Mwenendo wa nyumbu kati ya Serengeti na Maasai Mara unavyoshangaza mwaka huu

Nyumbu

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelfu ya nyumbu ambao huwa kivutio kikubwa cha watalii katika mpaka wa Kenya na Tanzania wanaripotiwa kurejea Tanzania mapema kuliko ilivyo kawaida yao, na ghafla kuanza kurejea Kenya.

Wanyama hao walianza kuvuka kutoka Hifadhi ya Wanyama ya Maasai Mara upande wa Kenya na kuingia katika Mbuga ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania, takriban mwezi mmoja mapema kuliko miaka ya awali.

Taarifa nchini Kenya zinasema kuna baadhi ya nyumbu walisalia mbuga ya Maasai Mara, na baadhi wamerejea majuzi kutoka Tanzania jambo ambalo linawashangaza wahudumu.

Kawaida, nyumbu huvuka kuingia Maasai Mara mwezi Juni na Julai, tukio ambalo limeorodheshwa kuwa miongoni mwa maajabu ya dunia.

Baada ya kukaa Kenya miezi mitatu hivi, hurejea Tanzania mwezi Novemba na Desemba kujifungua wakati mbuga hiyo ina malisho ya kutosha.

Husalia Tanzania kwa miezi 10 hadi Julai mwaka unaofuata ambapo huingia Kenya.

Hata hivyo, wadau wa utalii mbuga ya Maasai Mara wanasema kuna baadhi ya nyumbu walioanza kuondoka Maasai Mara kurejea Tanzania mwezi Agosti, lakini sasa wengi wameanza kurudi Kenya.

Hii inashangaza kwani tukio la kuhama kwao kuingia Kenya huwa mara moja pekee lakini mwaka huu ni kama wamevuka mara mbili.

Bw Nicholas Murero, mratibu wa mfumo wa ikolojia wa Mara-Serengeti amenukuliwa na gazeti la Nation la Kenya akisema hii ndiyo mara ya pili kwa tukio kama hilo kutokea.

"Septemba, nyumbu hao walitarajiwa kuwa bado wapo Maasai Mara, lakini walikuwa tayari wameanza safari ya kurejea Tanzania. Kurejea kwao kulisababisha wasiwasi kuhusu kutabirika kwa mwenendo wao, na kusababisha watalii waliotaka kuwatazama wakivuka kubadilisha mpangilio wa safari zao," amesema.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Mvua imekuwa ikinyesha Maasai Mara kwa karibu wiki tatu sasa.

Afisa wa mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete amenukuliwa na mtandao wa gazeti la serikali wa Daily News Online akikanusha taarifa kwamba nyumbu wengi bado wako Kenya.

Amesema kufikia sasa takriban asilimia 80 ya wanyama pori waliokuwa wamehama wamerejea Serengeti na hasa eneo la Ndutu, tayari kuzaa.

"Ni lazima warejee Ndutu ambapo huwa wanazaa. Ndio maana huwa mara nyingi nasema ni kama wanyama hawa wana pasipoti za Tanzania (uraia wa Tanzania)," alisema.

Anasema kuna uwezekano kwamba wanyama hao watakaa muda zaidi Serengeti kutokana na mvua inayonyesha maeneo hayo kwa saa ambayo inahakikisha kuna malisho tele.

Afisa mkuu wa wanyamapori katika hifadhi ya Maasai Mara Moses Kuyuoni amenukuliwa na gazeti la Nation akisema kwamba uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha mabadiliko yanayoshuhudiwa sasa ni mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema pia kuharibiwa kwa malisho kuliathiri kuhama kwao miezi miwili iliyopita.

"Mambo kadha yamechangia hili. Kuna nyasi nyingi Maasai Mara kutokana na mvua. Wengi wa nyumbu hawakuvuka Juni kama ilivyo kawaida kutokana na moto uliowashwa porini (Serengeti)," alisema kwa mujibu wa Nation.

Mwezi Julai mwaka huu, wanyama hao pia walichelewa kuvuka kuingia Kenya jambo lililosababisha kuzuka kwa lawama kutoka wahudumu wa kitalii Kenya.

Baadhi walidai Tanzania ilikuwa imewasha moto makusudi maeneo ya mbuga ya Serengeti kuwazuia wanyama hao kuvuka kuingia Kenya.

Serikali ya Tanzania ilikanusha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa mamlaka za hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania zilifanya hujuma kuchoma moto eneo la hifadhi ili kuzuia nyumbu kuvuka kuelekea nchini Kenya.

Msemaji wa Wizara ya mali asili na utalii Tanzania, Dorina Makaya alisema madai hayo hayakuwa ya kweli.

Alisema kilichotokea kilikuwa ni uchomaji wa kawaida wa awali ambao ulikuwa unafanywa kwa awamu.

Lengo la uchomaji huo wa nyasi na majani porini huwa kuzuia majanga ya moto kutoka nje ya hifadhi ambayo yanaweza kufikia ndani ya hifadhi.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Dorina alisema uchomaji wa moto hufanyika kitaalamu ili kuwezesha kuota kwa majani mapya kwa ajili ya malisho yao, pia kupunguza majani mengi ambayo huwafanya watalii kutoona vizuri wanapofika kutembelea hifadi ya Serengeti.

''Safari ya Nyumbu ni utaratibu wao wa asili , sababu pekee inayoweza kusababisha kuchelewa kwa Nyumbu kwenda Kenya inawezekana ni kutokana na mvua upatikanaji wa maji ya kutosha huwafanya kuendelea kubaki palepale kwa sababu wanapata maji ya kutosha''.

''Kwa kuwa Tanzania imepata mvua kwa kipindi kirefu hivyo inawezekana kabisa kuwa Nyumbu wanaweza kuchelewa kuhamia Kenya msimu huu."

''Zoezi la uchomaji majani kwenye hifadhi ni la kawaida ambalo hufanyika Tanzania lakini pia hata Maasai Mara hufanyika hayo pia''.

Nyumbu takriban milioni mbili huhama kila mwaka kati ya Kenya na Tanzania.

Kati ya Julai na Oktoba wakiwa Kenya, nyumbu hao hutunga mimba lakini hujifungua wakiwa nchini Tanzania ambapo ndama 400,000 huzaliwa katika kipindi cha wiki sita kati ya Januari na Machi katika mbuga ya Serengeti.

make their way back down south to the southern Serengeti to feed