Masharti ya Benki ya Dunia kwa Tanzania kabla ya kuipa mkopo ni yapi?

Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem walifanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam Haki miliki ya picha IKULU TZ
Image caption Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem walifanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem amesema kuna masharti wamekubaliana kabla Tanzania haijapewa mkopo wa Dola 300 milioni za Marekani kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk Ghanem alisema benki hiyo inatoa fedha kwa ajili ya wasichana wote bila kujali hali zao, hivyo kuwatenganisha kwa kigezo cha ujauzito .

Dk Ghanem amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema: "Mradi wa Tanzania haujajadiliwa. Lakini kwa mazungumzo tuliyofanya, utajadiliwa Serikali itakapotimiza masharti tuliyokubaliana.

Baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam juzi, Rais John Magufuli alisema benki imekubali kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.

Awali chanzo ndani ya benki hiyo kiliiambia BBC Swahili kuwa sababu kuu mbili za zuio hilo zilikuwa ni mosi, uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

Haki miliki ya picha IKULU TZ
Image caption Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem walifanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam

Pili, maboresho ya Sheria ya Takwimu yaliyopitishwa na Bunge la Tanzania Septemba 10 ambapo pamoja na mengine, inakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu rasmi za serikali.

Adhabu ya kufanya hivyo ni faini ya Dola 6,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Vilevile, Dk Ghanem alisema walizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Takwimu na wameishauri Serikali kuhakikisha wadau wake wanakuwa huru kukusanya na kutumia takwimu.

Siku ya Ijumaa Rais Magufuli alisema pesa hizo "hazijafyekelewa mbali" kama baadhi ya watu "wasiotutakia mema walivyosema."

Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa Ghanem alikwenda Tanzania kuthibitisha kuwa Benki ya Dunia haitaiacha nchi hiyo.

Haki miliki ya picha IKULU TZ
Image caption Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem walifanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam

"Namshukuru Dkt. Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa, na pia Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.

Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha." alisema Rais Magufuli.

Mazungumzo kati ya Magufuli na Ghanem yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Tanzania Bi. Bella Bird.

Mada zinazohusiana