Mtanzania mwanaharakati Rebeca Gyumi ashinda tuzo ya Umoja wa Mataifa

Rebeca Gyumi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rebeca Gyumi

Mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto kutoka nchini Tanzania Rebeca Gyumi, pamoja na wenzake watatu wameshinda tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2018.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa, kupitia ukurasa wake wa Twitter amewapongeza kwa mchango wao wa kusongesha mbele haki za binadamu.

Rebeca na washindi wengine watatu wa mwaka huu watapatiwa tuzo yao mjini New York, Marekani tarehe 10 Desemba mwaka huu, wakati wa kilele cha tamko la haki za binadamu la umoja wa mataifa ambalo mwaka huu linatimiza miaka 70.

Mshindi mwingine ni Asma Jahangir mwanaharakati na mwanasheria wa Pakistani ambaye amefariki dunia mwaka huu.

Tuzo hiyo ilianza kutolewa mnamo mwaka 1973 na hadi leo imetolewa mara 10.

"Kile tumekuwa tukikifanya ni kuwahamasisha wasichana kusimamia ndoto zao na kuzifikia katika jamii, kitu ambacho kimechukuliwa kuwa cha umuhimu,"

"Kwetu ni furaha kuwa dunia imetambua kile tukifanya na sasa ni fursa muhimu kuzungumzia changamoto ambazo wasichana wanapitia, na kuihamasisha serikali na wadau kuweza kuona faida ya mtoto wa kike katika maendeleo ya jamii," Bi Gyumi aliiambia BBC.

Bi Gyumi ni mwasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative nchini Tanzania, ambayo inapigania haki ya msichana kupata elimu.

Mwanasheria huyu alishinda kesi kubwa mwaka 2016 iliyohusu ndoa za watoto baada ya kupinga sheri ya ndoa ya mwaka 1971 nchini Tanzania, iliyoruhusu wasichana wenye miaka 14 kuolewa.

Kutokana na kazi yake ya kupigania haki ya msichana, Bi Gyumi ameshinda tuzo ya UNICEF ya mwaka 2016 na kutajwa kuwa mwanamke wa mwaka na jarida la New African Women.

Tuzo hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa hutolewa kwa watu binafsi na mashirika kwa kutambua mchango wao wa kipekee katika kuendeleza na kulinda haki za binadamu na uhuru wa msingi wa binadamu kwa mujibu wa tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa .

Baraza Kuu la UN lilianzisha tuzo hii kwa azimio la Desemba 10 mwaka 1968 wakati tamko la haki za binadamu lilipotimiza miaka 20 tangu kupitishwa.