Zimbabwe yagundua uwezekano mkubwa wa kuwa na mafuta na gesi, Rais Mnangagwa afurahia

Emmerson Mnangagwa

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Rais Emmerson Mnangagwa amesema hizo ni habari za kufurahisha sana kwa Zimbabwe

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametangaza kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa mafuta na gesi asilia kaskazini mwa taifa hilo.

Kampuni ya uchimbaji madini ya Australia kwa jina Invictus Energy kwa ushirikiano na serikali, sasa inatarajiwa kuanza uchimbaji kubaini iwapo mafuta hayo yanaweza kuchimbwa na kuuzwa kibiashara.

Kisima cha mafuta kitachimbwa na kampuni ya Invictus katika wilaya ya Muzarabani katika kipindi cha miaka miwili ijayo, rais huyo alisema.

Zimbabwe imekuwa ikishuhudia mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi katika zaidi ya mwongo mmoja.

Imekuwa kawaida kutokea kwa uhaba wa mafuta, na umeme kukatwa.

"Tumeshauriwa na Invictus kwamba matokeo ya upelelezi yana matumaini makubwa na yanaashiria kupatikana kwa mafuta na gesi eneo hilo,2 amesema Mnangagwa.

"Matokeo hayo kama yalivyotangazwa na Invictus ni habari za kufurahisha sana kwa taifa letu."

Waziri wa madini Winston Chitando amesema kisima hicho, ambacho kitachimbwa takriban 240km kaskazini mwa mji mkuu Harare kitachimbwa kwa gharama ya $20m (£15m), kwa mujibu wa sirika la habari la Reuters.

Zimbabwe ina utajiri wa madini mengine lakini haijakuwa na mafuta wala gesi.

Mafuta yataipa Zimbabwe utajiri?

Na Shingai Nyoka, BBC Africa, Harare

Miaka 25 baada ya kampuni ya mafuta ya Mobil kufanya upelelezi wa kutafuta mafuta na kuondoka mikono mitupu, teknolojia mpya inaonekana kuonyesha kuna mafuta kazkazini mwa Zimbabwe, karibu na mpaka wake na Msumbiji.

Upelelezi bado uko katika hatia za awali, lakini serikali ambayo imeishiwa na pesa inaonekana kutaka kutumia habari hizo kufufua matumaini ya wananchi katika taifa lao huku mgogoro wa kiuchumi ukiendelea kuuma.

Raia wamekuwa wakilalamikia kuenea kwa ufisadi na umaskini.

Invictus wanatarajiwa kuchimba kisima katika miaka michache ijayo ndipo ugunduzi wa mafuta hayo uthibitishwe.

Baadaye, itaingia kwenye mkataba wa kugawana mapato na serikali.

Hata kama uchimbaji wa mafuta ya kuuzwa utaendelea, haiwezi kutarajiwa kwamba utajiri huo utafikia kila raia.

Zimbabwe ina madini mengi ya platinum na almasi, lakini manufaa ya mapato yake huwa hayawafikii raia wa kawaida.

Hii ni kutokana na ufisadi na sera duni ambazo husababisha baadhi ya madini hayo kusafirishwa nje ya nchi yakiwa bado ghafi.

Chini ya Robert Mugabe, aliyelazimishwa kujiuzulu mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuongoza kwa miaka 37, kulikuwa na mpango wa sera ya kuanzisha viwanda vya madini ndani ya nchi kwa lengo la kuongeza mapato na ajira kwa wenyeji. Lakini hilo halikufua dafu.