Watu waliojihami wamteka mfanyakazi wa shirika la misaada pwani ya Kenya

RAMANI

Kundi la watu wasiojulikana waliojihami wamemteka mwanamke mfanyakazi wa shirika la misaada, raia wa Italia kutoka kusini mashariki mwa Kenya, Polisi inasema.

Wanaume hao wanaoarifiwa kujihami kwa bunduki, "wamefyetua risasi kiholela" kabla ya kumteka msaidizi huyo mwenye umri wa miaka 23 nje ya mji wa pwani Malindi.

Watu watano pia wanaarifiwa kujeruhiwa na wamepelekwa hospitalini, mmoja kati yao akiwa yuko katika hali mahututi.

Haijajulikana wazi ni kwanini shambulio hilo limetokea na waliolitekeleza ni akina nani, polisi wanasema.

Hatahivyo, polisi imeeleza kwamba wanalichukulia tukio hilo, lililotokea mwendo wa saa mbili Jumanne usiku kama la kigaidi.

Katika ujumbe kwenye Twitter, idara ya Polisi nchini imesema wanaume hao walikuwa wamebebea bunduki aina ya AK47 walizozitumia kulivamia jumba la kibiashara la Chakama katika kaunti ya Kilifi pwani ya Kenya nje kidogo ya mji wa Malindi.

Polisi kwa sasa wametawanywa kuwasaka wahalifu hao.

Lakini kuna hofu kuwa shambulizi hilo liliendeshwa na wanamgambo Al Shabaab. Mwaka 2011 Al Shabaab walimuua mtalii raia wa Uingereza na wakamteka nyara mke wake kwenye mji wa pwani ya Kenya wa Lamu.

Kundi hilo pia linadaiwa kuwateka wanawake wawili raia wa Uhispania kwenye kambiaya Dadaab mwaka huo huo hatua ambayo ilisababisha Kenya kutuma wanajeshi wake kwenda nchini Somalia ambapo wamesalia hadi leo.

Kiongozi wa vijana katika taarafa ya Chakarama Chadi Joshua Kazungu, anasema majambazi hao waliofika mwendo wa saa moja usiku na kuvamia makao ya raia wa Italia, walikuwa na mavazi yaliyofanana na wanamgambo wa kisomali na walikuwa wamejihami kwa bunduki.

"Walipofika hapa wakafyatua risasi ili wanakijiji watoroke na tukatoroka. Baada ya kama dakika mbili hivi tukaskia yule mtaliano akilia akisema nisaidieni, lakini wakati tukiwa tunaenda tukapata vina wanne wakikuwa tayari wamevunjwa miguu na pia tukapata mama mmoja amepigwa risasi kifuani na ameanguka," alisema Kazungu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii