Zitto Kabwe: Mbunge wa Kigoma Mjini aachiwa kwa dhamana

Zitto Kabwe

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe ameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa na polisi kwa siku tatu.

Zitto alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu majira ya saa nane mchana na kusomewa mashitaka matatu ya uchochezi kuhusu kauli yake juu ya mauaji ya polisi na raia katika kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, mkoani Kigoma. Zitto alikana mashtaka yote.

Waendesha mashtaka walitaka mbunge huyo anyimwe dhamana kwa sababu walizoziita ni za kiusalama na kusema upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.

Hata hivyo, mahakama ilimuachia baada ya kukidhi vigezo vya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya milioni 10 na vitambulisho vinavyotambulika kisheria. Ametakiwa kufika tena mahakamani Novemba 26, 2018.

Zitto alikamatwa saa tano asubuhi siku ya Jumatano na kufikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay kabla ya kuhamishiwa kituo cha polisi cha Mburahati ambapo alikuwa akishikiliwa kwa siku zote mpaka alipopandishwa kizimbani hii leo.

Wakati Zitto akiwa rumande kampeni mahsusi iliendeshwa mtandaoni kuwataka watu kusimama na Zitto ambaye wafuasi wake wanamtaja kuwa ni mpigania haki za wote.

Zitto amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya rais John Magufuli na mara kadhaa amekuwa akitumia mitandao ya kijamii ama mikutano na wanahabari kuwaasa watu kuacha woga wa kuikosoa serikali.

Kampeni ya kudai kuachiwa kwa Zitto iliendeshwa kwa kauli mbiu za 'Haki kwa Zitto' #JusticeForZitto na 'Mwachilieni Zitto Kabwe' #FreeZittoKabwe.

Baadhi ya wanasiasa wa chama tawala CCM pia walitakiwa kupaza sauti zao juu ya masaibu yaliyompata Zitto wakidai aliwatetea wakati wakiwa katika nyakati za matatizo. Ujumbe huo pia ulipelekwa kwa bilionea Mohammed Dewji ambaye kipindi alipotekwa Zitto alipaza sauti yake.

Wapo waliohoji wapi polisi wanapata uwezo wa kukaa na mtuhumiwa kwa siku tatu bila kumpandisha mahakamani.

Kelele za kutaka Zitto atendewe haki zimeifikia taasisi ya kutetea haki za binaadamu za Amnesty International ambalo limeitaka jeshi la polisi Tanzania kumuachia ama kumshitaki kiongozi huyo wa upinzani.