Asia Bibi: Wakili wa Mkristo aliyefutiwa adhabu ya kifo nchini Pakistan kwa kuhofia maisha yake

Waandamanaji wanataka hukumu ya kifo dhidi ya Asia Bibi kudumishwa

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Waandamanaji wanataka hukumu ya kifo dhidi ya Asia Bibi kudumishwa

Wakili aliye mwakilisha mwanamke mkristo aliyeondolewa mashtaka ya kifo baada ya kuzuiliwa kwa miaka minane ametoroka nchini Pakistan kwa kuhofia maisha yake.

Saif Mulook ameliambia shirika la habari la AFP kwamba alilazimika kuondoka nchin humo ili aweze kumwakilisha mteja wake Asia Bibi, ambaye mahakama iliamuru achiwe huru siku ya Jumatano.

Maafisa nchini Pakistan wamemzuilia Bibi kuondoka nchini ili kusitisha maadamano ya vurugu dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

Asia Bibi alifungwa mwaka 2010 baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka kumkashifu mtume Muhammad baada ya kulumbana na majirani zake.

Mwanamke huyo amekuwa akisisitiza kuwa hana hatia lakini ametumikia kifungo cha miaka nane kwenye chumba cha peke yake jela.

Mapema wiki hii bwana Mulook aliiambia BBC kuwa anahitaji kuondoka nchini humo kwa kuhofia usalama wake.

Waziri wa habari wa Pakistan, Fawad Chaudhry ameitetea serikali dhidi ya madai kwamba makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na chama cha kiislamu yanaelekea kuitumbukiza taifa hilo katika mgogoro wa kidini.

Amesema serikali ''Itachukuwa hatua zote muhimu'' kuimarisha usalama wa Asia Bibi.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mume wake Asia Bibi na binti yake wamedai kuhofia usalama wao nchini Pakistan

Bwana Mulook, hata hivyo ameyataja, makubaliano hayo kuwa "machungu".

"Hawawezi kutekeleza amri ya mahakama ya juu zaidi ya nchi," aliiambia shirika la habari la AFP kabla ya kuabiri ndege ya kuelekea Ulaya.

Wakili huyo pia amesema kua aliamua kuondoka nchini Pakistan kwa sababu "ni vigumu" kuendelea kuishi nchini humo, akiongeza kuwa ataendelea kumpigania vita vya kisheria mteja Asia Bibi.

Ameliambia gazeti la Pakistan Express Tribune kwamba atarejea nchini humo kumtetea mteja wake - lakini anataka serikali kumhakikishia usalama wake.

Chanzo cha picha, ARSHAD ARBAB

Maelezo ya picha,

Maandamano yalifanyika katika maeneo mbalimbali

Hukumu hiyo ya kihistoria tayari imesababisha maandamano yenye ghasia kutoka kwa makundi ya kisiasa yanayounga mkono sheria ya kukashifu dini.

Maandamano dhidi ya maamuzi ya mahakama yalifanyika katika miji ya Karachi, Lahore, Peshawar na Multan.

Makubaliano kati ya serikali na chama cha kiislamu cha TLP ni yapi?

Waandamanaji wote waliyokamatwa tangu Asia Bibi aachiliwe huru nao waachiliwe, na dhulma zozote dhidi yao kuchunguzwa.

Serikali pia atanzisha mchakato wa kisheria wa kumweka bi Asia Bibi katika orodha ya watu watakaopigwa b=marufuku kuondoka Pakistan.

Kwa upande wake chama cha TLP kitawaomba wafuasi wake kusitisha maandamanona kudumisha amani.

Awali mamlaka ilisema kuwa Bibi anapangiw kuachiliwa huru wiki hii.

Ni jambo gani ambalo Asia Bibi alishutumiwa?

Kesi ya Asia Bibi ambaye jina lake halisi ni Asia Noreen ilianzia kwenye malumbano na kikundi cha wanawake mwezi Juni 2009.

Wanawake hao walikuwa wanavuna matunda na ugomvi ulizuka kuhusu ndoo ya maji. Wanawake wa Kiisilamu walisema kuwa alikuwa ametumia kikombe ambacho wasingeweza kukishika tena kwa sababu imani yake imekifanya kikombe hicho kutokuwa safi.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa malumbano hayo yalikuwa yanamtaka Asia Bibi kubadili dini yake na kuwa muislamu ndio sababu iliyompelekea kutoa kauli za matusi dhidi ya mtume Muhammad katika majibu yake.

Baadaye alipigwa mpaka nyumbani kwake wakati waliomshtaki wakidai kuwa alikiri kukashifu dini.Alifungwa baada ya polisi kufanya uchunguzi.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Watu wengi wanaunga mkono adhabu kati kwa watu wanaoukashifu Uislamu nchini Pakistan

Kukashifu dini kuna maana gani Pakistan?

Sheria ambazo ziliwekwa na Waingereza mwaka 1860 waliifanya kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kusumbua mikutano ya dini, kupita makaburini , kukashifu imani ya mtu kwa maksudi mtu kuharibu chombo kinachotumika kuabudia na hukumu yake kwa hayo yote ni kifungo cha miaka 10.