Utafiti: Subiri angalau mwaka mmoja kabla ya kupata tena ujauzito

Chanzo cha picha, AFP
Kinamama wanastahili kusubiri kwa mwaka mmoja baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine ili kupunguza hatari ya kumpoteza mama na mtoto,wasema utafiti mpya.
Watafiti hao hata hivyo wanasema hawastahili kusubiri kwa muda wa miezi 18 kama ilivyopendekezwa katika kanuni iliyopo sasa ya shirika la Afya Duniani WHO.
Muda mfupi kati ya mimba moja hadi nyingine humuweka mama katika hatari ya kuzaa mtoto ambaye hajatimiza wakati wa kuzaliwa,mtoto mdogo au kifo chake.
Watafiti wanatumai matokeo ya uchunguzi huu utawapatia hakikisho wanawake waliyo na umri mkubwa.
Mmoja wa watafiti hao Dr Wendy Norman amesema hizi ni ''habari njema" kwa wanawake waliyo na zaidiya miaka 35 ambao wana mpanga familia zao.
"Wanawake waliyo na umri mkubwa kwa mara ya kwanza watapata mwongozo wa uhakika kuhusiana na suala la kupanga uzazi wa watoto wao".
Utafiti uliyohusisha kuzaliwa kwa karibu watoto 150,000 nchini Canada, uliyofanywa na vyuo vikuu vya British Columbia (UBC) na Harvard umebaini kuwa miezi 12 hadi 18 ni muda mwafaka kwa mwanamke kujipumzisha baada ya kujifungua kabla ya kupata tena ujauzito.
Mwongozo wa sasa wa shirika la Afya Duniani unapendekeza muda wa usiyopungua miezi 18 hadi 24.
Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti huo pia ulibaini kuwa:
- Kupata ujauzito chini ya miezi 12 baada ya kujifungua ni hatari kwa wanawake wa miaka yote.
- Ni hatari zaidi kwa mama aliye na umri wa zaidi ya miaka 35, na vile vile ni hatari kwa mtoto mchanga ikiwa mama ana miaka kati ya miaka 20 na 34
- Wanawake waliyo na miaka zaidi ya 35 waliyo pata ujauzito miezi sita baada ya ujauzito mwingine walikua katika hatari ya kupoteza maisha kwa 1.2% . (visa 12 vimeripotiwa kwa kila mimba 1000)
- Kusubiri kwa miezi 18 kabla ya kupata ujauzito mwingine kunapunguza hatari hiyo kwa 0.5% (visa vitano kwa kila mimba 1,000)
- Wanawake wadogo waliyopata ujauzita miezi sita baada ya kujifungua walikua katika hatari ya kupata uchungu wa uzazi kabla ya muda wa kujifungua kwa 8.5%.
- Hali hii inaweza kupunguzwa kwa hadi 3.7% ikiwa wanawake hao wangelisubiri kwa miezi 18 kati ya ujauzito mmoja hadi mwingine.
Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti huo uliangazia zaidi wanawake nchini Canada - kwa hivyo haijabaiika ikiwa matokeo yake yatakua sawa kote duniani.
Mtafiti Dr. Sonia Hernandez-Diaz anasema matokeo yaliashiria hali tofauti kwa wnawake wa miaka tofauti.
"Ujauzito wa haraka haraka huenda ukaashiria kutozingatia uzazi wa mpango, kwa baadhi ya wanawake wa umri mdogo.
Mandy Forrester, kutoka taasisi ya wakunga ya Royal College, anasema utafiti huu "ni muhimu kwa sababu unaimarisha tafiti nyingine kuhusiana na suala la muda wa kupata ujauzito mwingine baada ya kujifungua".
Chanzo cha picha, Getty Images
"Yote tisa kumi ni kuwa mwanamke atajiamulia mwenyewe anataka kuchukua muda gani baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine''
Anasema jambo la msingi ni kwa wanawake kote duniani kuwa na ufahamu wa kujihami nao kuhusiana na suala hili ili wafanya maamuzi ya busara.
"Wataalamu wa afya wako tayari kumsaidia mwanamke kufanya maamuzi yake, kuhusiana na kile kilicho sawa kwake.
Pia ameongezea kuwa wanawake wanastahili kupata ushauri kuhusiana na mbini tofauti za kupanga uzazi iliwweze kupanga familia zao ikiwa wanaazimia kufanya hivyo.
"Huduma za kitaalamu zinastahili kufikia wanawake wote."