Asia Bibi: Mkristo aliyefutiwa adhabu ya kifo nchini Pakistan 'kwa kuukashifu Uislamu'

Asia Bibi alifungwa mwaka 2010 baada ya kushutumiwa kumkashifu mtume Muhammad
Maelezo ya picha,

Asia Bibi alifungwa mwaka 2010 baada ya kushutumiwa kumkashifu mtume Muhammad

Mahakama ya Juu zaidi ya Pakistan imebatilisha hukumu ya kifo kwa mwanamke mmoja wa kikristo aliyekutwa na hatia ya kuikashifu dini ya kiislamu.

Mahakama hiyo imeamuru kuachiwa huru kwa mwanamke huyo katika kesi ambayo imeigawa nchi.

Asia Bibi alifungwa mwaka 2010 baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka kumkashifu mtume Muhammad baada ya kulumbana na majirani zake.

Mwanamke huyo amekuwa akisisitiza kuwa hana hatia lakini ametumikia kifungo cha miaka nane kwenye chumba cha peke yake jela.

Hukumu hiyo ya kihistoria tayari imesababisha maandamano yenye ghasia kutoka kwa makundi ya kisiasa yanayounga mkono sheria ya kukashifu dini.

Maandamano dhidi ya maamuzi ya mahakama yalifanyika katika miji ya Karachi, Lahore, Peshawar na Multan.

Mapigano ya waandamanaji hao na polisi yaliripotiwa.

Chanzo cha picha, ARSHAD ARBAB

Maelezo ya picha,

Maandamano yamefanyika katika maeneo mbalimbali

Nje ya mahakama hiyo katika mji mkuu wa Islamabad kuna kizuizi cha polisi na wanajeshi ambao wamejipanga kuwazuia waandamanaji hao kuingia ndani.

Jaji Mkuu Saqib Nisar, ambaye alisoma hukumu hiyo alisema Asia Bibi anaweza kuachiwa huru kutoka gereza la Sheikupura, lililokuwa karibu na Lahore, ikiwa hatahusishwa na kesi nyingine yeyote.

Mwanamke huyo hakuwepo mahakamani kusikiliza hukumu yake lakini hakuamini maamuzi hayo yaliyotolewa dhidi yake alipoelezwa akiwa gerezani.

"Siamini ninachokisikia kuwa nitaweza kutoka sasa. Kweli kabisa wataniachia huru?" Shirika la habari la AFP lilimnukuu akisema hayo kupitia njia ya simu.

Ni jambo gani ambalo Asia Bibi alishutumiwa?

Kesi ya Asia Bibi ambaye jina lake halisi ni Asia Noreen ilianzia kwenye malumbano na kikundi cha wanawake mwezi Juni 2009.

Wanawake hao walikuwa wanavuna matunda na ugomvi ulizuka kuhusu ndoo ya maji. Wanawake wa Kiisilamu walisema kuwa alikuwa ametumia kikombe ambacho wasingeweza kukishika tena kwa sababu imani yake imekifanya kikombe hicho kutokuwa safi.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa malumbano hayo yalikuwa yanamtaka Asia Bibi kubadili dini yake na kuwa muislamu ndio sababu iliyompelekea kutoa kauli za matusi dhidi ya mtume Muhammad katika majibu yake.

Baadaye alipigwa mpaka nyumbani kwake wakati waliomshtaki wakidai kuwa alikiri kukashifu dini.Alifungwa baada ya polisi kufanya uchunguzi.

Kukashifu dini kuna maana gani Pakistan?

Sheria ambazo ziliwekwa na Waingereza mwaka 1860 waliifanya kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kusumbua mikutano ya dini, kupita makaburini , kukashifu imani ya mtu kwa maksudi mtu kuharibu chombo kinachotumika kuabudia na hukumu yake kwa hayo yote ni kifungo cha miaka 10.

Mahakama kuu ilisemaje?

Majaji walisema kuwa mashtaka yaliyotolewa hayajajitosheleza kuthibitisha suala hilo

Kesi hiyo ilikuwa ina ushahidi mdogo, walisema kuwa hakukufuatwa utaratibu katika kufuatilia kesi hiyo.

Inasemekana tu kuwa mshtakiwa alikiri mbele ya kundi la watu wengi waliotaka kumuua.

Hukumu hii ambayo imeangalia Koran na historia ya dini ya kiislamu iimalizika na nukuu kutoka kwa hadithi ,inayosema kuwa mtume Muhammad alitaka usawa kwa hata wale ambao sio waislamu .

Kwa nini kesi hii imezua makundi?

Chanzo cha picha, EPA

Uisilamu ndiyo dini ya taifa la Pakistan na umeathiri pakubwa mfumo wa kisheria wa nchi hiyo. Uungwaji mkono wa sharia za kudhibiti kukashifu dini ni mkubwa.

Baadhi ya wanasiasa wenye msimamo mkali wamekuwa wakipigia chapuo adhabu kali zitolewazo kwa watu wanaokutwa na hatia ya kukashifu dini kama njia ya kujinufaisha kisiasa.

Wakosoaji wengi wanasema sharia hizo mara kadhaa zimekuwa zikitumika kulipiza kisasi baada ya malumbano binafsi, na hukumu zimekuwa zikitolewa kwa kutegemea ushahidi finyu.

Jamii ndogo ya Wakristo imekuwa ikilengwa na kushambuliwa kwa tuhuma za kukashifu uislamu. Na Wakristo wengi wamekuwa wakilalama na kuishi kwa hofu ya kubambikiwa kesi.

Hakuna mtu ambaye amenyongwa na serikali kwa kutumia sharia hizo, lakini baadhi ya watu wameuawa mitaani na watu waliojichukulia sharia mkononi baada ya kutuhumiwa kuukashifu uisilamu.

Asia Bibi ambaye ni mzaliwa wa mwaka 1971 na mwenye watoto wanne ndio mwanamke wa kwanza kuhukumiwa kifo kwa mashtaka hayo nchini Pakistan. Hukumu yake ya wali ilipingwa vikali kimataifa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu.

Nini kinaendelea?

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mume wake Asia Bibi na binti yake wamedai kuhofia usalama wao nchini Pakistan

Kuna hofu kubwa kuwa Asia Bibi na familia yake wanaweza kushambuliwa na watu wenye hasira kali baada ya kuachiwa huru.

Tayari kuna nchi kadhaa ambazo zimejitolea kumpa hifadhi yeye na familia yake na inategemewa kuwa watakubali kuihama nchi yao.

Binti yake, Eisham Ashiq alishawahi kuliambia shirika la habari la AFP kuwa endapo ataachiliwa huru: "Nitamkumbatia na nitalia kukutana naye na pia nitamshukuru Mungu kwa kuwezesha kuachiliwa huru."

Familia hiyo tayari imeshaeleza juu ya hofu yao na mipango ya kuikimbia Pakistan.