Stella Nyanzi: Mwanaharakati aliyekamatwa kwa 'kumtusi' rais Museveni

Stella Nyanzi
Image caption Dkt Stella Nyanzi

Msomi na mwanaharakati maarufu wa haki za wanawake nchini Uganda Stella Nyanzi amefikishwa mahakamani kwa mara nyigine tena na kushtakiwa ka kumtusi rais wa Uganda.

Nyanzi ambaye alikamatwa mwishoni mwa juma lililopita ameshtakiwa kwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii pamoja na kusambaza maandishi yaliyolenga kushusha hadhi ya rais Museveni pamoja na mamake.

Mawakili wake wamekuwa wakilalamikia hatua ya polisi kuendelea kumzuilia kwa zaidi ya saa 48 zinazohitajika kisheria.

Mmoja wa mawakili wake Issac Semakade amesema mteja wake amesomewa mashtaka yanayomkabili na kwamba anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Novemba 9.

Hapo jana msemaji wa polisi ya Uganda bwana Vincent Sekati aliambia BBC kuwa Bi Stela alikamatwa kutokana na maelezo aliyoyatoa kwenye mtandao wake akimtukana rais.

Anasema wala hakuishia hapo bali aliendelea mbele na kumtukana mamake rais'' Ni maelezo ambayo nisingependa kurudia kwa sababu yalikua machafu sana''.

Tukio hilo lilitokea tarehe 16 mwezi Septemba mwaka huu na msemaji wa polisi amesema mtu yeyote anaweza kutembelea ukurasa huo kujionea mwenyewe maneno aliyoandika mwanaharakati huyo ikiwa mtandao huo haujafungwa.

Ni siku ya tano sasa Dr. Stella Nyanzi anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kiraa kilichopo kitongoji cha mji wa Kampala.

Kumekuwa na maswali kuhusu mashtaka atakayofunguliwa mwanaharakati huyo anaepigania haki za wanawake.

Bwana Sekati anasema''Mashtaka tunayochunguza na makosa yake ambayo tunadhani hata mkurugenzi wa mashtaka atayakubali ni kuhusiana na kutumia vibaya mawasiliano chini ya sheria ya kutumia vitisho kwenye mtandao na kutumia vibaya kompyuta''

Msemaji wa polisi anadai kuwa awali Stella alikubali kutoa maelezo yake kwa polisi lakina baadae wakili wake akamkataza akitaka aelezee tu bila kutumia maandishi jambo ambalo halikubaliki.

Polisi inasema ikiwa Dkt Stella Nyanzi atakataa kutoa ushahidi wake kwa maandishi hilo si tatizo kwasababu itaendelea mbele na mchakato wa kumfungulia mashtaka.

Wanashikilia kuwa msomi huyo atatoa baadae maelezo yake akiwi mahakamani.

Haya yatakuwa ni mashtaka ya pili yanayomkabili Dkt. Stella Nyanzi.

Mwaka jana Dkt Nyanzi alikamatwa baada ya kuandika msururu wa ujumbe kwenye Facebook, ambapo alimshutumu rais Museveni kwa kushindwa kuwapa wasichana kutoka familia maskini vitambaa vya kutumia wakati wa hedhi.

Wasichana wengi nchini Uganda wameripotiwa kuacha masomo kutokana na aibu ya kukosa sodo.

''Ninakataa wazo kwamba mtu hawezi na hafai kukosoa watu wanaonyanyasa haki na mali za Waganda katika miaka 31 ya uongozi wa kidikteta wa familia moja," alisema katika ujumbe wake Facebook wakati huo.

Mwezi Machi mwaka 2017 Dkt Nyanzi alifutwa kazi katika chuo kikuu cha Makerere ambako alikuwa akihudumu kama mtafiti baada ya kumkemea mke wa rais, Janet Museveni.

Hivi karibuni Stella Nyanzi alishinda kesi dhidi ya chuo kikuu cha Makerere kuhusiana na kufutwa kwake kazi.Kulingana na maamuzi ya jopo la Chuo Kikuu,lililo sikiliza mamalamiko yake, Bi Nyanzi alitakiwa kurudishwa kazini mara moja, kulipwa mishahara yake yote na kufidiwa hasara aliyopata kutokana na kufutwa kazi.

Hata hivyo aliporudi kazini kama alivyoagizwa na mahakama alishikwa na kufunguliwa mashtaka.

Msomi huyo sasa amewasilisha shauri katika mahakama kuu akitaka Chuo Kikuu cha Makerere kiagizwe kumrudisha kazini.

Wakili wake ameiambia BBC kuwa '' Leo Stella amewasilisha hiyo kesi mahakamani akitaka arudishwe kazini'

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii