Zitto Kabwe: Mbunge wa Kigoma Mjini aendelea kushikiliwa na polisi Tanzania

Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe akitoka kituo cha polisi Kamata,mjini Dar es salaam
Maelezo ya picha,

Zitto Kabwe amekuwa akikamatwa na kuzuiliwa mara kadha

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe, anaendelea kushikiliwa na polisi kwa siku ya tatu bila kufunguliwa mashtaka.

Zitto, ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini, alikamatwa Jumatano mishale ya saa 5 asubuhi na kuzuiliwa na polisi katika kituo cha polisi Oysterbay kabla ya kuhamishiwa kituo cha polisi Mburahati mahojiano zaidi. Mpaka Alhamisi jioni bado alikuwa anashikiliwa katika kituo hicho na maombi yake ya dhamana yakigonga ukuta.

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma lilikuwa limemtaka mwanasiasa huyo kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita Oktoba 28, 2018.

Mbunge huyo alikuwa amewaambia wanahabari kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano kati ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Alisema hilo lilitokea wakati wa kuwahamisha wakulima katika eneo la Mpeta wilayani Uvinza mkoani humo.

Mke wa Zitto anena

Mke wa kiongozi huyo ameandika kupitia mtandao wake wa Twitter kuwa polisi walikagua nyumba yao asubuhi ya leo na wanaendelea kumshikilia mwanasiasa huyo kwa madai kua bado wanamhoji.

Lowassa azuiwa kumuona

Gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa ambaye sasa ni mwananchama wa chama cha upinzani Chadema alizuiwa kumuona Zitto alipomtembelea katika kituo cha polisi Mburahati.

Kwa mujibu wa gazeti hilo Lowassa alifika kituoni hapo saa tisa alasiri na kuambiwa muda wa kumuona Zitto ulikuwa umepita.

"Huyu ni kiongozi mwenzetu huku upinzani lazima tushikamane kukabiliana na lolote lililo mbele yetu. Tunahitaji kuwa kitu kimoja kuliko wakati mwingine wowote," amenukuliwa Lowassa akisema.

Masuala ambayo Zitto anahojiwa

  • Mauaji ya polisi na raia katika kijiji cha Mpeta, Uvinza katika mkoa wa Kigoma
  • Kutekwa kwa bilionea Mo Dewji
  • Hali ya usalama wa taifa Tanzania
  • Masuala ya jumla aliyoyaibua wakati wa kikao chake na wanahabari wikendi

*Kwa mujibu wa taarifa ya katibu mwenezi wa ACT Wazalendo anayesimamia pia mawasiliano Ado Shaibu

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno alisema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.

Wakili wa mbunge huyo Jebra Kambole ameambia BBC mapema leo kwamba hawajapiga hatua yoyote katika kumkatia dhamana mteja wao.

Siku ya Jumatano aliiambia BBC kuwa tamko la Zitto alilitoa siku ya Jumapili, kuhusiana na hali ya usalama wa nchi, lilikuwa na maneno ya uchochezi yanayokiuka kifungu cha 55, kifungu kidogo cha (a) cha Sheria ya Makosa ya Jinai Sura 16, ya mwaka 2002.

"Kwa msimamo wetu tunaamini kwamba haya ni makosa ya kisiasa, tunaamini kwamba kwa matamko yake aliyoyatoa ni matamko ambayo yanaonesha kutoridhishwa na utendaji wa serikali.

"Kitu ambacho kinaruhusiwa na sheria. Ni maoni ambayo ameyaeleza kama mtu wa kawaida, kama Mtanzania, kama mbunge, ambayo anaruhusiwa kwa mujibu wa sheria, lakini kwa kuwa wao wanafikiri ni kosa, na ndio maana wakati wanaandika maelezo yake, walipofika kutaka kumhusisha na kosa, yeye akasema kama kuna kosa lolote amejuhusisha nalo, ataenda kutoa maelezo ya kina mahakamani," amesema Bw Kambole.

Maelezo ya sauti,

Magufuli: Sijazima demokrasia Tanzania

Wakili huyo amesema hawakupewa taarifa rasmi ya sababu ya kunyimwa dhamana ya polisi.

"Tulipofuatilia dhamana, tukaambiwa kwamba huyu mtu bado tunaendelea kumshikilia. Kwa nini hapewi dhamana, bwana hayo maneno mtakuja kuambiwa kesho (leo), lakini huyu mtu lazima alale ndani," amesema wakili huyo.

Bw Kombale amesema kosa analodaiwa kutenda mbunge huyo ni kosa linalodhaminika na mteja wake anaweza kujiwasilisha wakati wote akihitajika.

"Kwa mujibu wa sheria, unaponyimwa dhamana ya polisi una haki ya kufungua shauri mahakamani ya kudai dhamana, na kwa kuwa polisi wana haki ya kuwazuilia watuhumiwa si zaidi ya saa 24, kwa hivyo itakapofika saa nne, sisi tutafungua kesi mahakamani ya kudai Zitto Kabwe apewe dhamana," ameambia BBC.