Kwa Picha: Kenya Airways yaanza safari za moja kwa moja hadi Marekani

Maafisa wa kipeperusha bendera za Kenya na Marekani kabla ya ndege aina ya Boeing 787-Dreamliner kuanza safari Jumapili

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Maafisa wa kipeperusha bendera za Kenya na Marekani kabla ya ndege aina ya Boeing 787-Dreamliner kuanza safari Jumapili

Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, limeanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa JFK jijini New York.

Rais Uhuru Kenyatta Jumapili usiku aliongoza hatua hiyo ya kihistoria kwa sekta ya safari za ndege nchini Kenya alipozindua safari ya ndege ya kwanza, KQ Boeing 787-8 Dreamliner.

Ndege hiyo ilikuwa imewabeba abiria 234. Tiketi za kawaida zinauzwa Sh89,000 ($890).

Ndege hiyo itachukua muda wa masaa 15, hii ikiwa imepunguza muda wa zamani wa safari hiyo kwa masaa saba.

Ndege hiyo iliondoka JKIA saa tano kasorobo usiku na inatarajiwa kuwasili uwanja wa JFK saa kumi na dakika 25 alasiri.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Safari ya kwenda Marekani itapunguzwa kwa saa saba

Miongoni mwa abiria waliosafiri kwa ndege hiyo katika safari yake ya kwanza ya moja kwa moja kutoka Nairobi hadi jijini New York ni Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni balozi Monica Juma na balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec.

Rais Kenyatta alimkabidhi Balozi Juma bendera ya Kenya huku afisa mmoja wa Ubalozi wa Marekani akimkabidhi balozi Godec bendera ya Marekani.

Chanzo cha picha, UHURU KENYATTA/FACEBOOK

Abiria wengine katika ndege hiyo ni Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Esther Koimett na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Kenya Airways Sebastian Mikosz.

Chanzo cha picha, UHURU KENYATTA/Facebook

Uzinduzi wa safari hiyo ya kwanza ya Ndege kwenda jijini New York, ni hatua kubwa kwa sekta ya uchukuzi wa ndege nchini Kenya hasa kwa kuimarisha sekta mbali mbali za kiuchumi kama vile utalii na biashara.

Chanzo cha picha, UHURU KENYATTA/FACEBOOK

Safari za ndege za moja kwa moja hadi nchini Marekani, zitaipa fursa nchi ya Kenya kunufaika na uchumi wa marekani, ambao ndio mkubwa zaidi ulimwenguni na vile vile katika eneo zima la kaskazini Marekani.

Mambo muhimu kuhusu safari hiyo:

  • Safari hiyo itachukua saa 15 kutoka New York hadi Nairobi na saa 14 kutoka Nairobi hadi New York.
  • Shirika hilo limesema litatumia marubani wanne na wahudumu 12 wa ndege.
  • Safari yote itatumia tani 85 za mafuta.
  • Shirika hilo litatumia ndege zake za kisasa aina ya Boeing 787 Dreamliner ambazo huwabeba abiria 234.
  • Ndege za kwenda Marekani zitaondoka JKIA Nairobi saa 23:25 na kufika JFK kesho yake saa 06:25.
  • Ndege za kurudi Nairobi zitaondoka New York 12:25 na kutua JKIA saa 10:55 kesho yake.

Safari hii ina maana gani kwa Kenya?

Shirika la ndege la Kenya Airways linahudumia vituo 40 barani Afrika pekee mbali na safari zake za ndege katika bara Ulaya, Asia, Mashariki ya kati na maeneo ya bara hindi.

Uzinduzi wa safari hizo za ndege kunatarajiwa kuvutia mashirika mengi ya kibiashara kwa soko la Kenya na kuongezea kwa zaidi ya makampuni 40 ya Marekani ambayo yamefanya Jiji la Nairobi kuwa makao makuu kwa huduma zao barani Afrika.

Vile vile, safari hizo za ndege za moja kwa moja zitaongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini Kenya huku serikali ikikadiria kwamba safari hizo zitasaidia kuleta watalii wengi mashuhuri na wa kibiashara.

Maeneo ya Afrika ya mashariki na ya Kati pia yatanufaika kiuchumi kutokana na hatua hiyo ya hivi punde katika sekta ya safari za ndege nchini Kenya.

Kabla ya shirika la ndege la Kenya Airways kupewa kibali cha ndege zake kusafiri moja kwa moja hadi jijini New York, Halmashauri ya Usimamizi wa Safari za Ndege nchini (KCAA) ilihitajika kutimiza masharti ya Halmashauri ya Ukadiriaji wa Safari za Ndege za Kimataifa ambayo yanatolewa na Shirika la usimamizi wa safari za Ndege nchini Marekani na hivyo kupewa kibali cha safari zake mwaka jana wa 2017.

Mbali na Kenya, mataifa mengine ya Afrika yanayoendesha safari za moja kwa moja hadi Marekani ni, Cape Verde, Misri, Ethiopia, Nigeria na Afrika Kusini.

Picha zote zina hakimiliki