Dawa mpya ya inayotajwa kuleta mabdailiko makubwa katika vita dhidi ya TB

Mtoto akipewa dawa ya TB Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mtoto akipewa dawa ya TB

Madaktari nchini Belarus wamefanikiwa kutibu zaidi ya 80% ya aina moja ya ugonjwa wa kifua kikuu sugu kwa kutumia mchanganyiko wa dawa mpya inayojulikana kama bedaquiline, pamoja na dawa zingine za antibiotiki.

Belarus imetajwa kuwa taifa lenye viwango vya juu vya maradhi ya kifua kikuu sugu.

Kwa mujibu wa shirika la Afya duniani(WHO) takriban watu milioni 2.5 waliambukizwa maradhi ya TB barani Afrika mwaka 2016 hii ikiwa ni robo ya visa vipya vya ugonjwa huo kote duniani.

Shirika hilo linasema mataifa saba duniani yalikadiria 64% ya visa vipya vya TB mwaka 2016, India ikiongoza kataka mataifa hayo ikifuatiwa na Indonesia, China, Philippines, Pakistan, Nigeria, na Afrika Kusini,

Dr Paula Fujiwara - kutoka shirikisho la kimataifa la kukabiliana na magonjwa ya Kifua kikuu na mapafu ameiambia BBC kuwa kupatikana kwa dawa mpya ya bedaquiline ni hatua kubwa katika harakati ya kutafuta tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Image caption Dawa za kifua kikuu

Lakini je Kupatikana kwa dawa hii kutasaidiaje katika vita dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ama TB barani Afrika?

Dr Kamene Kimenye, Mkurugenzi wa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu Nchini Kenya anasema dawa ya bedaquiline imekuwa ikitumika kwa karibu mika mitatu sasa.

Pamoja na kuwa ni dawa mpya ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu kikamilifu kwa sababu vimelea vinavyousababisha havijaizoea.

Dr Kamene pia anasema, ''Kenya tumetumia dawa ya bedaquiline kwa wagonjwa 30 na mataifa mengine pia katika bara la Afrika kama vile Afrika kusini na Ethiopia zimekua zikitumia''

Hivi karibuni Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali walipitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kuchagiza hatua dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, au TB unaosababisha vifo vya watu milioni 1.6 kila mwaka.

Azimio hilo linalofahamika kama "Ushirikiano wa kutokomeza TB: Hatua ya dharura ya kimataifa," linalenga kutafuta hatua ambayo itachangia kutokomezwa kwa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, ambayo pia ni ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Viongozi hao walisema kuwa wametambua changamoto zilizopo ikiwemo ukosefu wa vifaa, dawa sahihi na hata fedha, bila kusahau jinsi ambavyo TB inasababisha umaskini miongoni mwa familia, jamii na taifa.

Haki miliki ya picha Science Photo Library

Msingi wa azimio hilo ni upi?

  • Kutambua kuwa usugu wa dawa za TB unakadiriwa kusababisha theluthi moja ya vifo vitokanavyo na usugu wa dawa duniani
  • Malengo ya maendeleo endelevu yako mashakani kufikiwa ikiwa mataifa yatashindwa kushughulikia tatizo la usugu.
  • Ugonjwa wa Kifua Kikuu umelemaza utu wa binamu kwa miongo na bado unaendelea kutesa binadamu.
  • TB imetajwa kuwa inachochewa na mizozo, njaa na umaskini huku mazingira hayo nayo yakitajwa kuchochea kuenea kwa ugonjwa huo hatari.

Kwa mantiki hiyo viongozi hao wameazimia pamoja na mambo mengine kutenga fedha zaidi za utafiti na kusaka dawa sahihi sambamba na kuhakikisha hakuna mtu yeyote mwenye TB ambaye hatofikiwa na upimaji na matibabu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza hatua ya kupitishwa kwa azimio hilo lenye vipengele 53, akisema lina matarajio makubwa lakini mafanikio yake yatafikiwa iwapo jitihada za pamoja zitawekwa kwenye takwimu bora na sayansi, maamuzi sahihi, kuwezesha jamii na hatua za kimkakati na zilizofadhiliwa.

Ametaja changamoto kama vile usugu wa dawa akisema kila mwaka wagonjwa 600,000 wanakabiliwa na usugu wa tiba dhidi ya TB, "tunahitaji maendeleo ya kisayansi ili kupata mbinu bora zaidi za kukabiliana na TB, sambamba na tishio la ongezeko la usugu wa dawa za kuua vijiumbe maradhi."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ladha tamu ya dawa ya TB kwa watoto inasaidia katika tiba ya ugonjwa huo kwa watoto

Bwana Guterres amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kufuata mwongozo wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus na shirika lake katika kuchagiza usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa serikali na mashirika ya kiraia na wadau wengine ili kupata kasi inayohitajika kutokomeza TB duniani.

Kwa upande wake Dkt. Ghebreyesus ametaja mambo matatu muhimu ambayo yanaweza kusaidia kufikia lengo la kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.

- Msaada usiotikisika wa wadau wote utakaofanikishwa na ungwaji mkono na viongozi wa ngazi ya juu kabisa.

- Uwekezaji hasa katika sayansi na utafiti, dawa mpya, chanjo mpya na mbinu mpya za utambuzi wa TB.

- Jukumu la kila mtu kumwajibisha mwenzake.

Dkt. Ghebreyesus amesema "Ndio maana tunaandaa mfumo wa uwajibikaji ulio mtambuka ukiwa na misingi mikuu minne: Ahadi, hatua, ufuatiliaji na tathmini kuhakikisha kuwa kile tusemacho kinaenda sambamba na tunachotenda."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii