Jamal Khashoggi: CIA 'yamlaumu mwanamfalme wa Saudia '

mwanamfalme Mohammed bin Salman Haki miliki ya picha AFP
Image caption Saudi Arabia inasema mwanamfalme Mohammed bin Salman hakuhusika na mauaji ya Khashoggi

Shirika la ujasusi la Marekani(CIA) linaamini kuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia ndiye aliyeamuru kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Vyanzo kutoka shirika hilo vinasema kuwa vina ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa huenda mrithi huyo wa ufalme wa Saudi Arabia alijuwa kuhusu mipango ya kumuua Khashoggi.

Kauli hiyo ya CIA, iliyoripotiwa kwanza na gazeti la Washington ni ya hali ya juu kabisa kutolewa na Marekani mpaka sasa, ikimuhusisha moja kwa moja mtawala huyo mtarajiwa wa Saudi Arabia na mauaji hayo.

Ikulu ya Marekani na Wizara ya Mambo ya nje hazijasema lolote kuhusiana na suala juu hilo.

Msemaji wa ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington amesema tathmini hiyo ni ya uongo.

"Tumekuwa na tukituhumiwa kwa madai mbalimbali na mpaka sasa hatujabaini lolote la msingi kuhusu madai hayo,"

Haki miliki ya picha EPA

Siku ya Ijumaa (Novemba 17), Mwanamfalme Khaled aliandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba mawasiliano yake ya mwisho na Khashoggi yalikuwa kupitia ujumbe wa maandishi ya simu ya mkononi tarehe 26 Oktoba 2017, takribani mwaka mmoja kabla ya kifo cha mwandishi huyo wa habari.

Huku hayo yakijiri ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu nchini Saudi Arabia imemaliza uchunguzi wake juu ya nani aliyeamuru kuuawa kwa mwanahabari Jamal Khashoggi.

Uchunguzi huo umebaini kuwa mauaji hayo yaliamuriwa na afisa mwandawizi wa idara ya usalama wa taifa ya Saudia ambaye alipewa kazi ya kumshawishi Khashoggi kurejea Saudia.

Mwanahabari huyo ambaye alikuwa kinara wa kumkosoa Bin Salman alikimbia Saudia mwaka 2017 na kuhamia Marekani.

Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hiyo, Khashoggi alidungwa sindano ya sumu baada ya purukushani kuibuka ndani ya ofisi ndogo za ubalozi wa nchi hiyo jijini Istanbul, Oktoba 2, 2018.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Watu wakishiriki ibada ya wafu ya mwanahabari Jamal Khashoggi

Tayari ibada ya wafu imefanyika nchini Saudi Arabia na Uturuki

Salah,Mwana wa kiume wa Khashoggi, aliungana na mamia ya waombolezaji waliyohudhuria ibada mjini Jeddah huku mamia ya waombolezaji wengine wakifanya ibada hiyo ya maombi katika miji mitakatifu ya Mecca na Medina.

Watu 11 tayari wameshafunguliwa mashtaka kutokana na mkasa huo na waendesha mashtaka wanataka watano kati yao kupatiwa adhabu ya kifo.

Uchunguzi unaendelea kwa watu wengine 10 ambao wanshukiwa kushiriki mauaji hayo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Salah, mwana wa kiume wa Khashoggi akiwakaribisha waombolezaji katika mji wa Jeddah sik ya Ijumaa

Katika mkutano na waandishi wa habari, Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Saudia Shalaan bin Rajih Shalaan amesema mwili wa Khashoggi ulikatwa katwa ndani ya ubalozi baada ya kuuawa.

Vipande hivyo vya mwili vilikabidhiwa kwa mshirika wao ambaye ni raia wa Uturuki nje ya ubalozi.

Tayari picha ya kuchora ya mshirika huyo imetolewa na uchunguzi unaendelea kujua vipande hivyo vya mwili vilipelekwa wapi.

Bwana Shalaan hata hivyo hakuwataja wale ambao wamefunguliwa mashtaka juu ya tukio hilo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii