Uganda yatuzwa kwa kupiga hatua katika uzazi wa mpango

Uzazi wa mpango Haki miliki ya picha Serikali Rwanda

Uganda imetambuliwa kwa jitihada zake katika kufanikisha afya ya uzazi wa mpango.

Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uzazi wa mpango na kuhakikisha pia kuwa jamii inazifikia huduma hizo.

Katika mkutano wa zaidi ya wajumbe 4000 wa kimataifa kuhusu afya ya uzazi wa mpango uliofanyika Kigali Rwanda, washikadau walihimizwa kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza uzazi wa mpango na kuwahusisha vijana zaidi katika huduma ya afya kuhusu uzazi.

Kauli nzito iliyojitokeza miongoni mwa wajumbe katika kikao hicho ni kwamba kuna haja kwa vijana, hususan wasichana na wanawake, kulengwa katika mbinu zitakazosaidia kuyaokoa maisha yao.

Kufikia Julai 2018, idadi jumla ya wanawake na wasichana wanaotajwa kutumia mbinu za kisasa za uzazi wa mpango katika nchi 69 zenye kipato kidogo duniani, iliongezeka hadi zaidi ya milioni 317 kwa mujibu wa shirika la FP2020.

Haki miliki ya picha Serikali Rwanda
Image caption Mkutano wa kimataifa umekamilika Kigali Rwanda kuhusu uzazi wa mpango

Uganda inavyopiga hatua katika uzazi wa mpango

Uganda inasema imepiga hatua kubwa katika uzazi wa mpango tangu mkutano wa kimataifa uliofanyika London mnamo 2012.

Serikali inaeleza kwamba ufanisi mkubwa unatokana na usaidizi kutoka kwa washirika kama vile mashirika ya kijamii na ya kidini.

Waziri wa afya Dkt Jane Ruth Achieng, ameeleza kwamba licha ya kuwa umri wa kuridhia kushiriki tendo la ndoa ni miaka 18, wizara yake inatambua fika kwamba ukweli ni kuwa ndoa na mimba za utotoni bado ni tatizo.

" Ni lazima tuisisitize elimu ili wasichana waifahamu hatari ya kujihusisha na tendo la ndoa na kupata uja mzito katika umri mdogo. Hilo litahakikisha kwamba uamuzi wao utatokana na kwamba wanaijua athari ya wanachokifanya." Ameeleza waziri alipopokea tuzo kwa Uganda mjini Kigali.

Uganda inaonekana kupiga hatua tangu iidhinishe, ikaribishe uvumbuzi unaoimarisha kufikiwa na kukubalika kwa mbinu za kupanga uzazi.

Haki miliki ya picha PATH/PATRICK MCKERN
Image caption Sindano ya Sayana - kifaa kinacho wawezesha wanawake kujipiga sindano wenyewe za kuzuia uja uzito.

Mfano wa kupigiwa upatu ni sindano ya Sayana.

Ni kifaa kilichovumbuliwa kinacho wawezesha wanawake kujipiga sindano wenyewe za kuzuia uja uzito.

Uganda, ni mojawapo wa nchi nne ambazo kifaa hicho kilijaribiwa katika awamu ya kwanza ya matumizi tangu zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Mtumiaji mmoja kutoka kijiji kilichopo kaskazini mwa Uganda, mama ya watoto wawili, Bi Fiona, ameeleza namna ambavyo awali alilazimika kusafiri kwa pikipiki,masafa marefu kufikia zahanati kupata huduma.

Haki miliki ya picha AFP

Amesema: " Nahisi nina udhibiti mkubwa wa maisha yangu sasa na pia mustakabali wangu kama mama mzazi."

Hatahivyo ufanisi huu bado unaandamwa kwa changamoto nchini.

Wataalamu wanasema kando na kupunguza idadi ya vifo vya mama na mwana wakati wa kujifungua kutokana na mimba za utotoni, lakini pia kuna haja ya kuhakikisha huduma zinazohusiana na elimu kuhusu uzazi na tendo la ndoa inatolewa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii