Wanawake 100 wa BBC 2018: Mtanzania Juliet Sargeant mbunifu wa kurembesha bustani ni miongoni mwao

Some of the BBC's 100 Women 2018

BBC imetangaza orodha ya wanawake 100 bora wenye ushawishi kutoka kote duniani kwa mwaka 2018.

Kwa usaidizi wao tutaangazia masuala tofuati, ikiwemo kutumia ghadhabu kushinikiza hatua kuchukuliwa, na kuwafichua wanawake ambao hawakuangaziwa katika hostoria.

Wakiwa ni baina ya umri wa miaka 15 hadi 94, na kutoka zaidi ya mataifa 60, Msimu wa Wanawake 100 bora wa BBC inawajumuisha viongozi, wahamasishaji na mashujaa wa kila siku.

Baadhi watakuwa wakitueleza katika Pakacha la Uhuru - kikapu chetu cha kidigitali kuhusu masuala yote ambayo wanawake wanahisi yanawazuia kujiendeleza.

Wengine watatuletea hadithi za ufanisi dhidi ya vikwazo - kuanzia Mwanamke wa Uingereza aliyetumia kifungo chake kuanzisha biashara, hadi msichana wa Afghanistan ambaye nusra abadilishwe akifikiriwa kuwa ni mvulana.

Juliet Sargeant, 53 - Mbunifu wa kurembesha bustani, Tanzania.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Juliet Sargeant ametuzwa kwa harakati zake za kutaka utangamano katika kilimo cha maua

Juliet Sargeant amezaliwa nchini Tanzania na ni mbunifu anayerembesha bustani.

Juliet ni daktari pia ambaye sasa anajihusisha na kutengeneza bustani ili watu 'wahisi vizuri wanapozitembelea kama kwa mfano wa uzuri unaoonekana'.

Alituzwa kwa kulipangia bustani iliyodhihirisha na kuhamasisha kuhusu utumwa mambo leo.

Bustani hiyo ilijumuisha milango kadhaa na mti wa Mwaloni - iliyodhihirisha kukamatwa, na mti ambao William Wilberforce alikaa chini alipo apa kusaidia kumaliza biashara ya utumwa.

Bustani hiyo ilibuniwa kuadhimisha siku ambayo bunge Uingereza lilipitisha sheria ya 2015 ya kupambana na utumwa wa mambo leo.

"Nilitaka kusisitiza kwamba ni uhalifu wa kufichwa, nyuma ya milango iliyofungwa , kwahivyo ndani ya bustani kuna milango iliyo na rangi za kung'ara, iliyo na utepe katika pande nne," amesema Juliet.

Kwa mujibu wa Bi Sargeant kuna matumaini makubwa katika mti huo wa Mwaloni kwasababu " ni chini ya mti kama huo ambapo William Wilberforce alisimama alipojitolea maisha yake kusitisha utumwa".

Wengine kwenye orodha ya wanawake bora 100 wa BBC

Abisoye Ajayi-Akinfolarin, 33 - Mjasiriamali katika masuala ya kijamii, Nigeria.

Abisoye ni muasisi wa GirlsCoding, shirika lisilo la serikali linalowafunza wasichana namna ya kupamba na kuunda tovuti zinazosaidia kutatua matatizo katika jamii.

Nimco Ali, 35 - Mwandishi na mwanaharakati, Somaliland.

Nimco ametuzwa kwa harakati zake za kupambana na ukeketaji.

Noma Dumezweni, 49 - Muigizaji eSwatini (Iliyokuwa Swaziland).

Noma ni mwanamke wa kwanza kumuigiza Hermione Granger katika filamu ya Harry Potter and The Cursed Child, inayoonyeshwa katika ukumbi wa West End London na Broadway, New York.

Shrouk El-Attar, 26 - Mhandisi wa Electroniki, Misri.

Shrouk ni mkimbizi ambaye anafanya kazi ya uhandisi, anayenengua viuno kuhamasisha na kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Msiri.

