Kuchanganya nafaka kwa ajili ya lishe ya mtoto si salama

Haki miliki ya picha Mama Organic
Image caption Mchanganyiko wa nafaka nyingi katika unga wa uji husababisha mtoto kupata choo kigumu

Kupata mtoto ni safari mpya wazazi huanza kuipitia, ni kipindi ambacho hubadilisha maisha na mipango ya wazazi.

Chakula sahihi cha kumpatia mtoto anayeanza kula ni moja ya mambo muhimu ambayo huwasumbua wazazi wengi.

Kwa kawaida mtoto kuanzia umri wa miezi sita huanza kupewa uji maalumu kama kianzio cha kuanza kujifunza kula.

Uji huo ni mjumuisho wa nafaka mbalimbali na mara nyingine mpaka mboga mboga.

Kwa kawaida huchanganywa Mahindi, Mchele, Ulezi, soya, mtama, karanga na dagaa au Mahindi, ulezi, soya, mchele, karanga, ngano, ufuta.

Mchanganyiko hutegemea ni nani ambaye ametengeneza.

Kwa sasa unga huu umekuwa biashara muhimu kwa baadhi ya watu. Kwani huchanganya na kusaga kisha kuwauzia watu ukiwa katika vifungashio mbalimbali.

Baadhi ya kina mama huchanganya nafaka na kutengeneza wenyewe unga huu wa lishe kwaajili ya watoto wao na si biashara.

Image caption Wafanya biashara wa unga wa uji wa watoto wameongezeka sana

Lakini kumekuwa na maonyo kadha wa kadha juu ya usalama wa unga lishe, jumbe zinasambaa katika mitandao kukataza wazazi kuchanganya nafaka katika unga wa uji wa watoto.

Pia wapo wataalamu wanao hoji juu ya viwango vinavyotumika katika mchanganiko wa unga huo ambapo huatarisha usalama wake.

BBC imezungumza na baadhi ya kina mama wanaandaaji unga wa uji wa watoto? Au kama wananunua huzingatia mambo gani?

"Mimi mwanangu nampa unga wa dona tu nachanganya siagi na maziwa na huwepa sukari kiasi. Siamini katika unga lishe maana unaweza kuta mtoto ana pata mzio kwa mavitu tunayochanganya. Afu mie huyu mwanangu wa kwanza sitaki kumchanganyia hovyo," Mama Robert anaiambia BBC

"Binafsi huwa nanunua uji wa lishe na umetengenezwa na Mahindi, soya, Karanga, dagaa, mboga mboga na mchele. Na huwa naupika taratibu mpaka uive.

Na Alhamdulillah mwanangu anakua," anasema Bi Rahma.

Haki miliki ya picha Mama Organic
Image caption Uandaaji wa uji wa lishe unahitaji umakini na nafaka lazima zikauke vizuri.

Amina Ramadhani Muhando, ni mwandaaji na muuzaji wa unga lishe kwa ajili ya uji wa watoto maarufu kama Mama Organic. Yeye hutumia zaidi mahindi lishe viazi lishe na soya. Anasema uandaaji wa unga huu unahitaji uzoefu na ufahamu mzuri wa lishe ya watoto bila kuwa makini unaweza hatarisha afya ya mtoto.

"Natumia vitu vichache sana kwasababu hata wataalamu wanashauri hivyo unakuwa na base ambayo ni nafaka maana nafaka hazitakiwi kuzidi mbili alafu unachanganya na option ambapo inaweza kuwa viazi au samaki au protini yoyote. Unapoweka nafaka nyingi mfano zaidi ya mbili ndo inasababisha mtoto anapata choo kigumu, anapata shida kupata choo.

Alafu zile nafaka zinaiva kwa muda tofauti, mtama unaiva kivyake maindi kivyake, mchele una mda wake na hata ulezi unamuda wake. Kwahivo ukipika zote kwa pamoja unakuta kuna ambavyo vitakuwa vimeiva na vingine havija iva au vingine vitaiva sana mpaka vile vitu muhimu vinavyopatikana humo unakuta havipo tena.

Hivyo mimi huwa natumia Mahindi lishe kama nafaka kuu kisha Viazi lishe kama mbadala wa protini.

Pia hata soya natumia lakini naipika kwanza kisha nachanganya hivyo kwapamoja huiva haraka kama dadika kumi mpaka kumi na tano," Amina au Mama organic anaiambia BBC

BBC imezungumza na mtaalamu wa lishe daktari Louiza Tumaini Shem, anasema uji wa lishe ulio salama kwa mtoto ni ule ambao hauja wekwa vitu vingi na umechanganywa kila nafaka kwa kipimo sahihi bila kuzidisha wala kupunguza.

Image caption Kuna madhara endapo unga wa uji ulikosewa katika uandaaji

"Unga salama ni ule ambao hauja kaa mda mrefu, hauna mchanganyiko wa vitu vingi sana, na uwe umezingatia vipimo vya kila kiungo. Muhimu pia ni kuhakikisha nafaka unazo weka zimeandaliwa vizuri hazija vunda, zimeoshwa vizuri yaani mahindi yakauke vizuri, soya lazima ipikwe kidogo itolewe maganda yaani ni hatari kama umeweka mahindi yaliyohifadhiwa na dawa na hukuyaosha vizuri," Daktari Louiza anaiambia BBC

Hata hivyo daktari huyo ameonya juu ya madhara makubwa yanayoweza kutokana na kushindwa kuandaa vyema uji wa mtoto.

"Nafaka zikiwa chafu mtoto ataharisha na ikitokea mahindi au nafanka nyingine yoyote ilikuwa na dawa na ukapika bila kuosha vizuri mtoto anaweza pata matatizo ya ini.

Pia nafaka ambazo hazikukauka vizuri mfanoyaweza kuwa karanga mahindi au yoyote ikivunda kuna sumu ambayo inaitwa Flatoxin inapatikana humo inaweza pia leta tatizo la ini.

Na pia kama kiwango cha wanga kimezidi sana unampa mtoto nguvu nyingi ambayo haitaji kwa muda huo. Na kwa mtoto mwenye kisukari ukimpa uji wenye wanga mwingi lazima sukari itakuwa inapanda," daktari Louiza anaiambia BBC.

Hata hivyo daktari huyo amemaliza kwa kuwashauri wazazi kuwa makini na unga walishe wanao wapatia watoto wao.

Na wakague nafaka ambazo zinatumika kuwa zime oshwa,kukauka vizuri na zime wekwa kwa kiasi.

Mfano kama umeweka kilo mbili ya wanga basi weka kilo moja ya protini. Yaweza kuwa mahindi, ngano na mchele kisha ukachagua protini moja kati ya soya au karanga.

Mwisho amemaliza kwa ku onya kuwa maharage ya soya huwa yanachelewa kuiva hivyo ukitaka kuya weka kwenye uji uwe makini kwa kuyaandaa vyema kabla ya kuchanganya.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii