Je wapinzani Tanzania wamejipanga kutatua changamoto zinazowakabili?

Lowassa na Magufuli Haki miliki ya picha IKULU
Image caption Lowassa na Magufuli walikutana Ikulu Januari 2018 kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa 2015

Hama hama ya wabunge, madiwani na wenyeviti wa halmashauri ni miongoni mwa changamoto zinazovikabili vyama vya upinzani hapa nchini Tanzania.

Hadi sasa takribani wabunge 9 wamehama vyama vya upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema kimepoteza wabunge 7, huku CUF kikipoteza wabunge wawili.

Hadi sasa takribani madiwani na wenyeviti 150 wamevihama vyama vya upinzani na kujiunga CCM.

Je ukiondoa hama hama ya wabunge na viongozi wengine, nini hasa kinachoukabili upinzani Tanzania?

Mikutano ya hadhara

Mikutano ya hadhara kwa wanasiasa ni miongoni mwa nyenzo inayotumiwa kuwashawishi wananchi ili waunge mkono vyama vya upinzani.

Tangu kuingia serikali ya Rais John Magufuli, wabunge na wanasiasa wanaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo wanayowakilisha, na sio vinginevyo na wakati mwengine hata ruhusa hiyo pia huzuiliwa.

Hali hii imepunguza kasi ya upinzani kuwafikia wananchi. Mathalani tawala zilizopita tumeshuhudia wanasiasa wakiendesha vuguvugu mfano, Chadema waliendesha Operesheni Sangara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Movement For Change (M4C) kote nchini.

Matunda ya mikutano hiyo ndiyo ilichochea kuongezeka idadi ya wabunge wa upinzani kufika kufika 116 kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Haki na kesi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe akiwa mahakamani wiki iliyopita

Imeshuhudiwa wabunge kadhaa wa upinzani wakishtakiwa kwa makosda mbalimbali.

Miongoni mwa wabunge waliofunguliwa kesi ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini),Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Tarime Mjini), Esther Bulaya (Bunda), Freeman Mbowe (Hai), Peter Lijualikali (Kilombero), na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) kwa kuwataja wachache.

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa vyama vya upinzani navyo vimefungua kesi dhidi ya serikali ya Tanzania kama nyenzo ya kudai haki za msingi kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Chama cha ACT-Wazalendo wamefungua kesi mbili za Kikatiba. Kesi ya kwanza inahusu mikutano ya hadhara na nyingine ni haki ya Maandamano.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amefungua kesi mbili za kuhoji mamlaka ya Wakuu wa Mikoa.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Fatma Karume amefungua kesi ya kuhoji Uhuru wa Tume ya Taifa ya Uhcgauzi (NEC) akimwakilisha mdai mwanaharakati Bob Wangwe.

Umoja wa Wanaharakati wa kudai Demokrasia Tanzania na kushirikiana na wanashera wamefungua kesi mbili Namba 4 na Namba 6 za mwaka 2018 Mahakama Kuu wakipinga namna demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza unavyokiukwa nchini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Upinzani cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu anasema kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya utawala ni kutokana na kukandamizwa kwa misingi ya demokrasia na hivyo kutishia shughuli halali za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara.

Upande mwingine kesi walizofunguliwa wanasiasa wa upinzani zinawafanya wawe kwenye hekaheka za 'kushinda' mahakamani badala ya kuvijenga vyama vyama.

Hali ya usalama

Image caption Tundu Lissu akizungumza na mwandishi wa BBC, Zuhura Yunus

Ingawa halijatamkwa dhahiri kuwa kuna tatizo la usalama kwa wabunge na wanasiasa wa upinzani, lakini mazingira yanaashiria kuwa wanasiasa wa pande zote mbili wanaowakilisha majimbo yao wamekuwa kwenye wasiwasi.

Wengi wanatumia mfano wa shambulizi la Septemba 7 mwaka 2017 dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kama kiashiria cha hali ya usalama kwao sio nzuri.

Migogoro na ombwe la kiitikadi

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Upinzani cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu anasema, "Changamoto Kuu ya upinzani ni vyama kukosa itikadi inayoeleweka. Vyenye itikadi, haifahamiki vyema kwa wanachama na viongozi. Ndio maana ni rahisi kwa wanachama kuhama CUF (Chama cha Kiliberali) kwenda kujiunga CCM (Chama kinachojiita cha Kijamii). Hii ni dalili ya wazi ya vyama kutoendeshwa kiitikadi."

Kwa tafsiri yake ni kwamba vyamka vyote vinakuwa na itikadi zao zinazokubaliwa na wanachama. Inapotokea mwanasiasa, mfano Mbunge anatoka CCM na kujiunga chama chenye itikadi tofauti kama Chadema au kinyume chake, hilo ni ombwe kubwa la itikadi.

Vilevile migogoro ndani ya vyama vya upinzani kama vile UDP, CUF, TLP, NCCR Mageuzi na Chadema kwa kutaja vichache vimekuwa vichocheo vya baadhi ya wanasiasa kuvihama hivyo kuchangia wananchi kukosa imani.

Migogoro hiyo sio inaacha makovu pekee bali huibua makundi yenye kubeba visasi dhidi ya jingine hali inayochangia vyama vyenyewe kuporomoka.

Ni kweli wapinzani sio wazalendo?

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa vyama vya upinzani vimekuwa vikikosolewa na chama tawala pamoja na wafuasi wake kuwa hawana uzalendo kwa nchi na kwamba muda wote wanataka kupinga maendeleo ya nchi na hawajali maslahi ya wananchi.

Lissu aitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati Tanzania

Ado Shaibu, anasema "Watu kudhani wapinzani ni wapingaji wa kila kitu kutoka serikalini na kwamba yule anayetambua na kupongeza chochote serikalini ni msaliti. Fikra hizi sio za kweli, zinapotosha dhana nzima ya vyama vyama vya upinzani nchini. Inakubalika kuwa sote tunajenga nchi moja, hatuwezi kukosa uzalendo.

Wataalamu wa siasa wanasemaje?

Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. Richard Mbunda anasema, "Haki za vyama vya siasa zipo kwenye Katiba. Na zinaungwa mkono na Sheria zingine za Bunge kuhusu vyama vya siasa na Haki za uhuru wa kisiasa kwa ujumla wake. Lakini pale ambapo watawala wanazikanyaga haki kama hizi kwa makusudi, vyama vya upinzani vinafanya nini?"

Anaongeza: "Mosi, tunategemea mapambano ya kisheria. Mapambano haya yakisimamiwa na upinzani. Tunategemea kuona wanasiasa wa upinzani wakiomba 'Tafsiri ya Mahakama' kulingana na kauli kama za kuzuia mikutano ya siasa kitaifa. Na watafsiri sheria wetu nchini wangewekwa kwenye kipimo cha mizani,

"Pili, uzoefu wangu wa tafiti za migogoro Zanzibar unanikumbusha kuwa unapolegeza mapambano ndipo unapokuwa kwenye kona ya kushindwa. Ni lazima upambane ili uungwe mkono hata ya jumuiya ya Kimataifa."

"Chukua mfano wa tamko la Ubalozi wa Marekani hapa Tanzania kuhusiana na chaguzi ndogo. Lilikuwa tamko muhimu sana kwa upinzani lakini lilikosa maana kwa kuwa upinzani wenyewe umelala.

Sisemi hivi kama mpinzani wa vyama vya upinzani, lakini ninatazama siasa kisayansi, na kama mwanataaluma nafahamu dhahiri kuwa hata operesheni UKUTA ulikuwa mpango mzuri. Walipoogopa tu wameijengea serikali nguvu ya kuwabana zaidi."

Mustakabali wa upinzani?

Changamoto hizi zinazidi kuongezeka hasa pale Vyama vya upinzani vitakaposhindwa kuwa mfano mbadala wa kutengeneza viongozi, kuwa na ajenda mahususi ya kusimamia, kutumia fursa ya mikutano ya majimbo kuongeza tija zao zaidi katika kukubalika kwao.

Kila changamoto huwa na fursa yake. mathalani, uamuzi wa vyama vya upinzani kufungua kesi za kuhoji mamlaka ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na uhuru wa Tume ya Uchaguzi ni miongoni mwa mifano ambayo inatakiwa kuchukuliwa kwa kufanyiwa kazi maeneo mengine.

Kulingana na mazingira ya sasa, inategemewa vyama vya upinzani kuwa na kesi nyingi dhidi ya utawala, bila kujali matokeo ya kesi hizo yatakuwa hasi kwao. Kesi wanazofungua zinachochea mijadala ya kisheria,utawala na mabadiliko yake ndani ya nchi.

Lowassa asema Magufuli anafanya kazi nzuri

Aidha, kutumia 'vuguvugu' la 'tafsiri ya Mahakama' juu ya jambo lolote lile linaweka msingi kuwa vyama vya siasa vimechukua mkondo wa sheria kama viongozi mbadala na kuwaonyesha wananchi kuwa wao ni sehemu ya taifa hili hivyo kuitwa wapinga maendeleo au kukosa uzalendo sio sahihi.

Ikumbukwe, mambo yote mazuri hayaletwi kwa njia moja ya kuyaomba, lakini wakati mwingine yanaletwa kwa njia ya kushinikiza. Pale sheria inapotakiwa kutafsiriwa Mahakamani kwa namna yoyote ile huwa inaacha alama ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa mfumo wa demokrasia nchini.

Muda utaongea.

Mada zinazohusiana