Raghda Ezzeldin, 26 - Mpiga mbizi, Misri.

Raghda ameweka rekodi ya kupiga mbizi katika kina kirefu cha maji pasi kutumia vyenzo vya kumsaidia kupumua akiwa ndani ya maji.

Mamitu Gashe, 72 - Mhudumu mkuu/Daktari wa upasuaji wa fistula, Ethiopia.

Mamitu sasa ni daktari anayetambulika kimataifa wa upasuaji kurekebisha tundu linalojitokeza katika sehemu za siri au Fistula, baada ya kutibiwa kwa tatizo hilo mwenyewe.

Thando Hopa, 29 - Mwanamitindo,Wakili, Mwanaharakati, Afrika kusini.

Thando ni wakili anayetetea uwakilishi sawa na utangamano. Yeye ni mtu wa kwanza mweusi kuangaziwa katika chapisho la kalenda ya Pirelli 2018, Afrika kusini.

Hindou Oumarou Ibrahim, 35 - Mwanamazingira na mteteaji haki za watu wa asili na wanawake, Chad.

Hindou ni mwanamke wa asili nchini Chad, anayetetea kulindwa kwa mazingira na haki za watu wa asili katika kiwango cha kimataifa.

Ruth Medufia, 27 - Mfuaji Vyuma, Ghana.

Ruth ni mfuaji vyuma mwanamke anayeishi katika mitaa ya mabanda mjini na anatazamia kuwa mfano mwema kwa wasichana katika sekta ya ujenzi.

Amina J Mohammed, 57 - Naibu katibu mkuu Umoja wa mataifa, Nigeria.

Amina aliwahi kuwa waziri wa mazingira Nigeria na aliwahi pia kuwa mshauri maalum kwa katibu mkuu wa Umoja huo zamani, Ban Ki-moon.

Helena Ndume, 58 - Daktari wa macho, Namibia.

Helena amefanya upasuaji wa kurekebisha macho ya raia 35,000 nchini Namibia, bure bila ya malipo - baadhi kubwa ya wagonjwa aliowatibu sasa wanamuita "Daktari wa miujiza Namibia".

Olivette Otele, 48 - Mhadhiri wa Historia katika chuo kikuu cha Bath Spa, Cameroon.

Olivette ni mwanahistoria na msomi anayeshughulika na historia ya ukoloni wa Ulaya na tawala za uongozi wa baada ya utawala wa kikoloni.

Brigitte Sossou Perenyi, 28 - Mzalishaji makala ndefu ya televisheni, Ghana.

Brigitte ameshinda tuzo katika uzalishaji vipindi kwenye televisheni, aliyesimulia hadithi yake ya kuwa Trokosi nchini Togo - utamaduni wa kuwatumia wasichana kama watume kwenye mahekalu kama njia ya 'kutakasa madhambi' ya jamaa zao kwenya familia.

Fatma Samoura, 56 - Katibu mkuu wa FIFA, Senegal.

Fatma ni mwanamke wa kwanza na Muafrika wa kwanza kushikilia wadhifa wa katibu mkuu katika shirikisho la soka duniani Fifa.

Bola Tinubu, 51 - Wakili, Nigeria.

Bola ni wakili wa kibiashara aliyeanzisha huduma ya kwanza ya bure ya nambari za simu za usaidizi kwa watoto nchini Nigeria.

Je wanawake 100 ni nini?

BBC 100 Women huwataja wanawake 100 wenye ushawishi na wenye kutia moyo kote duniani kila mwaka na tunaangazia hadithi zao.

Umekuwa mwaka wenye umuhimu katika masuala ya haki za wanawake kote duniani, kwa hivyo mwaka 2018 msimu wa Wanawake bora 100 wa BBC, utaangazia wanawake waasisi wanaotumia ari , hasira na ghadhabu kushinikiza mageuzi halisi duniani.

Jumuika nasi kwenye Facebook, Instagram na Twitter na tumia #100Women

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii