Full Combat Jerrycan: Kanisa la walevi Turkana kaskazini magharibi mwa Kenya

  • Faith Sudi
  • BBC Swahili
Waumini

Kanisa la Full Combat Jerrycan ni kanisa linalohudhuriwa na walevi katika kijiji cha California mjini Lodwar, kaskazini mwa Kenya.

Kanisa hili ambalo ibada hufanyika chini ya mti, waumini wake huhudhuria wakiwa walevi wa pombe za kienyeji, inayojulikana kama Kaada kwa lugha ya Kiturkana.

Kanisa hili lilianzishwa mwaka wa 2016 na waumini wake wote ni walevi kutoka kwenye maduka ya kuuzia pombe za kienyeji katika soko la California.

Aidha jina la kanisa hili limezua utata kwa kuwa waumini wake wanasisitiza kuwa linajulikana kama Full Combat Jerrican huku mhubiri akisisitiza kuwa ni Redeemed Gospel.

Mhubiri wa kanisa hilo Peter Ekatorot anasema kwamba alianzisha kanisa hilo wakati ambapo kijiji hicho kilijulikana sana kwa uhalifu.

"Tulianza na watu watatu wakati ambapo eneo hili lilijulikana sana. Mahali ambapo wakora sugu waliishi, walevi na mahali ambapo ugonjwa ulikuwa umekithiri sana, hata makanisa mengi yaliogopa sana. Makanisa yalikuwa yanafurushwa, watu wanamwagiwa pombe, wanatukanwa hadi ikawafanya wachungaji wengi kuogopa kuja hapa.

Mhubiri huyo anasema kuwa alifika huko baada ya Mungu kumtuma kuwahudumia 'watu wake'.

"Nilikuja nikaongea na watu moja kwa moja, halafu Jumapili ya kwanza tulipoanza, watu watatu tu pekee ndiyo walikuja. Wengine walikuwa tu wanaendelea na shughuli zao".

Hata hivyo ni kazi ambayo ilimlazimu kuwa na uvumilivu.

"Wakati tulipoanza wiki ya pili, ikawa sasa wakati tunapofanya ibada, wengine wanapigana, wanafukuzana ndani ya kanisa lakini niliweza kuvumilia nikijua ya kwamba Mungu huleta mtu mahali ambapo atakomaa".

Maelezo ya video,

Full Combat Jerrycan: Ibada huwa vipi katika kanisa hili lenye walevi wa pombe Kenya?

Waumini huanza ibada kwa nyimbo za sifa zinazosindikishwa na kupiga ngoma na mbinja na washirika.

Kanisa hili pia liko na waimbaji na Susan Akimat ni mmoja wa wanakwaya ambaye amepunguza ulevi baada ya kujiunga na kanisa hilo.

"Kwanza sisi tulikuwa walevi sana, lakini sasa tumebadilika kidogo. Hii kanisa imetusaidia, kuna wale tumebadilika kiasi, lakini wengine pia watabadilika tukiendelea. Saa zingine tunaamua kama wanakwaya kupanga nyimbo zile tutakazoimba. Tulimwambia pia mhubiri wetu atusaidie kushona sare za kwaya, ili tujulikane kama wanakwaya."

Kevin Erot ni mshirika wa kanisa hilo na anasema kwamba imemsaidia sana kumjenga kiroho na hata kumwezesha kupunguza ulevi.

"Hii kanisa imenisaidia, kwa vile ulevi nilikuwa nao, kwa ile bangi nilikuwa navuta, kwa ule uasherati nilikuwa nafanya".

Dorkas Tioko anasema kuwa kanisa limewasaidia kupunguza pombe.

"Ile pombe tulikuwa tunakunywa, tumeshakanyaga kwa sababu tuliona ilikuwa inatupeleka pabaya, lakini wengine huwa wanakufa ovyo ovyo.

"Hii kanisa ilianza na walevi wakiwa wengi lakini sasa wamepunguza ulevi. Mimi nimebadilika kwasababu nimeona hali yangu ni mbaya sana, kwasababu pombe inahatarisha maisha yangu".

Picha/David Wambundo, BBC