Madaktari Canada kutumia michoro ya sanaa kama dawa kwa wagonjwa

A woman views contemporary pop art is on display at the Montreal Museum of Fine Arts

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Je, michoro hii inaweza kukuponya maradhi yako?

Madaktari jijini Montreal, Canada wapo mbioni kutoa dawa mpya kwa wagonjwa; michoro ya sanaa.

Chama cha madaktari na Jumba la Makumbusho ya Sanaa la Montreal (MMFA) wanashirikiana katika kuwawezesha matabibu kuwaandikia dawa wagonjwa wao ya kwenda kutazama michoro bila kiingilio kwenye makumbusho hayo.

Mkakati huo unatajwa kuwa wa kipekee na wa kwanza duniani.

Uongozi wa jumba hilo la la makumbusho unasema, "wagonjwa watapata fursa ya kupumzisha na kusisimua akili zao."

Matibabu hayo mapya yanatarajiwa kuanza kutolewa Novemba mosi.

Madaktari hao wa Montreal katika siku za mwanzo za mradi huo wataweza kutoa fursa hiyo ya matibabu mpaka kwa wagonjwa 50 kwa kila daktari kutembelea makumbusho ya MMFA kama dawa mbadala.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mchoro wa majira ya kipupwe ukiwa ndani ya Jumba la Makumbusho ya Sanaa la Montreal. Mchoro ni sehemu ya kazi za sanaa zitakazotumika kama dawa mbadala.

Mkurugenzi Mkuu wa MMFA Nathalie Bondil, ambaye ni kinara wa mradi huo anaamini kuwa manufaa ya njia hiyo mbadala ya tiba yataonekana na kukubaliwa na jamii kwa ujumla hivi karibuni.

Bi Bondil ameiambia BBC hivi karibuni kuwa, "mazingira tulivu, mazuri na yenye kuvutia ya makumbuso yanaweza kuchochea kufikiria vyema na kuwawezesha wagonjwa kutafakari nje ya maradhi yanaowasumbua."

Anaamini mafanikio ya mradi huo yatavutia majumba mengine ya makumbusho duniani kuiga na kuboresha huduma zao.

"Tunaweza kufungua milango mipya ya fursa si tu kwa wagonjwa na pia kwa madaktari," amesema.

Kiongozi wa chama cha madaktari , Dkt Hélène Boyer, amesema kuna tafiti nyingi ambazo zinaonesha kuwa kazi za sanaa zinaweza kuwa na taathira njema kwa wagonjwa.

"Nina hakika kuwa wagonjwa wangu watafurahia kwenda makumbusho kupunguza maumivu yao bila kupata athari yeyote (ya kiafya, kama itokeavyo baada ya kula baadhi ya dawa)."

Madaktari wanaweza kuwapa tiba hiyo mbadala wagonjwa wa aina mbali mbali ikiwemo wenye matatizo ya akili.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hoja ya "sanaa ni matibabu bora", kama Jumba la Makumbusho la Montreal linavyodai inapata ufuasi mkubwa ulimwenguni.

Mwaka 2017, kundi la Wabunge nchini Uingereza lilitoa ripoti inayotaka kuthaminiwa kwa nguvu kubwa ya sanaa katika matibau ya binaadamu. Ripoti hiyo ilitaka Uingereza kuanza kutumia njia hiyo kama tiba mbadala kwa haraka iwezekanavyo.