Lion Air: Ndege mpya inawezaje kuanguka?

Ndege aina ya Boeing MAX 8 ilikuwa imehudumu chini ya mwaka mmoja

Chanzo cha picha, Boeing

Maelezo ya picha,

Ndege aina ya Boeing MAX 8 ilikuwa imehudumu chini ya mwaka mmoja

Ndege ya shirika la Lion Air iliyoanguka baharini, ikiwa na abiria karibu 190 muda mfupi baada ya kupaa kutoka mji mkuu wa Jakarta nchini Indonesia imeendelea kuvutia hisia mbali mbali.

Ndege hiyo aina ya Boeng 737 MAX 8, ilikua mpya. Hii ni ajali ya kwanza kuhusisha ndege aina hiyo.

Maelezo kuhusu nini hasa kilitokea yamekua finyu lakini chanzo cha ajali hiyo kitajulikana baaada ya uchunguzi kufanywa.

Ajali ya ndege mara nyingi husababishwa na mchanganyiko wa mambo tofauti ikiwa ni pamoja na hitilafu ya kimitambo au makosa ya kibinadamu-lakini je ndege mpya inawezaje kuanguka?

Ndege hiyo ya Boeng 737 MAX 8 iliyohusika katika ajali siku ya jumatatu ilikuwa imehudumu kutoka mwaka Agosti 15 mwaka 2017

Kwa mujibu wa mkuu wa tume ya kitaifa ya usalama wa uchukuzi wa angani Soerjanto Tjahjano ndege hiyo ilikua imesafiri kwa saa 800.

Inasemekana rubani aliomba waelekezaji wa ndege katika uwanja wa Jakarta wamruhusu kurudi uwanjani hapo muda baada ya kupaa.

Sasa imebainika ndege hiyo ilikumbwa na hitilafu ya kimitambo siku ya Jumapili.

Stakabadhi za kunakili hali ya kimitambo ya ndege iliyppatikana na BBC, katika uwanja wa ndege wa Denpasar mjini Bali - zinaashiria kuwa mtambo wa kudhibiti kasi ya ndege upande wa marubani ilikua ina hitilafiana.

Kutokana na hilo rubani ilipeana udhibiti wa ndege hiyo kwa afisa wa kwanza na kuendelea na safari na hatimaye wakatua salama mjini Jakarta.

Lion Air ahaijathibitisha ripoti hizo, lakini huenda ndege hiyo ilikumbwa na hitilafu isiyojulikana ya kimitambo iliyotajwa na mkuu wa shirika hilo

Edward Sirait amesema hitilafu hiyo ilitatuliwa kitaalamu kulingana na kanuni zilizowekwa.

Ameongeza kuwa shirika la Lion Air lina ndege 11 za aina hiyo na kwamba hakuna mpango wa kusitisha huduma ya ndege hizo.

Ni 'nadra' ndege mpya kupata ajali

Mchambuzi wa masuala ya ndege Gerry Soejatman ameiambia BBC kwamba ndege zilizozeeka ndizo zilizopo katika hatari ya kupata ajali lakini pia kuna uwezekano wa ndege mpya kukumbwa na matatizo ya kiufundi.

"Ikiwa ndege ni mpya kuna matatizo huchukua muda kujitokeza lakini ikitumiwa mara kwa mara matatizo hayo hugunduliwa na mara nyingi hutatuliwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza.''

Maelezo ya picha,

Ramani ya mahali ilipoangunga ndege hiyo

Mchambuzi mwingine , Jon Ostrower wa jarida la The Air Current, amesema "Kila wakati kunatokea matatizo madogo ambayo ni ya kawaida lakini si matatizo ambayo yanaweza kutishia usalama wa ndege".

Ameongezea kuwa uzuri wa ndege mpya ni kuwa imekaguliwa vilivyo kwa sababu kila kitu ni kipya.

Wachambuzi wote wawili wanasema ni mapemno kubaini kilichosababisha ajali ya ndege JT 610.

Bwana Ostrower aliiambia BBC "Sijui ni kitu gani kitaifanya ndege mpya kama hii kuanguka,"

"Kuna vitu vingi vinavyoweza kuchangia ajali kama hii."

Kwa upande wake Bwana Soejatman amesema anaamini huenda "chanzo cha ajali hii isiwe matatizo ya kiufundi japo ni mapema kubaini hilo".

Wataalamu Iwanaamini huenda utepetevu wa usalama wa angani kama vile makosa ya kibinadamu nchini Indonesia, huenda umechangia mkasa wa siku ya Juma tatu.

Shirika la Boeing limeelezea kusikitishwa kwake na kisa cha kupoteza ndege yake.

Limetuma rambi rambi zake kwa jamaa za wahasiriwa wa mkasa huo na kuongeza kuwa itashirikiana katika uchunguzi wa kubaini nini hasa kilichotokea.

Kwa mujibu wa shirika hilo ndege aina ya 737 MAX imekua ikinunuliwa sana katika historia yake na kwamba karibu ndege 4700 ilikua tayari imeagizwa.

MAX 8 ilikuwa imeagizwa na mashirika kadhaa ya ndege ya American Airlines, United Airlines, Norway na FlyDubai.