Historia ni mwalimu mzuri: Panda shuka ya uchaguzi mkuu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

  • Leonard Mubali
  • BBC Swahili
Kabila

Waswahili walisema safari ni hatua, siasa ni moja ya safari kwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo moja ya taifa kubwa barani Afrika.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa nchi zenye historia ndefu zilizopita mabonde na milima.Taifa hili lenye idadi kubwa ya watu wapatao milioni 84.8 sawa na asilimia 1.1 ya idadi ya watu wote duniani si haba, imejaaliwa utajiri wa madini ,misitu minene na neema nyingine zimekuwa kama maua mazuri ya mapambo ambayo huwezi chemsha na kula.

Mambo kama hayo ndiyo yanayowafanya raia wa taifa hilo kuinua mikono yao juu na kuomba kila liwezekanalo, ili taifa lao liwe na utulivu kisiasa na shughuli nyingine za kimaisha na kimaendeleo ziendelee.

Wamechoshwa na majina mapya ya wapiganaji wa msituni yanayozuka kila uchao na kuwafanya akina mama na watoto kugeuka kuwa wahanga wakubwa wa machafuko na vita hivyo vilivyo dumu kwa miaka mingi na kusababisha hali ya watu kulazimika kuikimbia nchi yao na ukizingatia kwamba nyumbani ni nyumbani kuna tamu yake.

Katika taifa lolote ambalo kwa miongo mingi limekuwa katika machafuko, suala la uchaguzi mkuu hutegemewa kuwa na matokeo chanya, katika suala zima la kuleta amani kwa wananchi ambao wanakuwa wamechoshwa na machafuko na vita, hali ambayo kwao kama wananchi wa kawaida hawana manufaa yoyote.

Jamhuri ya Demokrasia ya Congo raia wake, wameanza kuhesabu siku kuelekea uchaguzi mkuu wa taifa hilo mwezi disemba, tarehe 23 mwaka huu, ambapo kabla ya kutajwa kwa tarehe hiyo pia kulikuwa na panda shuka na mivutano ya kisiasa baina ya upinzani na chama tawala na hatimaye matumaini ya uchaguzi yakapatikana baada ya makubaliano kufikiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Jean Pierre Bemba kiongozi mkuu wa upinzani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

Maelezo ya picha,

Moise Katumbi

Wapo baadhi ya viongozi wa upinzani kama vile Moise Katumbi na Pierre Bemba,wamewekwa pembeni na vigezo vilivyopo kwa mjibu wa taratibu zao za kisiasa na sheria za nchini humo, huko sitaki kwenda zaidi,bali lengo la makala hii ni kutaka kujua taifa hili , historia yake inasema nini katika mfumo wa kupokezana madaraka,taifa lilitoka wapi na mikononi kwa akina nani pamoja na mfumo uliotumika kupokezana madaraka.

Madaraka walibadilishana vipi?

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Patrice Lumumba

Historia ya uwepo wa taifa lenyewe unaanzia mbali sana huko miaka ya 1200, ikapita mikononi mwa mfalme wa Ubelgiji Leopold wa II miaka ya 1870.

Miaka ya 1960 harakati za kujikomboa hatimaye zilianza ambapo wanasiasa kama Patrice Lumumba walianza kupambania taifa lao, Lumumba Waziri mkuu, Joseph Kasavubu rais.

Pamoja na kwamba walikuwa wakishirikiana vilivyo waziri mkuu na rais wake na kukabiliana na changamoto kama vile za Katanga kujitangazia uhuru lakini bado wao pia walifarakana, ambapo mwezi Septemba 1960, rais Joseph Kasavubu alimfukuza katika nafasi hiyo Patrice Lumumba, mwezi disemba mwaka huo huo na kawawekwa chini ya ulinzi na mwezi February mwaka uliofuata akauawa.

Historia ni mwalimu mzuri na muongozo mzuri pia waweza rejea kuchukua uzoefu ama waweza rejea kuchukua tahadhali pia. Ile kazi ya kuwakabili wale wa Katanga waliokuwa wamejitangazia uhuru sasa ilibidi ifanywe na vikosi vya umoja wa mataifa UN.

Kasavubu akamchagua Tshombe kuwa waziri mkuu baada ya kukubali kulegeza msimamo wake wa kulitanga jimbo la Katanga kama taifa huru ama eneo huru,hiyo tayari ilikuwa mwaka 1964.

Waswahili walisema ukiua kwa upanga, utauawa kwa upanga kwani mwaka 1965 Kasavubu na Tshombe waliondolewa katika mapinduzi yaliyofanywa na Joseph Mobutu Sese Seko ambaye alibadilisha jina la jimbo lililokuwa linataka kujitenga la Katanga.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mobutu Sese Seko aliitawala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyokuwa Zaire, kwa miaka 30

Lakini katika utawala wa Mobutu, mwaka 1991 ulikuwa na machafuko yaliyosababishwa na wanajeshi waliokuwa wakidai malipo yao na Mobutu akakubali muungano na wapinzani,lakini kwa masharti ya kuendelea kushikilia sekta ya ulinzi.

Mwaka 1993 makundi mawili yalizuka,lile linamuunga mkono Mobutu na lile linalompinga na mwaka mmoja baadaye Mobutu akamteua Kengo Odondo kuwa waziri mkuu,hata hivyo Mobutu akiwa nje ya nchi kwa matibabu mwaka 1996 hadi 1997,waasi wa Kitutsi wakashikilia eneo la mashariki mwa Zaire sasa Jamhuri ya demokrasia ya Congo.

Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi sema ukila nyama ya mtu kamwe huwezi kuacha,wapiganaji wa Kitutsi wakisaidia na kundi linampinga Mobutu walifanikiwa kutwaa mji mkuu Kinshasa,na hapo hapo wakabadilisha hata jina la nchi kutoka Zaire na kuliita Jamhuri ya demokrasia ya Congo Laurent-Desire Kabila akatawazwa kuwa rais.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Laurent Kabila

Kuna usemi usemao kikulacho ki nguoni mwangu,ulitimia kwa rais Laurent Kabila mwaka 2001 ambapo alipigwa risasi hadi kufa na mlinzi wake. Rais wa sasa Joseph Kabila akachukua nafasi ya baba yake na sasa anaratibu uchaguzi ujao wa mwezi disemba mwaka huu.

Historia ni mwalimu kivipi?

Chanzo cha picha, AFP

Iko wazi kwamba dunia kwa sasa inasubiria kuona uchaguzi huu wa Congo utakuwa na matokeo gani. Lakini pia ni jambo la kuleta faraja kwamba angalau taifa hili kubwa barani Afrika na lenye utajiri mkubwa unaodaiwa kwamba kwa kiwango kikubwa raia wake hawajaonja tamu na majaaliwa hayo.

Sasa historia hii ni mwalimu,kubainisha kuwa siku zote misuguano na utengano wa ndani unakuwa na matokeo makubwa ambapo hata waasisi wa taifa hili walijikuta katika harakati za kusalitiana na kupinduana, lakini kila zama na kitabu chake, ambapo kwa sasa rais wa sasa amefikia hatua ya kuwa na uchaguzi mkuu.

Umoja wa Afrika pia unapaswa kupata somo kwa historia hii na kuhakikisha inakuwa na ukaribu mkubwa na mbinu zote za amani na maridhiano zinapaswa kutumika kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa hatua ya kuelekea katika taifa lenye ukimya wa matukio ya machafuko na vita hali ambayo imekuwa ikisababisha raia kulikimbia taifa lao.

Jitihada zilizofanyika hadi kusaka amani ya Congo.

Mwaka 1999 mwezi julai, nchi sita za Afrika zilitia saini mkataba wa kusitisha mapigano mjini Lusaka Zambia, ambapo matokeo yake ni kwamba miezi michache baadaye kundi la MLC na RCD walisaini makubaliano.

Kana kwamba haitoshi baraza la usalama la umoja wa mataifa UN mwaka 2000 lilipeleka kikosi cha askari wa kulinda amani wapatao 5,500 kusitisha mapigano lakini mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Rwanda na Uganda yaliendelea.

Zipo jitihada nyingi na kubwa zilizoendelea kama mazungumzo ya amani ya Afrika Kusini mwaka 2002 na uongozi wa mpito kuelekea uchaguzi mkuu ni hatua zinazotia moyo.

Je ni mambo gani ya kuzingatiwa kuelekea uchaguzi huo.

Hadi sasa ni kwamba kambi ya upinzani wamekuwa katika mjadala wa kuangalia uwezekano wa kuwa na mgombea mmoja wa urais, hilo jema kwa sababu waswahili husema umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.

Lakini kwa jumuiya za kimataifa na na umoja wa Afrika unapaswa kugeuka nyuma na kuangalia historia ya taifa hili ili kukabiliana na kila dalili mbaya zinazochomoza ambazo zinaweza kuirejesha historia mbaya iliyopita.