Neils Högel: Nesi akiri kuua wagonjwa 100 Ujerumani

Nesi Neils Högel akijiziba uso kwa aibu

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Maelezo ya picha,

Nesi Neils Högel akijiziba uso kwa aibu alipopandishwa mahakamani

Nesi mmoja nchini Ujerumani amekiri mbele ya mahakama kuwaua wagonjwa takriban 100, hali inayomfanya kuwa miongoni mwa wauaji wakubwa kabisa kuwahi kutokea.

Wapelelzi wanasema kuwa Neils Högel alikuwa akiwapatia wagonjwa wake dozi kali ambazo zilipelekea umauti wao katika hospitali mbili ambazo alikuwa akifanya kazi.

Lengo la nesi huyo, kwamujibu wa wapelelezi ilikuwa ni kuwashangaza na kuwavutia wafanyakazi wenziwe kwa kuwarejeshe fahamu wagonjwa aliowalaza kwa kotumia dozi kali. Mchanganiko huo wa dozi za kuwalaza na kuwaamsha ndio uliowaathiri zaidi wagonjwa.

Högel tayari anatumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kusababisha vifo sita vya wagonjwa aliokuwa akiwahudumia.

Sasa inaaminika kuwa amewaua wagonjwa 36 katika mji wa Oldenburg na wengine 64 katika mji jirani wa Delmenhorst kati ya mwaka 1999 na 2005.

Alipoulizwa na Jaji katika mahakama ya Oldenburg mapema leo kama mashtaka yanayomkabili yana ukweli wowote, nesi huyo alikubali kutenda mashtaka yote hayo.

Kesi hii mpya ilianza kwa watu kukaa kimya kwa dakika moja kwa heshima ya wagonjwa waliouawa inatarajiwa kuunguruma mpaka mwezi Mei mwakani. Ushahidi wake umetokana na uchunguzi wa miaka kadhaa ulioambatana na kufanyia vipimo vya umu kwa miili 130 iliyofukuliwa makaburuni.

Wapelelezi wanaamini kuwa nesi huyo aliua watu wengi zaidi ila ushahidi unakosekana kutokana na baadhi ya miili ya watu hao kuchomwa moto.

Christian Marbach, ambaye ni msemaji wa familia zilizopoteza wapendwa wao amesema ni aibu kubwa kuwa nesi huyo aliachwa akiua watu kwa miaka kadhaa bila ya mamlaka kuingilia kati.

"Tumepambana kwa miaka minne ili kesi hii isikilizwe na tunatarajia Högel afungwe kwa kuwaua watu wengine 100," amesema Marbach ambaye babu yake aliuawa na Högel.

Högel alikamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 2005 akimdunga mgonjwa sindano ambayo hakuandikiwa katika mji wa Delmenhorst.Mwaka 2008 alihukumiwa kwenda jela kwa miaka saba kwa kosa la kujaribu kufanya mauaji.

Kati ya mwaka 2014-15, alishitakiwa na kukutwa na hatia ya mauaji ya wagonjwa wawili na jaribio la kuua wagonjwa wengine wawili ambapo alihukumiwa kifungo cha maisha.

Aliiambia mahakama kuwa anaomba radhi ya dhati na anatumaini kuwa ndugu wa marehemu hao wangepata utulivu na amani. Alijitetea kuwa maamuzi yake ya kuwadunga wagonjwa sindano za sumu hayakuwa ya kupanga.

Hata hivyo, katika kesi hiyo alikiri mbele ya daktari wa akili wakati wa kesi hiyo kuwa aliua zaidi ya wagonjwa 30.

Baada ya hapo wapelelezi wakatanua wigo wa uchunguzi wao kwa kufukua miili ya wagonjwa 130 ambao walipitia mikononi mwake.

Rekodi katika hospitali ya Oldenburg zinaonesha kuwa kiwango cha vifo na wagonjwa kuamshwa kwa dawa kali vilikuwa zaidi ya mara mbili wakati nesi huyo alipokuwa zamu, vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti.