Jamal Khashoggi: Mamlaka za Uturuki zinaamini mwili wa mwandishi Khashoggi ulitoswa kuwenye tindikali baada ya kuuawa

Jamal Khashoggi

Chanzo cha picha, EPA

Kiongozi wa ngazi ya juu nchini Uturuki, Yasin Aktay, amesema anaamini kuwa mwili wa mwandishi Jamal Khashogi uliyeyushwa kwenye tindikali baada ya kuuawa na kukatwa katwa.

Bw Atkay ambaye ni mshauri wa Rais wa Uturuki Racip Erdogan amesema hitimisho pekee linaloingia akilini ni kuwa waliomuua mwandishi huyo wameteketeza mwili wake "ili kufuta kabisa ushahidi."

Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa utawala wa Saudia hususani sera za mrithi wa kiti cha ufalme mwanamfalme Mohammed bin Salman aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mnamo Oktoba 2.

Alikimbilia Marekani mwaka 2017 akihofia usalama wake na huko alikuwa akiandika makala na maoni kwenye gazeti la Washington Post.

"Sababu ya kumkata vipande vipande ilikuwa ni kurahisisha kuyeyusha mwili huo kwa wepesi", Bw Aktay ameliambia gazeti la kila siku la Hurriyet.

"Sasa tunafahamu kuwa si tu walikata kata mwili wake vipande bali waliuyeyusha kabisa."

Licha ya kauli hiyo kutoka kwa kiongozi mkubwa, bado hakuna ushahidi wowote wa kiuchunguzi uliotolewa unaothibitisha kuwa mwili huo ulitoswa kwenye tindikali. Lakini mpaka hii leo, mwezi mmoja toka auawe, mwili wake bado haujapatikana.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Mwanamfalme Mohammed Bin Salman ameiambia Marekani kuwa Khashoggi alikuwa mtu hatari.

Pia hii leo taarifa mpya zimeibuka kuwa mwanamfalme Mohammed bin Salman aliwaambia maafisa wa Marekani kwamba anamchukulia mwanahabari Khashoggi kama mshirika hatari wa kundi la kiislamu lenye itikadi kali.

Mwanamfalme Mohammed ameripotiwa kusema hayo katika mazungumzo yake ya simu na maafisa wa Ikulu ya Marekani baada ya kupotea kwa Khashoggi.

Saudia hata hivyo imekanusha ripoti hiyo iliyochapishwa katika magazeti ya Washington Post na New York Times.

Waendesha mashtaka wa Istanbul wamethibitisha siku ya Jumatano kuwa mwandishi huyo alinyongwa, huku wenzao wa Saudia wakikiri kuwa mauaji hayo yalipangwa.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Salah,mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi alipokutana Mwanamfalme Mohammed Bin Salman

Huku hayo yakijiri mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi, Salah pamoja na familia yake wamewasili Marekani siku chache baada ya kukutana na Mwanamfalme Mohammed Bin Salman.

Katika taarifa iliyochapisha magazetini familia nya Khashoggi imekanusha madai kwamba Khashoggi alikua mwanachama wa kundi la Muslim Brotherhood.

Familia hiyo pia imeongeza kwamba yeye mwenyewe aliipinga madai hayo mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.

"Jamal Khashoggi hakua mtu hatari kwa vyovyote. Madai hayo ni ya kushangaza sana," ilisema taarifa hiyo.

Uchunguzi umebaini nini kufikia sasa?

Mpaka sasa hakuna makubaliono yaliyofikiwa kuhusu jinsi Khashoggi alivyofariki.

Aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul kushughulikia stakabadhi za kumwezesha kumuoa mchumba wake wa Uturuki, Hatice Cengiz.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Hatice Cengiz, aliyekuwa mchumba wa Jamal Khashoggi

Siku ya Jumatano Uturuki ilisema kuwa aliuawa alipoingia ndani ya ofisi za ubalozi huo na mwili wake kukatwa katika vipande "kulingana na utaratibu uliopangwa awali''.

Vyombo vya habari vya Uturuki viliwahi kuripoti kuwa Khashoggi aliteswa kabla ya kuuawa.

Saudi Arabia imebadilisha kauli yake ya awali kuhusu mkasa wa kutoweka na kuuawa kwa Khashoggi.

Habari za kutoweka kwake zilipoangaziwa kwa mara ya kwanza Saudi Arabia ilisema kuwa Khashoggi alitoka ndani ya ubalozi wake mjini Istanbul akiwa hai.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Lakini baadaye ikakiri kuwa aliuawa na watu hatari waliyokuwa wanatekeleza oparesheni ya kikatili.

Kufikia sasa Saudia imewakamata washukiwa 18 ambao inasema watashtakiwa nchini humo.

Uturuki inataka washukiwa hao wafunguliwe mashtaka katika taifa hilo kwasababu uhalifu ulifanywa katika ardhi yake.

Mataifa mengine yanasema nini?

Saudi Arabia imekosolewa vikali kufuatia mauaji hayo huku washirika wake wa karibu wakitaka kupewa majibu kuhusu mkasa huo.

Rais Trump amesema ''hajaridhika'' na kauli ya Saudia lakini hata hivyo hayuko tayari kuvuruga mkataba wa kuiuzia silaha taifa hilo.

Wanaharakati nchini Marekani wamezindua ombi la kutaka jina la sehemu ya barabara iliyopo karibu na ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington igeuzwe kuwa bara bara ya Jamal Khashoggi.

Siku ya Jumatano waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema mauaji ya Khashoggi yalikuwa uhalifu na ukatili mkubwa.