Watu wafukiwa baada ya jengo la ghorofa 8 kuporomoka Malindi Kenya

mafuriko pwani ya Kenya
Image caption Kumeshuhudiwa mvua kubwa pwani ya Kenya

Mtu mmoja amefariki na watu kadhaa wamekwama katika jengo la orofa nane lililoporomoka katika eneo la Barani Malindi pwani ya Kenya Ijumaa alfajiri.

Inaarifiwa kwamba jengo hilo liliangukia majengo yaliokuwa karibu kikiwemo kituo cha mafuta pamoja na makaazi ya watu.

Haijulikani wazi nini kilichosababisha jengo hilo kuporomoka, licha ya kwamba mvua kubwa imekuwa ikinyesha kwa siku mbili mtawalia katika eneo hilo.

Mashirika ya kupambana na majanga kama vile shirika la msalaba mwekundu yanaendeleza operesheni ya uokozi, na idadi kamili ya watu waliokwama ndani ya kifusi haijulikani.

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakaazi kufuatia mafuriko ambayo yameshuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya pwani.

Wakaazi wanazungumzia wasiwasi walio nao kufuatia mvua kubwa inayonyesha.

Katika eneo la mji wa Mombasa, barabara zilionekana kufurika maji , tatizo ambalo hushudiwa mara nyingi mvua kubwa inaponyesha kutokana na kuziba kwa mabomba ya kupitisha maji.

Hali ambayo pia imechangia kushuhudiwa kwa msongamano wa magari kwa wanaoingia na kutoka katika mji huo na viunga vyake.

Idara ya hali ya hewa nchini imetoa tahadhari ya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo, tangu kaskazini mpaka kusini mwa Pwani.

Mambo muhimu ya kuhakikisha usalama wako mvua inaponyesha

Huwezi kusikiliza tena
Mafuriko yadaiwa kuhatarisha maisha ya wakazi nchini Kenya

Maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama Barabarani (NTSA) pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wanashauri kwamba:

Wakati wa kiangazi, vumbi, mchanga na taka za aina mbalimbali hurundikana barabarani.

Mvua inaponyesha, husababisha barabara kuwa telezi na kwa hivyo ukiwa na gari ni muhimu kutoendesha gari lako kwa mwendo wa kasi kupindukia kwani gari likiteleza utashindwa kulidhibiti gari lako kwa urahisi.

Kwa sababu ya maji, huwa vigumu sana kupiga breki wakati wa mvua na hivyo hatari ya mwenye gari kumgonga anayetembea barabarani huwa juu. Unashauriwa kutoendesha gari kwa mwendo wa kasi.

Kwa sababu ya mvua, wapita njia mara nyingi hutembea wakiwa wameinamisha vichwa chini na huenda wasilione gari linapokaribia. Wenye magari wanashauriwa kuwa makini zaidi wanapofika kwenye vivuko barabarani au wanapomuona mtu akivuka barabara.

Kwa wanaotembea kwa miguu, wanashauriwa kutumia vivuko vilivyotengwa na kuwa tahadhari zaidi pia.

Kwa wenye magari, iwapo barabara imefurika maji, ni vyema kutafuta barabara nyingine ya kupitia badala ya kujaribu kupitia ndani ya maji. Huwa vigumu kukadiria kina cha maji barabara inapofurika.

Wakati mvua inaponyesha, wenye magari wanatakiwa kuwasha taa kuwawezesha kuona mbele na pia kutokaribia sana magari yaliyo mbele yao.

Maji yanayorushwa na gari lililo mbele yanaweza kutatiza mwenye gari iwapo atakuwa karibu sana.

Unashauriwa kufuata kanuni ya sekunde 3, hicho ndicho kipindi kinachochukuliwa na binadamu kuona jambo na kuchukua hatua. Usipofanya hivi, kufikia wakati unapoona aliye mbele yako amesimama na kuchukua hatua utakuwa tayari umesababisha ajali.

Breki za gari huathiriwa na maji, kwa hivyo unapoendesha gari eneo lenye maji, ni vyema kuendesha gari kwa mwendo wa polepole. Hii itaziwezesha breki kukauka.

Madereva wanashauriwa pia kutumia mikono yao miwili kudhibiti mwelekeo wa gari kuhakikisha wanadhibiti vyema gari.

Wapita njia, waendesha baiskeli na waendeshaji pikipiki wanashauriwa kuvalia mavazi yanayoweza kuonekana vyema au mavazi yanayoweza kuakisi mwanga. Haya yatamuwezesha mtu kuonekana na madereva na kumpungushia mtu hatari ya kugongwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii