Zanzibar: Tunguja na vijiwe vidogo vinavyotumika kufundishia madrasa na kuwafanya wanafunzi kuzingatia masomo yao

wanafunzi

Kusini mwa Zanzibar nchini Tanzania, kuna utaratibu usio wa kawaida ambapo baadhi ya wanafunzi wa madrasa wamekuwa wanawekewa vijiwe vidogo au hata tunguja (nyanya pori) kwa lengo la kuwafanya wanafunzi hao kuzingatia masomo yao.

Mwalimu Jecha Sule Mohamod kutoka chuo cha madrasatul-Qadiriya kisiwani Zanzibar, anasema mbinu hizo zilikuwa zinatumika tangu zamani ukiwa ni ubunifu wa kuwafanya watoto watulie na kuzingatia kile wanachofundishwa.

Jecha anaeleza kwamba zamani kulikuwa na njia mbalimbali za kufundishia kama vile kusoma kwa kutumia mbao na wino maalumu ili kuwafundisha watoto namna ya kuandika lugha ya kiarabu na kuhifadhi kile walichofundishwa.

"Tulikuwa tunafundishwa jinsi ya kuzingatia kile ambacho tunafundishwa kwa kuwekewa kijiwe chini ya kidevu hivyo mwanafunzi akishawekewa tu anakuwa anaangalia pale ambapo anafundishwa," anasema.

"Njia hii pia inasaidia kwa sababu madrassa zetu ziko mtaani karibu na barabara ambapo watu wanapitamara kwa mara hivyo mwalimu kuwadhibiti wanafunzi inakuwa ngumu inabidi amuwekee kijiwe ili ashughulikie masomo yake badala ya kuangalia mambo mengine."

Maelezo ya video,

Tunguja zinatumika kuwafanya wanafunzi kuzingatia masomo yao

Hata hivyo wanaamini kuwa njia hiyo ni ubunifu unaoangalia mazingira husika yakoje na wanaamini kuwa utamaduni huo umeweza kuleta matokeo chanya ya upatikanaji wa viongozi wa dini kama vile mashehe na maimamu.

Wanaamini pia ili kufikia mikakati mizuri ya taaluma lazima ubunifu uhusike.

Kwa nini watoto hawa wanaweza kuzingatia masomo kwa njia hii

Wanafunzi wanakuwa wanaelewa na sio tu kuimba bila kuelewa.

Maelezo ya picha,

Tunguja inatumika kufundishia

Mwalimu Haji Mohamed Mahamud anasema kwamba lengo la mbinu hii ni kumfanya mwanafunzi kutoshughulika na kitu chochote zaidi ya kusoma.

Mtoto akiangusha tunguja hiyo huwa anaonywa tu lakini sio kuadhibiwa.

Ukimuona mtoto ana michezo mingi unamuwekea ili aweze kuzingatia katika kusoma.

Muda wa kukaa nayo inategemea na lazima apate mazoezi kujua kuweka tunguja hiyo, kama hana mazoezi hawezi kukaa nayo hata dakika moja.

Mbinu ambayo wanaitumia ni kuweka kitu kimoja kinachoitwa tunguja unamuwekea chini ya kidevu na kuinamisha uso .

Maelezo ya sauti,

Kisiwani Zanzibar, madrassa zatumia nyenzo za asili kufundishia

Hapo anaweza kushughulikia kusoma na lazima apate mazoezi kabla lakini hapo badae hatawekewa tena.

Kwa upande wao wanafunzi, wanaona njia hiyo ni nzuri na inawasaidia kuzingatia masomo na moja ya mazoezi kwao.

Mohamed Simba ,mkazi wa Makunduchi ni mwanaharakati anayekubaliana na matumizi ya njia hizi za ufundishaji.

Simba anaamini kuwa walimu huwa wana saikolojia ya kutosha ya kujua kama watoto wamechoka basi wanapaswa kutafutiwa njia mbadala.

"Ni vizuri kuchukua maoni ya walimu wa madrassa kwa kuwa wao ndio wanajua mazingira halisi wanayoyafanyia kazi na wanajua wanafunzi wanaowafundisha.

Hivyo kama wanaofundisha vyuo vya madrassa wakiona kwamba kutumia njia hizi za kutumia tunguja,

vijiwe au nyanya pori ili kuwafanya wanafunzi kuzingatia katika masomo ni vyema kwa sababu hata sisi tulitumia njia kama hizo" Simba alisema.

Kusoma na kuweza kufahamu na kuzingatia, kuna kusoma kwa aina nyingi kuna kusoma kwa kuimba lakini pia kuna kusoma kwa kuzingatia.

Hata hivyo njia hiyo ni mila ambayo imekuwepo ingawa sasa imeanza kutoweka baada ya baadhhi ya watu kulalamikia kuwa ni unyanyasaji kwa watoto.