Martin Fayulu achaguliwa kuwa mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa urais DRC

uchaguzi drc Haki miliki ya picha AFP
Image caption Martin Fayulu kuwakilisha upande wa upinzani katika uchaguzi mkuu ujao nchini DRC

Viongozi wakuu wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo wamemchagua mfanyabiashara maarufu nchini humo Martin Fayulu kama mgombea wao katika kinyang'anyiro cha uraisi katika uchaguzi unaotarajiwa Decemba 2018.

Martin Fayulu ataingia kwenye uchaguzi huo kutoshana nguvu na mgombea mteule wa serikali, bwana Emmanuel Ramazani Shadary ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani nchini humo.

Uteuzi wa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 61 Martin Fayulu umekuja baada ya siku kadhaa za mazungumzo baina ya viongozi wakuu wa vyama saba vya upinzani yaliyofanyika mjini Geneva nchini Uswiss.

Mwanasiasa huyu wa upinzani chama chake kinaitwa ACD, na inaarifiwa kuwa mnamo uchaguzi wa mwaka 2011 alimfanyia kampeni kiongozi wa upinzani marehemu Ettiene Tshisekedi.

Raisi anayeondoka madarakani , Joseph Kabila, ameamua kutogombea tena muhula mwingine wa uongozi madarakani.

Image caption Raisi anayemaliza muda wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila

Ingawa inafahamika wazi kuwa aligoma kuondoka madarakani baada ya muhula wa uongozi mnamo mwaka 2016 na kujitetea kuwa wakati huo haukuwa mwafaka kuachilia madaraka na kuitisha uchaguzi kwani ulikuwa ni wakati wa hatari.

Vikundi vya vyama vya upinzani, vilichukulia mtazamo huo kama mbinu za raisi Kabila kuongeza muda wake madarakani.Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unatarajiwa kufanyika tarehe 23, mwezi December.

Martin Fayulu ni nani?

Mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Martin Fayulu ni miongoni mwa watu wenye ushawishi katika siasa nchini.

Ni mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 61.

Martin mbali ya kujihusisha na masuala ya kisiasa ni mfanya biashara maarufu nchini Congo, miongoni mwa vitega uchumi vyake ni umiliki wa hoteli.

Alisomea nchini Marekani, Ufaransa lakini pia aliwahi kufanya kazi katika makampuni makubwa ya simu nchini Marekani.

Alikuwa mstari wa mbele katika kumfanyia kampeni ya kisiasa aliyekuwa kiongozi wa upinzani marehemu Ettiene Tshisekedi.

Aliwahi kukamtwa mara kadhaa katika maandamano ya upinzani nchini.

Wengi wameshangazwa na kuchaguliwa kwa Fayulu kando na kwamba ni mbunge, wengi wanamtazama kama mfanyabiashara kuliko kiongozi wa upinzani.

Wagombe wengine wawili wa upinzani Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe, sasa watampigia upatu Fayulu.

Uamuzi wa upinzani kuungana na kumchagua mgombea mmoja ni muhimu kwasababu katika uchaguzi wa duru moja kuwepo wagombe wengi kutavunja hesabu ya uwingi wa upinzani na huenda ukaishia kushindwa.

Wakikutana kwa mara ya kwanza wote pamoja, viongozi hao wa upinzani pia wamekubaliana kuidhinisha mpango na kikosi cha pamoja.

Kampeni zinatarajiwa kuanza baadaye mwezi huu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii