Tanzania Albinism Collective: Albino watumia Muziki kupinga unyanyapaa Tanzania

Tanzania Albinism Collective

Chanzo cha picha, Standing Voice

Maelezo ya picha,

Bendi hiyo yenye miaka miwili tu imeshashiriki tamasha kubwa la WOMAD nchini Uingereza

Taarifa kuwahusu Albino nchini Tanzania mara nyingi zimekuwa za majonzi na kukatisha tamaa, lakini kundi moja la Albino visiwani Ukerewe lipo katika kampeni ya kipekee.

Maaalbino watano walijiunga pamoja na kuunda kundi la muziki, wanatumia sanaa katika kuelimisha jamii juu ya matatizo wanayokumbana nayo katika maisha yao ya kila siku ikiwemo unyanyapaa na na elimu ndogo na fikra hasi juu ya uwepo wao kama binaadamu wa kawaida.

Tanzania Albinism Collective ni bendi iliyoasisiwa mwaka 2016 na mtunzi na muaandaaji wa muziki kutoka Marekani Ian Brenann ambaye hujikita katika kusaidia makundi yaliyotengwa na jamii, alipotembelea kisiwa cha ukerewe katikati ya Ziwa Victoria kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Kwa msaada wa shirika la Standing Voice linalohudumia watu wenye ualbino katika kisiwa cha Ukerewe na maeneo mengine ya Tanzania, Brenann ambaye ameshawahai kushinda tuzo maarufu za Grammy alitoa wito kwa Albino wanaotaka kujtolea kuanza kuimba katika hiyo Bendi, baadhi ya Albino hao hawajawahi kuimba katika sehemu yoyote kwenye Maisha yao.

Ndani ya miaka miwili toka kuanza kufanya kazi Tanzania Albinism Collective tayari wameshaachia vibao kadhaa na kushiriki katika Tamasha kubwa la WOMAD nchini Uingereza mwezi Julai mwaka huu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kupanda ndege na kutoka nje ya Tanzania.

Chanzo cha picha, Standing Voice

Mbali na kuwa Albino nchini Tanzania wanakumbana na visa vya Mauaji na mashambulizi, lakini Unyapaa na kutengwa na jamii ni suala wanalokutana nalo kila siku,

Elias Sostenes ni mmoja wa kundi la Tanzania Albinism Collective, anasema kuwa yeye alipozaliwa ndugu wa Baba yake alimkataa na kusema kuwa ameleta laana katika Familia hiyo.

''Nilipozaliwa ndugu wa Baba hawakufurahi, walimchukia Mama kwa sababu amenizaa, walisema niliLeta laana, lakini baba yangu akawaambia mimi sio laana, bali ni zawadi kutoka kwa Mungu," anasema Elias.

Bendi hii ya muziki imekua fursa kwao kuimba na kufikisha ujumbe kiurahisi kwa jamii ambayo kuna baadhi wanaona wao si watu wa kawaida.

'' naweza kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia wimbo, nikawaelezea hali yangu , watu wenye ualbino tunaishije na tunapaswa kuishi vipi katika jamii," anasema Riziki Julius ambaye pia ni mwanakikundi.

Mauaji ya Albino yalitikisa Tanzania katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita ambapo viungo vyao vimekuwa vikitumika na waganga kwa imani potofu kuwa huvutia utajiri. Mauaji hayo pia yalitikisa Malawi kwa kiasi fulani.

Chanzo cha picha, Standing Voice

Kwa mujibu wa Shirika la Under the same Sun albino zaidi ya 70 wameuawa kutokanana na imani za kishirikina nchini Tanzania.

Lakini kwa kundi hili la Albino visiwani Ukerewe muziki umekua sehemu ya kuwafiriji kupitia nyimbo zao kama 'Tanzania ni nchi yangu pia, majonzi na amani imepotea'.