Jamal Khashoggi na uhusiano wa familia yake na Kenya

Jamal
Image caption Kashoggi alitoweka akiwa ndani ya ubalozi wa Saudia nchini Uturuki

Taarifa kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi maarufu aliyeangazia taarifa kubwa kwa mashirika tofuati nchini Saudia, zimetawala vichwa vya habari duniani.

Khashoggi alitoweka baada ya kuingia katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul mnamo Oktoba 2, sehemu ambayo maafisa wa Uturuki kuanzia mwanzo walidai kwamba aliuawa.

Saudi Arabia ilikana kuwa na ufahamu wowote wa kilichomsibu.

Baadaye ilikiri kwamba aliuawa lakini wakasema aliuawa akipigana na makachero waliokuwa wakimhoji na kutaka kumsafirisha hadi Saudia.

Siku chache baadaye tena, wakabadilisha kauli na kusema aliuawa na watu 'wahalifu' ambao hawakuwa wamepewa maagizo yoyote kutoka serikalini.

Khashoggi ni nani hasa?

Jamal Ahmad Khashoggi, 59, alizaliwa Medina, Saudi Arabia, moja ya miji mitakatifu zaidi katika dini ya Kiislamu.

Alienda ng'ambo kwa masomo katika Chuo Kikuu cha Indiana, Marekani na akafuzu na shahada ya kwanza katika uanahabari mwaka 1983.

Kazi yake ya kwanza ilikuwa kuwa meneja wa maduka ya vitabu ya Tihama Bookstores 1983 hadi 1984 na baadaye akawa mwandishi wa gazeti la Saudi Gazette na naibu meneja wa jarida la Okaz kuanzia 1985 hadi 1987.

Kuanzia 1991 hadi 1999, alifanya kazi kama mwandishi ya mashirika ya habari za kigeni Afghanistan, Algeria, Kuwait, Sudan, na Mashariki ya Kati.

Familia ya watu maarufu na uhusiano wao na Kenya

Khashoggi alitoka katika familia maarufu sana na yenye ushawishi Saudi Arabia.

Ni mjukuu wa Muhammad Khashoggi, daktari mzaliwa wa Uturuki ambaye alimuoa mwanamke Msaudia na alihudumu kama daktari wa kibinafsi wa Mfalme Abdulaziz Al Saud, mwanzilishi wa ufalme wa Saudi Arabia.

Jamal Khashoggi ni binamu wa Adnan Khashoggi, mfanyabiashara maarufu wa Saudi Arabia aliyehusika katika ununuzi na uuzaji wa silaha, ambaye alihusishwa na kashfa ya silaha ya Iran-Contra. Adnan Khashoggi alihusika kama wakala katika mwafaka huo uliohusisha kusalimishwa kwa mateka na badala yake kukabidhiwa kwa silaha kwa watekaji.

Kufikia miaka ya 1980, Adnan Khashoggi alikuwa na utajiri ambao ulikuwa unakadiriwa kuwa na thamani ya jumla ya $4 billion.

Bw Khashoggi alikuwa na biashara kadha nchini Kenya ambapo alikuwa pia na uhusiano wa karibu na aliyekuwa Rais Daniel arap Moi miaka ya themanini.

Alinunua Mount Kenya Safari Club mwaka 1967 ana baadaye akanunua Ranchi ya Ol Pejeta katika jimbo la Laikipia kaskazini mwa Nairobi ambapo anadaiwa kutumia $7.5 milioni (thamani sawa na Sh750 milioni za Kenya kwa sasa) kujenga jumba la kifahari ambalo hadi wa leo hufahamika kama Jumba la Khashoggi.

Ol Pejeta baadaye ilichukuliwa na Tiny Rowland aliyemiliki hoteli za Lonrho ambaye baadaye aliiuza. Anadaiwa kukabidhi Mount Kenya Safari Club kwa mwanawe kama zawadi wakati wa kusherehekea kutimiza miaka 18.

Haki miliki ya picha AFP

Adnan Khashoggi, alifahamika sana na jamaa zake kama AK na alifariki akiwa na miaka 81 akitibiwa ugonjwa wa Parkinson jijini London.

Ingawa familia hiyo ni ya asili ya Uturuki, Adnan aliwahi kudai kwamba babu yake alikuwa Myahudi.

Dadake Adnan Khashoggi ni mwandishi maarufu Samira Khashoggi ambaye aliolewa na mfanyabiashara Mohamed Al-Fayed na wakajaliwa Dodi Fayed.

Hii inamfanya Dodi kuwa binamu wa Jamal Kashoggi.

Dodi Fayed alikuwa anachumbiana na Princess Diana wa Uingereza wawili hao walipofariki katika ajali ya barabarani mjini Paris mwaka 1997.

Uhusiano wake na Osama bin Laden

Aliunda urafiki na Osama bin Laden katika miaka yake ya kwanza alipoanza kuwa mwandishi habari na alifahamika kama mzaliwa maarufu wa Saudia aliyelazimika kutoroka nchi hiyo.

Walifahamiaka miaka ya '80 na '90 Osama alipokuwa anaongoza mapigano dhidi ya Muungano wa Usovieti nchini Afghanistan. Alimhoji Osama mara kadha, sana wakikutana Tora Bora na kuna wakati waliwahi kukutana Sudan.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanamfalme Mohammed bin Salman amekosolewa kuhusiana na kutoweka kwa mwanahabari Jamal Khashoggi

Kipindi hicho alishirikishwa na majasusi wa Saudia katika kujaribu kumshawishi Osama amalize tofauti zake na familia ya kifalme ya Saudia.

Kabla ya kutoweka kwake katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, uhamisho wa kibinfasi wa Khashoggi ulimlazimu kuishi baina ya Marekani, Uingereza na Uturuki.

Aliondoka Saudi Arabia mnamo Septemba 2017, baada ya kukosana na maafisa katika ufalme wa nchi hiyo.

Haki miliki ya picha Getty Images

Akiwa uhamishoni, alikuwa akiandikia gazeti la Washington Post Marekani makala kali za kuukosoa utawala wa Saudia, na pia katika akaunti yake ya Twitter ambako alikuwa na wafuasi zaidi ya milioni 1.6.

Wanawe na watoto

Kufikia wakati wa kifo chake Khashoggi alikuwa anapanga kumuoa Hatice Cengiz, mwanamke mwenye miaka 36 anayesomea shahada ya uzamifu katika chuo kikuu kimoja cha mjini Istanbul.

Wawili hao walikutana Mei 2018, wakati wa kongamano lililoandaliwa mjini Istanbul.

Khashoggi, ambaye alikuwa ni raia wa Saudia alikuwa ametembelea ubalozi wa nchi hiyo Istanbul kupata stakabadhi za kumruhusu kufunga ndoa na Cengiz.

Khashoggi alikuwa ameoa na kutaliki wanawake watatu.

Kutoka kwenye ndoa yake ya kwanza na Rawia al-Tunisi walijaliwa wana wawili wa kiume na mabinti wawili.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii