Mila za kiajabu: Jamii ya Pokot inavyowafunga uzazi wasichana kwa njia ya kitamaduni kaskazini magharibi mwa Kenya

Wanawake kufungwa

Katika jamii ya Pokot kaskazini magharibi mwa Kenya, upangaji uzazi kwa watoto umekuwa ukifanywa tangu jadi.

Jamii hii 'humfunga' mtoto wa kike kupitia tambiko ili kumzuia kupata mimba punde tu msichana anapoanza kupata hedhi.

Baba hushirikiana na mama ili kujua kama msichana ameanza kupata hedhi na kwa pamoja wanafanya tambiko hilo kwa siri bila msichana kujua.

Elizabeth Ndotuch anasema alifungwa na wazazi wake bila kujua, na anaamini kwamba njia hiyo hufanikiwa.

"Baada ya kuolewa na kuishi kwa muda, babangu alitumana mimi na mume wangu twende nyumbani. Tulipofika wakaandaa sherehe, wakanifungua... kumbe walinifunga na sikuwa najua."

Wanaume huhusika pakubwa katika kufanikisha utamaduni huu.

"Mama anaposema mtoto ameanza kupata hedhi, tunaungana na kutafuta wanawake wakongwe ili waweze kufanyiwa tambiko la kumfunga mtoto," anasema Francis Tiang'ole.

Hata hivyo anaongeza kuwa kizazi cha sasa kimepotoka kimaadili na kuacha kufuata utamaduni, jambo ambalo kwake anaamini ndilo linalochangia wasichana wengi kushika mimba wakiwa bado shuleni.

Mamake msichana huwakusanya pamoja wanawake wakongwe kutoka kwenye kijiji hicho na kufanya sherehe ya kufunga dawa hiyo.

Hedhi ya msichana huchanganywa na miti ya kiasili na kuwekwa ndani ya mfuko mdogo wa ngozi ya mbuzi unashonwa na kina mama hao wakongwe, huku wakiimba nyimbo za kitamaduni.

"Wanachukua damu ya hedhi, wanachanganya ya na miti za kienyeji kisha wanaweka kwa mfuko," Elizabeth Noruu anaelezea.

Mamake msichana hupewa mfuko huo kuuficha hadi wakati ambapo msichana wake ataolewa na sherehe nyingine kufanywa ili kumfungua msichana wake.

Jinsi ilivyo kawaida ya dawa yoyote huwa na madhara, hii pia iko na madhara.

Huwezi kusikiliza tena
Mila za kiajabu: Jamii ya Pokot 'inavyowafunga' wasichana wasishike mimba Kenya

Mwakilishi wa wadi ya Ribkwo eneo la Pokot, Daniel Tuwit, anasema wakati mwingine mama aliyeficha mfuko huo akifa bila mfuko kujulikana ulifichwa wapi, basi huenda mwanawe akasalia bila mtoto maishani.

"Mama akifa kama hakuna mtu anajua mahali aliweka dawa, msichana ataishi bila watoto," anasema.

Kisayansi, jambo kama hili haliwezi kutokea, lakini jamii hiyo inaendelea kuamini katika nguvu ya dawa hiyo.

Je, umekumbana na tamaduni na mila za aina hii? Unaamini kwamba zinafanikiwa?

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii