Thamani ya Shilingi ya Tanzania yaporomoka kwa kasi, gavana wa BoT Florens Luoga atetea kutumiwa kwa jeshi Arusha

SHILINGI YA TANZANIA

Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imezidi kuporomoka na kufikia kiwango cha chini zaidi katika miaka mitatu iliyopita.

Dola moja kwa sasa ni wastani wa Sh2,300 mara ya mwisho kwa kiwango hicho kufikiwa ilikuwa ni Julai 2015 ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliingilia kati.

Mkurugenzi wa Masoko na Fedha wa BoT Alexander Mwinamila ameliambia Gazeti la The Citizen la Tanzania kuwa kuporomoka huko kwa thamani ya shilingi kulitarajiwa.

"Hali ya sasa si kitu cha kustaajabisha, na kwa kiasi imechangiwa na kuimarika kwa dola dhidi ya sarafu nyengine kwa siku za hivi karibuni."

Sababu nyingine zinazotajwa kuchangia kuporomoka huko kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ni kushuka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuingia kwa fedha za kigeni kutoka kwenye miradi ya wawekezaji.

Hata hivyo, wakati shilingi ikishuka, jana Jumatatu Novemba 19 katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanajeshi walitanda kwenye maduka ya kubadilishia fedha jijini Arusha.

Hali iliyowafanya baadhi ya wananchi washindwe kufanikisha biashara waliyokusudia.

Gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa hali hiyo ilianza kujitokeza kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka jioni huku kila duka likilindwa na walau askari wawili waliokuwa wamevaa kombati huku maofisa wanaodaiwa kuwa ni wa BoT.

Maduka hayo yote hayajafunguliwa hii leo. Japo ni sikukuu ya Maulid lakini Imekuwa kawaida kwa baadhi ya maduka hayo kufunguliwa walau kwa nusu siku kwenye siku za siku kuu.

Hakuna kauli rasmi iliyotolewa na mamlaka juu ya msako huo uliofanyika jijini Arusha.

Kwenye ukaguzi huo wa kushtukiza ambao hakuna mteja aliyeruhusiwa kuingia ndani ya maduka hayo kubadilisha fedha alizozitaka. Wote walielekezwa kwenda kubadilisha sarafu kwenye tawi la BoT la Arusha.

Jiji la Arusha linamzunguko mkubwa wa fedha za kigeni kutokana na kuwa kitovu cha sekta ya utalii na biashara ya vito.

Gavana Florens Luoga aeleza sababu ya kutumiwa kwa jeshi

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof Florens Luoga ameandaa kikao na wanahabari jijini Arusha kufafanua kuhusu sababu ya kutumiwa kwa wanajeshi katika operesheni hiyo.

Amesema ukaguzi ukaguzi huo katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha jijini Arusha uliendeshwa na Benki yake kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vya dola ili kubaini watuhumiwa wa uhalifu wa kutakatisha fedha.

Ameeleza kuwa kufuatia askari wengi wa Jeshi la Polisi kuwa katika usimamizi wa mitihani ya kidato cha pili, taasisi yake ilihusisha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wasio na silaha ili kuongeza nguvu katika kufanikisha zoezi hilo.

Prof Luoga amesema kuwa watuhumiwa waliokamatwa katika zoezi hilo wanahojiwa na hatua za kisheria zitachukua mkondo wake.

Sababu ya operesheni kufanyika Arusha

Gavana wa BoT amesema operesheni ya kushtukiza ya kukagua maduka ya ubadilishaji fedha na baadhi ya maduka bubu Arusha ilifanyika kutokana na maafisa wa serikali kubaini kwamba wafanyabiashara hutumia njia mbalimbali kukwepa mkono wa sheria.

Msako huo ulipangwa na Kitengo cha Ukaguzi cha Benki Kuu na ulifanywa baada ya misako mingine miwili kufanyika awali, lakini bila mafanikio makubwa.

Uchunguzi wa kina katika miezi sita iliyopita ulibaini kuongezeka kwa biashara za kubadilisha fedha kinyume cha sheria, na kukua kwa biashara haramu ya fedha za kigeni na utakatishaji fedha, hususan kupitia maduka ya kubadilisha fedha, amesema Prof Luoga. "Juhudi za Kitengo cha Ukaguzi kuwapata wahusika hazikuzaa matunda katika oparesheni mbili zilizopita," ameeleza.

"Hii ni kwa sababu iligundulika kuwa kuna mtandao mpana na madhubuti wa shughuli hizo na ambao ulilenga kuhakikisha kuwa shughuli za udhibiti hazifanikiwi. Baada ya mashauriano na wataalam na kushirikisha vyombo vya upelelezi na usimamizi ilionekana kuwa ili kufanikisha zoezi lililokusudiwa ni muhimu wahusika wote wadhibitiwe kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi.

"Hii ilihitaji ushiriki wa maafisa wengi sana kutoka vyombo mbalimbali na kuhakikisha kila mahali ambapo ukaguzi uliendeshwa kuna usalama wa kutosha na Wananchi wanaarifiwa liarifiwa] kutoingia sehemu husika kwa wakati huo."

Maduka kufungwa

Benki Kuu ya tanzania imesema uchunguzi uliofanyika umebaini waendeshaji wengi wa maduka ya kubadilisha fedha hawakukidhi vigezo vyote japokuwa leseni zilitolewa kwao baada ya taarifa kupotoshwa.

"Hao wote watapewa notisi ya kusitisha leseni na maduka yao kufungwa. Yeyote ambaye anajua kuwa upatikanaji wa leseni yake una dosari anashauriwa kurejesha leseni hiyo kwa hiari," amesemaProf Luoga.

"Wale ambao wanaendesha maduka ya kubadilisha fedha bila leseni au kwa kutumia leseni zisizo zao wanatakiwa kufunga maduka hayo mara moja kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii