Kwa Picha: Mwili wa mwandishi Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba wapokelewa Tanzania

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Andrea Schmidt akiwa na picha ya marehemu
Maelezo ya picha,

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Andrea Schmidt akiwa na picha ya marehemu

Mwili wa mwandishi maarufu kutoka Tanzania aliyekuwa anafanyia kazi Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba umewasili Tanzania.

Mwili wa Nyagabona umewasilishwa uwanja wa ndege Dar es Salaam na safari ya kuusafirisha hadi Mwanza inakaribia kuanza baada ya ibada kuanyika.

Mwandishi huyo, aliyekuwa mtangazaji wa michezo na burudani katika DW alipatikana akiwa amefariki dunia mjini Bonn nchini Ujerumani Alhamisi ya tarehe 18 Oktoba baada ya kutoonekana afisini Jumanne na Jumatano.

Kutoonekana kwake kazini kuliwashtua wafanyakazi wenzake, na kuwafanya waamue kwenda kutoa taarifa polisi ambao walifika nyumbani kwake na kuvunja mlango uliokuwa umefungwa na kumkuta amefariki dunia.

Ibada inatarajiwa kufanyika eneo la Lugalo baadaye leo na kisha mwili wake utasafirishwa kuelekea Bunda, Musoma kwa ajili ya mazishi siku ya Jumatano.

Bi Schmidt amesema pengo la Isack haliwezi kuzibika kwani alikuwa mchapa kazi, mbunifu mcheshi na asiyekata tamaa

''Nakumbuka wakati mmoja kabla ya kuja Tanzania alisema naenda nyumbani kula bata ,akiwa na maana kwamba furahia maisha," amesema.

Maelezo ya picha,

Jeneza lenye mwili wa marehemu

Isaac Gamba ni nani?

Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba alizaliwa Januari 19, 1970 wilayani Bunda Mjini.

Ni mtoto wa 12 kati ya watoto 13 wa familia ya marehemu mzee Elizaphan Munyenjwa Maribwa.

Alipata elimu yake ya msingi, katika shule ya msingi Kabalimu iliyoko mjini Bunda kuanzia mwaka 1978 nakuhitimu mwaka 1984. Baada ya hapo, aliendelea na masomo ya Sekondari katika shule ya sekondari Majengo Moshi kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 1988.

Baadaye aliendelea na masomo ya A Level katika shule ya Old Moshi kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1991.

Alijiunga na mafunzo ya jeshi kwa mujibu wa Sheria katika jeshi la kujenga Taifa (JKT) mwaka 1991.

Baadaye alipata mafunzo ya uandishi wa Habari katika Radio Sauti ya Injili ya Mjini Moshi.

Marehemu alifanikiwa kuhitimu elimu yake ya shahada ya Uanahabari na Mawasiliano katika chuo cha Tumaini jijini Dar es Salaam mnamo mwaka 2010.

Marehemu alianza kufanya kazi kwa muda wa takribani miezi sita akiwa Arusha katika Radio 5, na ndipo kwenda kujiunga na kituo cha utangazaji cha Radio Free Africa (RFA) Mwanza mwaka 1997's mpaka mwaka 2003, Kisha akajiunga na Radio Uhuru ya jijini Dar es Salaam mwaka 2004.

Marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba mwaka 2005 alijiunga na kampuni ya IPP Media katika kituo chake cha habari cha Radio One na ITV hadi mwaka 2015 alipohamia katika shirika la utangazaji Ujerumani la Deutsche Welle (DW) ambapo mauti ilimfika akiwa huko.

Utangazaji wa michezo

Gamba aliyejiunga Dw mwaka 2015 akitokea ITV/ Radio One alikuwa mmoja wasoma habari mahiri na kuendesha vipindi vya habari na kifo chake kiliwashtua wengi.

Akiwa Bonn, Gamba alifahamika sana kutokana na ucheshi wake na wepesi wa kufahamiana na watu.

DW imesema imepoteza mtangazaji mahiri aliyemudu kazi yake kuanzia kwenye habari, ripoti za matukio duniani hadi michezo.

Isaac alikuwa kwenye kikosi cha watangazaji waliokuwa wanapeperusha matangazo ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.

Pambano la mwisho alilotangaza ni mchuano kati ya Augsburg na Borussia Dortmund.

Picha zote zina hakimiliki