Trump amfuta kazi Session: Whittaker ateuliwa kuwa mwanasheria mkuu

Jeff Session Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jeff Session

Rais wa Marekani Donald Trump amemfukuza kazi Mwanasheria mkuu wa nchi hiyo Jeff Session.

Akitoa taarifa kupitia mtandao wa Twitter, Rais Trump amesema nafasi yake itashikwa kwa muda na mwanasheria Matthew Whittaker.

Katika ukurasa wake wa Twitter Rais wa Marekani amemshukuru Jeff Sessions kwa kazi yake hiyo na kumtakia kila la kheri.

Kwa upande wake, Jeff Sessions katika barua yake ya kujiuzulu, aliweka bayana kuwa uamuzi wa kuondoka katika nafasi hiyo haukuwa wake.

Katika barua isiyokuwa na tarehe alimjulisha Rais kwamba anawasilisha barua yake ya kujiuzulu kama alivyomtaka afanye hivyo.

Akimshukuru Rais Trump kwa uamuzi wake huo kwake akiongezea kwamba cha muhimu wakati wa uongozi wake kama mwanasheria mkuu wa serikali walirudisha na kuimarisha utawala wa sheria.

Kwa mujibu wa Afisa wa Ikulu ya Marekani John Kelly, alimuita bwana Sessions siku ya Jumanne kabla ya Rais Trump kuitisha mkutano wa habari kujadili matokeo ya uchaguzi wa muhula uliofanyika jana.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Marekani Donald Trump

Mara kwa mara Rais Trump alikuwa akimkosoa Bwana Sessions, Seneta wa zamani wa Republican na mfuasi wake wa mwanzo kabisa wakati wa harakati zake za kuwania kiti cha Urais.

Dalili za mwanasheria huyo kutimuliwa kazi zilionekana wazi kutokana na Rais Trump kuonesha uwezekano huo mapema.

Awali Rais wa Marekani alielezea kutofurahishwa kwake na hatua ya Mwanasheria huyo kujiondoa katika uchunguzi wa FBI kuhusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani 2016.

Alidai kuwa Sessions alikuwa na msimamo dhaifu.

Kufuatia hatua hiyo ya Rais kumfukuza kazi mwanasheria huyo, wanasiasa nchini humo wametoa kauli mbalimbali

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii