Waandishi wa habari wawili wa CPJ wanatuhumiwa kufanya kazi Tanzania bila kibali

Kushoto ni Muthoki Mumo, na wa kulia ni Angela Quintal Haki miliki ya picha CPJ
Image caption Kushoto ni Muthoki Mumo, na wa kulia ni Angela Quintal

Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imeelezea mazingira iliyowafanya waakilishi wawiili wa Kamati ya Kimataifa ya kuwalinda wanahabari CPJ, kukamatwa.

Msemaji wa idara hiyo Ally Mtanda amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema kuwa wafanyikazi hao walikiuka madhumuni ya ujio wao kama walivyoandika katika vibali walivyopewa wakati wakiingia nchini,kutokea Afrika Kusini.

Waakilishi hao wa CPJ walikamatwa na kuzuiliwa kwa muda kutokana na tuhuma za kufanya mkutano na waandishi wa habari, tofauti na madhumuni ya kufanya matembezi tu.

Bwana Mtanda hata hivyo amethibitisha kuwa, Muthoki Mumo na Angela Quintal, wamerudishiwa hati zao za usafiri.

Wawili hao pia wameruhusiwa kuendelea kuwepo nchini Tanzania kwa sababu bado vibali vyao vinawaruhusu kuendelea kuwa nchini humo hadi Januari 9 mwakani.

Awali Idara ya kimataifa wa uhusiano na ushirikiano nchini Afrika Kusini (DIRCO) ilisema waandishi hao wamerudi kwenye hoteli yao.

"Balozi wa Afrika Kusini Bw Thami Mseleku amekutana nao na kuzungumzia kile kilichotokea.

Kisha atazungumza na mamlaka za Tanzania. Msemaji wa DIRCO Bw Ndivhuwo Mabaya, alizungumza na Bi Quintal leo asubuhi," Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Afrika Kusini ilisema kwenye mtandao wa Twitter.

Chama cha wahariri wa habari nchini Kenya kimelaani kukamatwa kwa waandishi hao wa habari na kutoa wito kwa serikali ya Tanzania kuwaruhusu kukamilisha kazi yao.

Maafisa waliojitambulisha kama wafanyakazi wa idara ya uhamiaji nchini Tanzania waliwakamata Quintal na Mumo kwenye hoteli yao mjini Dar es Salaam, kwa mujibu wa CPJ.

Maafisa hao walichukua bidhaa za wawili na hawakurudisha pasi zao za usafiri wakati waliombwa.

Quintal na Mumo kisha wakatolewa hotelini na kupelekwa eneo ambalo halikujulikana, Mara baada ya kukamatwa, ujumbe wa twitter ulitumwa kutoka akaunti ya Quintal, ukisema "Mungu ni mkuu tumeachiliwa na tunarudi hotelini," na kuzua hofu kuwa mtu fulani alitumia simu zake.

"Ujumbe wa @angelaquintal haukutumwa naye," aliandika mpwa wake Quintal, Genevieve Quintal, ambaye pia ni mwandishi wa habari. "Hii inaonyesha kuwa kuwa kuna mtu anatumia simu yake."

Akaunti za Twitter za Quintal na Mumo zimezimwa tangu wakati huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii