Raila Odinga: Je, majukumu mapya yatambana kwenye siasa za Kenya?

  • Hezron Mogambi
  • Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
Odinga

Uteuzi wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kama mwakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika kuhusu maendeleo ya miundo mbinu barani Afrika kumefungua awamu mpya katika maisha ya kisiasa ya kiongozi huyo wa upinzani nchini Kenya na kuzua mjadala mpya kuhusu hatima yake katika siasa za Kenya.

Katika uteuzi ambao ulitangazwa na Ras wa Kenya Uhuru Kenyatta katika siku ya kuadhimisha sikuu kuu ya Mashujaa nchini Kenya, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, alieleza kuwa jukumu la Bw Odinga litahusisha kushirikisha uungwaji mkono wa kisiasa miongoni mwa nchi za Afrika na makundi ya kieneo na wadau mbalimbali ili kufikia uungwaji mkono katika maendeleo ya muundo msingi kote barani Afrika.

Serikali ya Kenya tayari imempa Raila Odinga paspoti ya kiwango cha kazi yake mpya ili kumwezesha kusafiri na kutekeleza majukumu yake mapya.

Bw Odinga ndiye atakayekuwa mwakilishi wa ngazi ya juu zaidi akiwa na afisi katika nchi tano za Afrika kwani majukumu yake yanahusisha masuala mengi ya kiuchumi, kisiasa na kiufundi.

Wadhifa huu ambao unaonekana kuwa mzito kwani atamwakilisha mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat katika masuala ya kimaendeleo katika nchi 55 za Afrika ambazo ni wanachama wa Umoja wa Afrika.

Uteuzi huu ulijibu swali ambalo limekuwa likiulizwa na wengi kuhusu nafasi ya Raila Odinga katika uamuzi wake wa kufanya kazi karibu na kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta tangu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2017.

Je, uteuzi wa Odinga unamwacha wapi?

Kama mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika, Bw Odinga atakuwa na afisi jijini Addis Ababa, Ethiopia, jijini Nairobi, Johannesburg, Abuja, Nigeria na jijini Cairo, Misri lakini atakuwa akisafiri sana katika maeneo mengi kote barani Afrika.

Aidha, Bw Odinga atahusika katika kupatikana kwa suluhu katika mizozoz barani.

Bw Odinga atakuwa na afisi jijini Nairobi ambayo itakuwa na wafanyikazi na washauri kumsaidia kutekeleza jukumu lake vilivyo pamoja na ushirika wake na Rais Kenyatta katika kuwaunganisha Wakenya.

"Makubaliano yetu na Bw Odinga ya kusahau tofauti zetu na kufanya kazi pamoja yametambuliwa kote duniani. Umoja wa Afrika umemteua Raila Odinga kama mwakilishi wake wa ngazi za juu kuhusu muundo msingi na maendeleo barani Afrika," Rais Kenyatta alisema.

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha,

Odinga aliapishwa kuwa 'Rais wa Wananchi' mapema mwaka huu

Spika wa Bunge la kitaifa la Kenya Justin Muturi na mwenzake wa seneti Bw Ken Lusaka walipongeza uteuzi wa Raila Odinga wakisema kuwa sifa na ujuzi wa Bw Odinga zinatosha kumfanya kupewa wadhifa huo hasa ikizingatiwa majukumu ambayo amewahi kuyashikilia nchini Kenya.

Itakumbukwa kwamba, katika siku za hivi karibuni, Bw Odinga alikuwa amezua mjadala mkali kuhusiana na mageuzi ya kikatiba nchini Kenya uliokuwa umezua na kuleta utata katika uwanja wa kisiasa.

Katika muktadha huu, wanasiasa ambao wanapinga kuwepo mabadiliko ya kikatiba wangependa kumwona Bw Odinga nje ya siasa za Kenya.

Odinga astaafu siasa?

Mshirika mkubwa na mshauri wa Rais Uhuru Kenyatta, David Murathe, ametupilia mbali madai ya wale wanaomtaka Bw.Odinga kustaafu kutoka siasa za Kenya kwa sababu ya majukumu yake akieleza kuwa majukumu yake huenda yakamwongezea sifa zaidi katika siasa za Kenya.

"Ni watu wangapi ambao wamezitumia kazi kama hizi za kimataifa ili kujitayarisha kwa majukumu ya kisiasa humu nchini? Ni nini kinachoweza kumzuia Raila Odinga kuwania kiti chochote cha kisiasa?" Bw Murathe ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama tawala cha Jubilee nchini Kenya aliuliza.

Msimamo kama huu unashikiliwa na wanasiasa wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) ambacho Raila Odinga anakiongoza.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa chama cha Jubilee wamekuwa wakimtaka Bw Odinga kuachana na siasa za Kenya kwa sababu ya uteuzi wake wa ngazi za Afrika.

Bw Odinga mwenye umri wa miaka 73, atakuwa akifanya kazi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika katika kushauriana na kuwashawishi marais wa nchi mbali mbali za Afrika kufikia ajenda ya kuboresha muundomsingi kote barani.

Katika jukumu hili lake jipya anaungana na marais wa zamani ambao wameteuliwa kama mabalozi maalum wa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Kiongozi wa zamani wa Mozambique Joaquim Chissano ni mmojawapo wa viongozi wa zamani ambao wameteuliwa kama mabalozi maalum wa Umoja wa Afrika.

Kiongozi wa muda wa nchi ya Guinea, Sekouba Konate, aliteuliwa kama kiongozi mkuu kwa niaba ya mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuhusu utendakazi wa jeshi la muda la Afrika.

Kiongozi wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya pia aliteuliwa kuwa mwakilishi Umoja wa Afrika kuhusu Mali na sehemu ya Sahel.

Kuteuliwa kwa Raila Odinga kunamfanya kuwa Mkenya wa kwanza kuteuliwa katika wadhifa wenye ngazi za juu kama hiyo. Itakumbukwa kuwa mwaka wa 2014, mwanajeshi mstaafu katika jeshi la Kenya jenerali Jackson Tuwei aliteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mwakilishi maalum kuhusu kundi la Uganda la Lord's Resistance Army.

Kisiasa, Bw Odinga amewania Urais nchini Kenya mara nne na ana uungwaji mkono na urafiki na wanasiasa wengi kote nchini Kenya na uteuzi huu mpya ambao utamfanya kusafiri nje ya nchi mara nyingi unaonekana kutilia shaka matamanio yake ya kisiasa nchini Kenya.

Kama ilivyo, wanaoteuliwa katika ngazi za juu kama uteuzi huu wa Bw Raila Odinga ulivyo hupendelea na kuchukua muda mwingi katika nafasi hizi ikilinganishwa na siasa za nchi zao.

Dalili zinaonesha nini?

Hata hivyo kiutekelezi, Bw Raila Odinga haonekani kuwa atauacha uwanja wa kisiasa nchini Kenya kwa urahisi kulingana na wanasiasa wa chama chake na wandani wake wa karibu.

Kwa sababu hii, Bw Odinga atalazimika kuhakikisha kuwa ametia mizani katika utekelezaji wa majukumu haya mawili.

Dalili kwamba hii itakuwa ndio hali itakayojiri hata baada ya Bw Odinga kuteuliwa ilibainika tu baada ya Bw Odinga kukubali uteuzi wake wa wadhifa huu na kusema kuwa atatumia ujuzi wake wa zaidi ya miaka 30 kuharakisha maendeleo ya muundomsingi barani Afrika.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Kenyatta na Odinga walikutana Machi mwaka huu na kuahidi kuwaunganisha Wakenya

Katika jukumu lake mpya, Bw Odinga anatarajiwa kushughulikia zaidi mapengo ya muundo msingi katika barabara kuu za nchi nyingi za Afrika kama moja ya mapengo yaliyopo katika mfumo wa barabara kuu zinazounganisha nchi za Afrika yenye lengo la kuharakisha maendeleo ya kisasa barani Afrika.

Zaidi, Bw Odinga atazingatia reli yenye mwendo wa kasi ambayo ni mmojawapo ya ajenda kuu katika mpango wa miaka ya kwanza kumi katika ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.

Wengine wanaoyaona majukumu haya kuwa mazito na yatakayochukua muda mwingi wa kiongozi huyu wa upinzani lakini wengine wanadai kuwa hali hii itamjengea sifa na kumwongezea zaidi kwa minajili ya siasa za mwaka wa 2022 nchini Kenya. Wendani wake wa kisiasa hawangependa kumwona Bw Odinga akiondoka kwenye siasa za Kenya kwa sababu baadhi yao wanamtegemea sana kisiasa kwa sababu ya ushawishi wake wa miaka mingi.

Kwa upande mwingine, wapinzani wa Bw Odinga wangependa kumwona Bw. Odinga akiondoka kwenye uwanja wa siasa za Kenya. Kwneye kundi hili, wanangependa kuona kwamba majukumu haya mapya ya Bw Odinga yanampa nafasi ndogo sana ya kushiriki katika siasa za Kenya na kupunguza kasi yake ya siasa za mwaka wa 2022.

Itakumbukwa kwamba wanasiasa nchini Kenya tayari wameanza kampeini za mwaka ujao kwa kutumia mbinu mbalimbali.

Zaidi, kuna tetesi na wasiwasi iwapo Bw Odinga ataweza kutekeleza majukumu yake mapya pamoja na kwamba mwanasiasa huyu atakuwa na umri wa miaka 77 wakati wa uchaguzi ujao wa mwaka 2022.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Bw Odinga akiwa na kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) nchini Zimbabwe Nelson Chamisa

Washirika wa kisiasa wa Naibu wa Rais wa Kenya, William Ruto wamekuwa wakimtaka kiongozi huyu wa upinzani ambaye wanamtambua kuwa mpizani wao wa kwanza kuhusiana na siasa za Urais mwaka wa 2022, kustaafu kutoka siasa za Kenya.

Hata hivyo, kuna wale wanaouona uteuzi wa Bw Odinga kama njia mmojawapo ya kuinua hadhi ya Bw. Odinga kama mwanasiasa mweledi ambaye Kenya inamhitaji kama kiongozi wakati Kenya inapoendelea kukumbwa na changamoto nyingi.

Ni bayana kuwa, ili kufikia azma yake na kuonekana kufaulu katika majukumu yake mapya ni lazima Bw. Odinga kujiundia sifa zaidi barani na kumweka katika nafasi nzuri kisiasa ndani na nje ya Kenya.

Kwa sasa, kilicho bayana kuhusu mjadala wa hatima ya kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga ni kuwa wanasiasa wanajitayarisha kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022 na kwa vyovyote, wangependa kuwaondoa wapinzani wao!

Prof. Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi@yahoo.co.uk