Kenya SGR: Tamu na chungu ya usafiri wa reli mpya baina ya Mombasa na Nairobi

  • John Nene
  • BBC Swahili

Treni ya kisasa ya SGR imeleta raha na karaha miongoni mwa Wakenya.

Wakati abiria wengi wanafurahia treni hiyo kwa kupunguza muda wa usafiri kufukia saa sita tu badala ya siku nzima. Kwa upande wa mizigo treni hiyo imesababisha wengi kupoteza kazi zao mjini Mombasa.

Rais Uhuru Kenyatta alizindua treni ya abiria mwezi Mei mwaka jana katika kituo cha Miritini mjini Mombasa, na mwezi wa Julai treni hiyo ikaanza kusafirisha abiria.

Ujenzi wa reli hiyo ya SGR umenufaishwa na mkopo wa dola bilioni 3.2 kutoka kwa serikali ya China, kiwango ambacho baadhi ya Wakenya hasa wanasiasa wa upinzani walidai kiko juu sana ikilinganishwa na reli ya kilomita 756 ya Ethiopia iliyogharimu dola bilioni 3.4 na ya Kenya ni kilomita 472.

Isitoshe ya Ethiopia ni ya umeme na gari lao ni la kisasa zaidi.

Mwandishi wa BBC John Nene hivi karibuni alitumia usafiri huo kuelekea Mombasa na kukutana na abiria kadhaa ambao hawakuficha hisia zao juu ya gari hilo moshi la kisasa kabisa.

Nelson Nyamau ameiambia BBC kuwa anaipenda SGR kwa sababu ya kutumia muda mfupi baina ya Mombasa na Nairobi.

"Tumefurahia sana kusafiri na SGR kwa sababu ya usalama sio kama barabarani ajali zimezidi. Tunaomba zingine kama mbili hivi ziongezwe ya saa tano na ya saa nane ikiwezekana ya usiku pia. Hatahivyo naomba tupate gari zinazosafiri kwa kasi zaidi ya hii tufike Mombasa kwa saa mbili hivi," amesema Nyamau.

Maelezo ya picha,

Abiria wakipiga picha ndani ya treni

"Mara ya kwanza nilisafiri na watoto wangu tulifurahi sana hatukuamini tuko Kenya. Tunamshukuru Rais wetu kwa gari hili ambalo limepunguza masaa ya kusafiri, hivi punde nitawasili Voi.Lakini sijafurahishwa na kununua chakula na vitafunio vingine hasa kwa first class kwa sababu tunalipa pesa nyingi. Elfu tatu (dola 30) za Kenya ni nyingi. Tunataka iwe kama vile kwenye ndege tunapata kinywaji na kitafunwa,'' amesema Ann Mwadime.

Kwamujibu wa Philip Mainga ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirika la reli la Kenya ameiambia BBC kuwa usafirishaji wa abiria upo juu toka huduma hiyo ilipoanza mwaka jana.

Kwa siku abiria 6,000 husafirishwa na mipango ya kuwa na safari ya usiku ipo katika hatua za mwisho kufanikishwa.

"Changamoto yetu kubwa ni abiria wengi kupita kiasi. Gari zinajaa kila siku kama mwezi huu wa Novemba na Disemba tayari zimejaa.Baadae tutaanzisha gari la kutumia umeme kwa sababu hii reli imetengenezwa kwa njia ya kisasa. Najua kunachangamoto ya umeme wa kutosha lakini hilo serikali inashugulikia."

Maelezo ya picha,

Kituo cha kisasa cha kusubiria treni

Jambo lingine la kufurahisha ni kwamba treni hii ya SGR imewapa ajira Wakenya. Cynthia Damaris na Irene Chebet ni miongoni mwa walionufaika. Wao ni wahudumu wa treni.

"Kama nisingepata kazi hapa ningekua nina hustle (nahangaika) kama vijana wengine lakini nashukuru serikali kwa mradi huu, sasa nina kazi na ninasaidia wazazi wangu,'' anasema Chebet.

Damaris ndiye mkuu wa wahudumu, kazi anayosema aliipata kwa haki bila kutegemea mtu amsaidie.

Kuhusu uhusiano wao na Wachina, Damaris anasema: "Uhusiano wetu ni mzuri. Hivi sasa wameanza kurudi kwao pale wanaona tumejifunza kazi wakatosheka.

La muhimu tumejifunza kwa Wachina ni nidhamu hasa gari linapoondoka lazima kila mtu afike kituoni mapema. Tulipoanza tulikua na shida sana hasa kwa wasafiri wa kutoka Mombasa kuelekea Nairobi. Mara nyingi walikua wanaachwa."

Sio Wakenya wote hatahivyo wamechangamkia SGR. Mercy Ireri ni mmoja wao akisema treni hiyo hajaifurahia hata kidogo.

"Kwanza kusafiri hadi Miritini ni shida tupu tukitilia maanani msongamano wa magari. Mtu inabidi utoke mapema nyumbani kwa hivyo sikubaliani na wale wanasema SGR imepunguza masaa ya kusafiri,'' anasema Ireri.

"Shida nyingine kubwa viti ni vya kuangaliana kwa second class (daraja la pili). Siku hiyo nikisafiri niliangaliana na mwanamume ana miguu mirefu sana mpaka ilikua inafika kule nimeketi. Yule nilikua naye kiti changu ni mwanamume mwingine ana mwili kubwa sana ananifinya saa zote na miguu yake anaiweka sehemu ya watu kupitia kwa sababu ni mirefu. Ilibidi nitoke hapo. ''

Kuna wengine kwa hivi sasa wanaumia kwa kukosa ajira tangu treni ya mizigo ianze kazi mwezi Januari mwaka huu.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha wamiliki ya malori ya kusafirisha mizigo, KTA, Newton Wang'oo hii inatokana na uamuzi wa uongozi wa bandari kuwalazimisha wanachama wake kusafirisha mizigo Nairobi na SGR.

"Watu wengi wamepoteza kazi kuanzia madereva na wale wameajiriwa na makampuni ya kusafirisha mizigo," anasema Wang'oo ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya kusafirisha mizigo, One2One.

"Kwangu bado hatujaumia kwa sababu tunasafirisha mizigo nje ya nchi. Hapo hawajagusa bado wanashugulika na mizigo ya kwenda Nairobi. Watu wameuza magari tayari maanake hayana kazi sasa. Inasikitisha sana.''

Maneja msimamizi wa ajira wa miongoni mwa makampuni ya kusafirisha mizigo yajulikanayo kama CFS (Container Freight Stations) Yusuf Mwinyi anathibitisha asemayo Wang'oo kuhusu watu kutimuliwa kazini.

"Kwangu tumefuta watu 85 kati ya 125 tuliowaajiri, na waliobaki hawana uhakika wa kuendele zaidi. Kuna shida kubwa sana Mombasa watu hawajui. Vijana wa maskani wamerudi huko baada ya kufutwa kazi. Hapa kuna hatari kubwa sana kama wataendelea hivyo bila kazi."

Maelezo ya picha,

Mwenyekiti wa chama cha wamiliki ya malori ya kusafirisha mizigo, KTA, Newton Wang'oo amelalamikia kushuka kwa biashara

Baadhi ya waliofutwa kazi ni Diana Aura aliyekuwa akifanya kwa kampuni ya Consolbase CFC.

"Ni jambo la kuudhi kuona serikali yetu ikituletea shida zote hizi bila kujali tutaenda wapi.Mimi na watoto wangu wawili sasa tunajiandaa kuhamia Nairobi nijiunge na mume wangu kwa sababu mizigo yote inapelekwa huko lakini maisha ya Nairobi magumu sana.

Mkurugenzi mkuu wa Weston Logistics Limited Salim Nassib Mbarak ana uchungu na SGR akidai imechukua biashara yao yote.

"Tunahisi serikali inafanya hivyo kulipa mkopo wa serikali ya China lakini bado hawatafaulu sana huo mkopo ni wa juu sana. Kwanini tulazimishwe kutumia SGR? Kuna wengi sana wanapenda kutumia lori,'' anasema Mbarak.

Madai ya Mbarak yamekanushwa na mkurugenzi wa operesheni wa Halmashauri ya Bandari Capt. William K. Ruto.

"Huo ni uongo mtupu ati sisi tumewalazimisha kutumia SGR. Kulingana na takwimu zetu asilimia sabuini ya wafanya biashara wameamua kutumia SGR sio sisi tumewaambia ni kupenda kwao,'' anasema Ruto.

"Wengi wamefurahia huduma yetu ya gari la SGR, kwa siku moja karibu lori nane mpaka kumi zinapeleka mizigo Nairobi.''

Maelezo ya picha,

Mwenyekiti wa kampuni ya Coast Bus Mohamed Ajaz Mirza anasema SGR imeathiri pakubwa biashara yao

Mwenyekiti wa kampuni ya Coast Bus Mohamed Ajaz Mirza anasema SGR imerudisha biashara yao nyuma sana kutokana na abiria wengi kukimbilia treni hiyo.

"Biashara si nzuri kabisa...Sisi hatujafuta kazi madereva wetu ni wao wenyewe wanaamua kuondoka kwa sababu labda anaona hapati ile posho yake. Kati ya magari yetu 39 ni kama 19 hivi yako barabarani lakini tunapanga mikakati ya kuboresha biashara yetu tuwe na mambo mapya."