ulifadhiliwa na mwekezaji na mwanafizikia Mrusi Yuri Milner, kwa lengo la kuunda chombo cha kusafiri anga za juu kisichoweza kuharibiwa na jua. Chombo hicho kingesafiri kwa kasi asilimia 20 ya kasi ya mwanga.

Mpadi huo ukifanikiwa, basi vyombo hivyo vya usafiri vinaweza kuchukua miaka 20 kufikia Proxima Centauri b na miaka mingine minne kutuma data na taarifa kwenye Dunia.

11. Viumbe werevu

Wataalamu wa anga za juu wanaamini huenda kukawa na viumbe wanaoishi maeneo yasiyo na chochote, au kwenye nyota kubwa sana - au kwenye kitovu cha Kilimia.

Haki miliki ya picha Getty Images

Viumbe ambao wamekuwepo kwa maelfu au mamilioni ya miaka kabla yetu wanaweza kuwa na werevu wa hali ya juu na pengine ufanisi wa kiteknolojia.

Huenda wasiwe dhaifu na wanyonge, au wawe wanahitaji kuwa kwenye eno linaloweza kutosheleza uhai ndipo waendelee kuishi. Si lazima wawe wanategemea maji na oksijeni.

Baadhi ya wataalamu wa anga za juu wanaamini teknolojia hiyo inaweza kuwawezesha viumbe kama hao kuishi maeneo yenye kiwango cha juu sana cha kawi na joto.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii